Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga ilivyomuachia mzigo Mabedi, ishu ipi hivi...

CAF Pict


HII ni wikiendi iliyobeba ujazo wa kutosha kwa upande wa wapenda soka. Si Tanzania pekee, bali hadi nje ya mipaka kwani ni burudani bandika bandua.


Jana Ijumaa, tulishuhudia Azam FC ikirudiana na KMKM katika mechi ya kihistoria katika Kombe la Shirikisho Afrika ambayo timu hizo kila moja ilikuwa inaisaka nafasi ya makundi kwa mara ya kwanza.


Sasa leo Jumamosi, hapa nchini kuna mechi mbili za CAF, Yanga vs Silver Strikers saa 11:00 jioni na Singida Black vs Flambeau saa 1:00 usiku. Pia kuna mitanange mitatu ya Ligi Kuu Bara, Mashujaa vs Namungo saa 8:00 mchana, Fountain Gate vs KMC saa 10:00 jioni na Dodoma Jiji vs Pamba Jiji saa 1:00 usiku.

Nje ya mipaka ya Tanzania kwa maana ya Ulaya, ligi ambazo ni pendwa zaidi na maarufu ni England, Hispania, Ufaransa, Italia na Ujerumani kuna mechi zinapigwa wikiendi hii.

Kubwa zaidi, kesho Jumapili kuna El Clasico, Real Madrid itaikaribisha Barcelona kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu saa 12:15 jioni.

CA 01

MABEDI TUMAINI LA YANGA

Baada ya kipigo cha bao 1-0 ilichopokea Yanga ugenini dhidi ya Silver Strikers, klabu hiyo ikasitisha mkataba wa Kocha Mkuu, Romain Folz.

Sasa Yanga inakwenda kurudiana na Silver Strikers ikiwa inanolewa na Kaimu Kocha Mkuu, Patrick Mabedi ambaye amekabidhiwa kikosi hicho akiachiwa msala wa kuipeleka timu makundi.

Mabedi ndiye alikuwa msaidizi wa Folz katika mechi hiyo ya kwanza na alitambulishwa Oktoba 13, 2025, siku tano kabla ya mechi hiyo akichukua nafasi ya Manu Rodriguez, aliyewasilisha barua ya kuomba kuvunja mkataba wake baada ya kupata changamoto ya kiafya.

Yanga inafahamu ina deni kubwa kwa mashabiki nalo ni kufuzu makundi, ikifanya hivyo itakuwa ni mara ya nne mfululizo katika mashindano ya CAF baada ya 2022-2023 (Kombe la Shirikisho), 2023-2024 (Ligi ya Mabingwa) na 2024-2025 (Ligi ya Mabingwa).

Tayari Mabedi ametema cheche kuelekea mechi hiyo akisema anaingia na mambo mawili, kwanza kucheza kwa tahadhari ya kutoruhusu bao na kushambulia kwa kasi, pili kutumia kila nafasi ili kufunga mabao ya kutosha.

Mabedi raia wa Malawi, anafahamu ili Yanga ifuzu makundi, lazima washinde kwa angalau tofauti ya mabao 2-0 baada ya ugenini kufungwa 1-0, amesema: "Mechi ya ugenini hatukuwa na nidhamu nzuri sana kwenye ulinzi ndiyo maana tuliruhusu lile bao, nimewaambia wachezaji wasirudie makosa yale, hii ni timu kubwa (Yanga) na wao ni wachezaji wakubwa.

"Tunatakiwa kucheza kwa nidhamu lakini wawe wakatili kutoruhusu wapinzani kujipanga na hata kukaribia lango letu, kama tutaruhusu bao tutazidi kujiweka kwenye presha."

Mabedi aliongeza: "Tupo nyumbani, tutakuwa mbele ya mashabiki wetu tunaoamini watajaa uwanja mzima, tunatakiwa kuipigania klabu yetu, hapo ni muhimu kutangulia kupata mabao ya haraka.

"Tunatakiwa kuhakikisha tunakuwa na njaa ya kumalizia nafasi ambazo tutazingeneza, mpinzani anapofanya makosa tunatakiwa kumwadhibu na sio kumfanya ajipange upya.

"Hizi ni mechi kubwa, hatutakiwi kuidharau Silver Strikers, ina kocha na wachezaji wazuri lakini Yanga inaweza kuonyesha kuwa bora zaidi kwenye mchezo huu wa nyumbani ambao utaamua hatma yetu, tunatakiwa kumaliza mechi mapema."

Yanga ambayo awali ilitangaza viingilio vya mechi hiyo, baadae ilibadili mambo na kusema hakutakuwa na kiingilio, hivyo mashabiki wataingia bure lengo likiwa ni kuujaza uwanja na kutoa sapoti ya kutosha ili timu ifikie malengo ya kufuzu makundi.

Kocha wa Silver Strikers, Etson Kadenge Mwafulirwa, ataendelea kutumia silaha zake zilizompa ushindi nyumbani mechi ya kwanza akiwemo Ernest Petro, Andrew Joseph, McDonald Lameck, Uchizi Vunga.

Lakini pia Yanga itakuwa na kazi ya ziada kuipenya ngome ya Silver Strikers ikiongozwa na Nickson Mwase na Maxwell Paipi. Golini akikaa George Chikooka.

CA 04

MZUKA WA MZIZE

Kuelekea mechi hiyo, taarifa njema ni Clement Mzize amerejea na huenda akaanza kutokana na hivi sasa kuwa fiti. Hali hiyo moja kwa moja itabadili kikosi na kuwa tofauti na kile kilichocheza mechi ya ugenini.

Mzize aliyekuwa mshambuliaji kinara wa mabao Yanga msimu uliopita, msimu huu amecheza mechi moja pekee ya kimataifa kati ya tatu.

Mzize aliyepata majeraha katika mechi ya kwanza dhidi ya Wiliete iliyochezwa Septemba 19, 2025 nchini Angola, alikosekana katika mechi nne za mashindano dhidi ya Pamba Jiji (Septemba 24, 2025), Wiliete (Septemba 27, 2025), Mbeya City (Septemba 30, 2025) na Silver Strikers (Oktoba 18, 2025).

Nyota huyo aliyeibuka kinara wa mabao ndani ya kikosi cha Yanga katika Ligi Kuu Bara msimu uliopita akifunga 14, mawili nyuma ya kinara wa jumla, Jean Charles Ahoua, amekuwa na mchango mkubwa anapopata nafasi ya kuwepo kikosini kutokana na kasi na uwezo alionao wa kutokea pembeni akitengeneza nafasi kwa wenzake na kufunga mwenyewe.

Kwa mujibu wa Mabedi ambaye ametangaza kuingia uwanjani kwa kushambulia kwa kasi, moja kwa moja Mzize inampa nafasi ya kuanza kikosini kwake.

Kama Mzize ataanza, maana yake kuna mchezaji mmoja atasubiri. Kumbuka tangu kuanza kwa msimu huu, Yanga imekuwa ikisimamisha mshambuliaji mmoja, Andy Boyeli au Prince Dube, kisha Mzize huwa anatokea pembeni.

Kuwepo kwa Mzize, tunaweza kushuhudia Mohamed Doumbia au Mudathir Yahya ambao walianza mechi za karibuni wakisubiri benchi.

Kule eneo la mbele la ushambuliaji ukimtoa mchezaji anayecheza namba nane, linaweza kuonekana hivi; winga Mzize na Maxi Nzengeli, Pacome Zouzoua akiwa namba 10, kisha namba tisa ni Boyeli au Dube.


WABENIN KUAMUA

Shirikisho la Soka Afrika (CAF), limewatangaza waamuzi kutoka Benin ndiyo watakaochezesha mechi ya Yanga dhidi ya Silver Strikers.

Katika mechi hiyo, mwamuzi wa kati atakuwa Adissa Abdul Raphiou Ligali kutoka Benin kama ilivyo kwa msaidizi wake namba moja, Lucien Todégnon Hontonnou. Lamien Dofinte Adolphe anayetokea Burkina Faso ni msaidizi namba mbili.

Mwamuzi wa akiba (Fourth Official) atakuwa Dedjinnanchi Tanisla Ahomlanto Dedjinnand wa Benin, wakati kamishna wa mechi ni Ahmad Nazeer Hossen Bowud (Mauritius) na mtathimini waamuzi ni Andriamparany Lova Rakotoarimanana (Madagascar).

Rekodi zinaonyesha, Adissa Ligali alichezesha mechi moja pekee ya Kundi A katika michuano ya CHAN 2024 iliyofanyika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda mwaka 2025, iliyochezwa Agosti 10, 2025 kwenye Uwanja wa Nyayo nchini Kenya, Angola ikiichapa Zambia mabao 2-1.

Katika msimu wa mashindano 2023-2024, mwamuzi huyo alichezesha jumla ya mechi 11 zikiwamo za kufuzu Kombe la Dunia, CHAN, AFCON na Kombe la Shirikisho Afrika. Jumla ya kadi 41 za njano alitoa katika mechi hizo ikiwa ni wastani wa 3.7. Kadi nyekundu ni moja pekee.

CA 02

MSAKO WA REKODI SINGIDA BLACK STARS

Zimebaki dakika tisini za Singida Black Stars inayofundishwa na Miguel Gamondi kuandika rekodi kama ya Namungo iliyoiweka msimu wa 2020-2021 katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Kwa sasa ukiitoa Simba na Yanga zenye rekodi nzuri ya kucheza hatua ya makundi ya michuano ya CAF, hakuna klabu nyingine ya Tanzania tangu mwaka 2004 ilipoanzishwa Kombe la Shirikisho Afrika iliyowahi kucheza hatua hiyo zaidi ya Namungo.

Kumbuka Kombe la Shirikisho Afrika, ni michuano iliyoanzishwa mwaka 2004 baada ya CAF kuyaunganisha mashindano mawili, African Cup Winners' Cup yaliyoanzishwa mwaka 1975 na CAF Cup ya mwaka 1992, ndipo ikazaliwa yenyewe.

Rekodi ambayo Singida Black Stars inaifukuzia ni kama ile iliyowekwa na Namungo msimu wa 2020–2021 na ilishiriki Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza na kufika hadi makundi licha ya kwamba haikuendelea zaidi ya hapo ikimaliza mkiani bila pointi.

CA 03

Timu ambazo zimeshiriki michuano hiyo mbali na Simba na Yanga ni KMC (2019–2020), Mtibwa Sugar (2018-2019), Biashara United (2021–2022), Geita Gold (2022-2023), Singida Fountain Gate (2023-2024), Coastal Union (2024-2025) na Azam iliyowahi kushiriki mara nane.

Sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya Flambeau du Centre, kwa namna moja ama nyingine imekuwa na faida kwa Singida Black Stars inayonolewa na Gamondi, kocha ambaye katika misimu miwili aliyoifundisha Yanga, aliifikisha timu hiyo hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara zote, huku moja akienda nayo hadi robo fainali.

Hata hivyo, Flambeau du Centre nao sio wanyonge, kwani hii ikiwa ni mara ya pili wanashiriki mashindano ya kimataifa baada ya mwaka 2022 kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika, walifanya vizuri hatua ya awali kwa kuiondosha Al Akhdar ya Libya kwa mabao 4-3. Singida Black Stars iliitoa Rayon Sports kwa mabao 3-1 na ilianzia pia ugenini kama hivi ikashinda 1-0, nyumbani ikashinda 2-1.

"Uwekezaji na utayari ndiyo siri kubwa ya kufanya vizuri kwenye michuano hii ya kimataifa, naona Singida Black Stars ikifanya vizuri hasa tukifanikiwa kutinga hatua ya makundi mchezo wetu wa nyumbani, wachezaji wangu wana utayari na nina bahati kuwa na kikosi chenye wachezaji wengi wazoefu," alisema Gamondi.

Clatous Chama na Khalid Aucho wenye rekodi nzuri na timu za Tanzania kufika mbali michuano ya kimataifa, ni tumaini la Singida Black Stars kutoboa.

Chama ameendelea kuwa mchezaji muhimu wa kikosi hicho, akifunga bao katika sare ya ugenini dhidi ya Flambeau, huku pia mechi ya ugenini hatua ya awali dhidi ya Rayon, alitoa asisti ya bao lililofungwa na Marouf Tchakei.