Yanga imeonyesha njia soka la watoto
Muktasari:
- Huko nyuma Yanga na Simba zilishakuwa na timu za watoto na vijana, maarufu kama Yanga Kids na Simba Kids na Yanga B na Simba B, zilizokuwa za wachezaji waliokuwa wameshapikwa, lakini hawajawa tayari kupambana katika vikosi vya kwanza.
INAWEZA kuwa si klabu ya kwanza na wala ya si mara ya kwanza kuanzishwa kwa Shule ya Soka, lakini uamuzi uliofanywa na uongozi wa Yanga kuanzisha kituo cha mafunzo kwa watoto wenye umri chini ya miaka 15 hauna budi kusifiwa na kupongezwa na mpenda soka yeyote.
Huko nyuma Yanga na Simba zilishakuwa na timu za watoto na vijana, maarufu kama Yanga Kids na Simba Kids na Yanga B na Simba B, zilizokuwa za wachezaji waliokuwa wameshapikwa, lakini hawajawa tayari kupambana katika vikosi vya kwanza.
Klabu kama Azam FC imekuwa ni utamaduni wake kulea watoto na vijana na kuwapeleka timu nyingine kwa mkopo, ili wapate uzoefu wa kupambana na baadaye kurudishwa au kuuzwa pale inapoona haina nafasi kwa mchezaji aliyehitimu mafunzo kituoni kwake.
Tabora kulikuwa na kituo cha Chipukizi kilichowalea watoto kuanzia umri chini ya miaka 12 hadi timu ya vijana, hivyo kuchangia maendeleo ya klabu nyingi za mikoa ya kanda ya Magharibi.
Hivi sasa kuna kituo cha Magnet ambacho kina watoto wa umri tofauti na vijana. Hapo hujazungumzia Alliance, Fountain Gate na vituo vingine.
Hata hivyo, uamuzi wa uongozi wa Yanga kuanzisha shule ya watoto kwa mafunzo ya mpira wa miguu, una mashiko yake katika maendeleo ya mpira wa miguu nchini.
Yanga na Simba ndizo klabu zinazoangaliwa zaidi na wadau wote wa mpira wa miguu. Kama klabu hizi zinafanya kitu cha maendeleo, ni rahisi sana kwa klabu nyingine au wadau kuiga na kama zikifanya kitu cha kipuuzi, ni rahisi sana kuvuruga soka la Tanzania.
Binafsi nimekuwa nikiandika sana kuhusu umuhimu wa Shirikisho la Soka (TFF) kulazimisha klabu za Ligi Kuu na Championship kuanzisha timu za watoto kama fidia ya maendeleo ya soka baada ya kuziruhusu kusajili hadi wachezaji 12 wa kigeni.
Wengi wanaona ujio wa wachezaji wengi wa kigeni utasababisha kuweka ushindani kwa wachezaji wazawa na hivyo kukuza kiwango chao. Lakini si dhana sahihi.
Kama klabu inamleta mchezaji kama Aziz Ki ambaye amekulia katika shule ya soka, unategemeaje mchezaji mzawa ambaye hajakulia katika shule ya soka ashindane naye ili akuze kiwango chake? Jibu ni huwezi kutegemea ushindani mzuri.
Mmoja atakuwa amepikwa vizuri na mwingine hakukutana na mwalimu sahihi wa mpira wa miguu katika umri mdogo na hivyo ameshajenga mazoea ambayo ni shida kuyaacha ukubwani. Anaweaza kupambana naye uwanjani, lakini hawezi kuwa na maono ya kiwango cha juu uwanjani.
Wapo wachezaji wachache wanaoweza kupambana kama Feisal Salum, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na Dickson Job, lakini huwezi kuwa na kundi kubwa la wachezaji wa kiwango hicho cha kupambana na wachezaji waliopata mafunzo sahihi katika umri mdogo.
Kwa hiyo dawa ya kuwezesha wazawa kupambana na wachezaji waliokuzwa kisoka ni kulazimisha klabu kubwa kuanzisha timu za watoto badala ya hizi za vijana wa chini ya miaka 20 au 17 kwa kuwa nao tayari wameshakosa mafunzo sahihi katika umri mdogo.
Hii inawezekana na kuthibitisha kuwa inawezekana Yanga wameanzisha shule ya mpira wa miguu ya watoto wa umri chini ya miaka 15, 12 na 11 na ili iweze kujiendesha imeweka kiingilio cha Sh600,000 na ada ya kila mwezi ya Sh400,000, ambazo baadhi wameanza kulalamikia kuwa ni kiwango kikubwa kwa mchezo ambao unachezwa zaidi na maskini.
Ni kweli nyota wengi wa mpira wa miguu wametokea katika familia maskini, lakini si kweli kwamba viongozi wa kituo watashindwa kumchukua mchezaji ambaye ataonekana ana uwezo wa kuwa nyota mkubwa wa baadaye, si hapa nchini tu bali Afrika na duniani.
Tumeona hivyo kwa klabu kubwa kama Barcelona ambayo ilimchukua Lionel Messi akiwa kinda, ikamuhamishia Ulaya pamoja na familia yake na ameandika historia ya kuwa mmoja wa wachezaji bora kuwahi kutokea duniani.
Kwa hiyo, kama TFF ilikuwa inahofia kuwa klabu za Ligi Kuu na Championship zitashindwa kulea watoto wadogo, Yanga imeonyesha mfano kwa kuanzisha na kuweka ada kama hiyo, ikijua kuwa kutokana na chapa yake, wazazi wengi watakimbilia kupeleka watoto wao kwenye klabu ambayo wanaijua na ambayo ina fursa nyingi.
Hili pia ni sharti la leseni za klabu linalotakiwa kuingizwa kwenye kanuni baada ya mamlaka za soka kujadiliana kwa kina na wamiliki wa klabu kuangalia uendeshaji wa shule za soka kwa watoto na vijana.
TFF na Bodi ya Ligi (TPLB) kutokuwa na uwezo wa kujua taarifa za fedha za klabu inaweza kuwa ni kikwazo kingine. Kama klabu zinafikia bajeti ya hadi Sh6 bilioni, kuna umuhimu mkubwa kwa mamlaka hizo kuwa na kanuni itakayozipa nguvu ya kujua matumizi ya klabu ili iweke sharti katika kanuni za fedha kuwa asilimia fulani ya mapato iende katika maendeleo, na hasa mafunzo kwa watoto na vijana.
Azam ilishaonyesha njia, lakini kwa utamaduni na fikra za Watanzania haikuwa rahisi kuona njia hiyo. Sasa Yanga imeonyesha njia na hakuna sababu tena ya TFF na TPLB kuhofia kuwa timu za watoto hazitawezekana kwa klabu za Ligi Kuu. Ni suala la kukaa na wamiliki na waendeshaji wa klabu kujadili suala hilo litawezekanaje.
Hakuna nchi ambayo imetwaa Kombe la Dunia bila ya kuwa na program za soka la watoto (grassroot football). Hispania ilikuwa inatamba na klabu zake kubwa za Real Madrid na Barcelona, lakini duniani haikuwahi kutamba hadi kizazi cha kina Iniesta kilipohitimu shule za soka na kupata nafasi kwenye timu ya taifa.
Tunahitaji kufuata mfano wa Yanga kwa kuweka soka la watoto kama lazima kwa kutumia kanuni za leseni za klabu.