AK 47 aingia studio, ngumi zabaki kazi kuu
Muktasari:
- Akizungumza na Mwanaspoti Tony alisema muziki ni moja ya vitu anavyovipenda na amekuwa akitumia muda wa ziada kwenda studio hiyo, ambapo mbali na kuimba pia hupata nafasi ya kujifunza mambo mbalimbali yanayomsaidia kupanua mawazo yake nje ya ulingo.
BONDIA wa Tanzania, Tony Rashid maarufu ‘AK 47’, amesema pamoja na kutumia muda wake mwingi kwenye mazoezi na maandalizi ya mapambano, anapopata nafasi huenda studio ya rafiki yake Kush kwa ajili ya kuimba na kujifunza mambo mengine nje ya mchezo wa ngumi.
Akizungumza na Mwanaspoti Tony alisema muziki ni moja ya vitu anavyovipenda na amekuwa akitumia muda wa ziada kwenda studio hiyo, ambapo mbali na kuimba pia hupata nafasi ya kujifunza mambo mbalimbali yanayomsaidia kupanua mawazo yake nje ya ulingo.
“Napenda muziki, kwa hiyo nikishapata muda huwa naenda studio kwa rafiki yangu Kush. Naingia kuimba na pia kujifunza mambo mengine tofauti na ngumi,” alisema Tony.
Bondia huyo alisema kufanya shughuli nyingine nje ya ngumi hakumaanishi anapunguza umakini wake katika mchezo huo, bali kwake ni sehemu ya kutumia vipaji na muda wake vizuri wakati ambao hana majukumu ya mazoezi au mapambano.
Tony ni miongoni mwa mabondia wenye uzoefu nchini na amewahi kutwaa ubingwa wa African Boxing Union (ABU) katika uzito wa super bantamweight.
BoxRec inaonyesha alitwaa mkanda huo Septemba 15, 2019 baada ya kumshinda Siboniso Gonya kwa TKO raundi ya 10.
Tony ana rekodi ya mapambano 24, akishinda 17, vipigo vinne na sare tatu, huku akiwa ameshinda baadhi ya mapambano yake kwa njia ya KO/TKO.
Katika pambano hilo la mwisho lililoonyeshwa kwenye rekodi hizo, Tony alipoteza kwa uamuzi wa majaji dhidi ya Asanda Gingqi nchini Afrika Kusini. Kabla yake alikuwa ameshinda mapambano matatu mfululizo dhidi ya Twalib Tuwa, Oscar Duge na Bright Nazaidi.