Ally Salim aanza tizi Dodoma
Muktasari:
- Salim kabla ya kuumia dhidi ya Mbeya City, mechi iliyopigwa Uwanja wa Sokoine, Feb 3, 2026 alikuwa na cleansheets tano, tofauti na cleansheets mbili alizomamaliza nazo msimu wa 2024/25 akiwa na Simba ambako alikuwa anasubili benchi mbele ya Moussa Camara aliyemaliza na cleansheets 19 kabla ya msimu huu kuondolewa katika mfumo wa usajili kutokana na kuuguza majeraha.
KIPA wa Dodoma Jiji, Ally Salim amesema anaendelea na programu ya mazoezi magumu ya gym, ili kujiweka tayari kuungana na wachezaji wenzake baada ya kupona majeraha yaliyomuweka nje kwa muda mrefu.
Salim kabla ya kuumia dhidi ya Mbeya City, mechi iliyopigwa Uwanja wa Sokoine, Feb 3, 2026 alikuwa na cleansheets tano, tofauti na cleansheets mbili alizomamaliza nazo msimu wa 2024/25 akiwa na Simba ambako alikuwa anasubili benchi mbele ya Moussa Camara aliyemaliza na cleansheets 19 kabla ya msimu huu kuondolewa katika mfumo wa usajili kutokana na kuuguza majeraha.
Salim alisema tayari amerejea kambini, lakini wakati wenzake wanapewa mapumziko ya wiki moja kutokana na Ligi Kuu kusimama kupisha kalenda ya FIFA kwa Taifa Stars kucheza mechi mbili za kirafiki za kimataifa dhidi ya Rwanda na Uganda, yeye aliamua kuutumia muda huo kujifua na mazoezi magumu.
"Mimi nilibakia kambini kwa lengo la kuendelea na programu ya mazoezi magumu wachezaji wenzangu wakirejea wanikute nipo fiti kuliko kuanza moja, mchezaji anapokaa nje muda mrefu anakuwa hayupo fiti na kujiamini kunapungua, hivyo nafanya bidii ya kuhakikisha nakuwa sawa," alisema Salim na kuongeza;
"Ingawa msimu huu niliuanza vizuri ila kwa bahati mbaya majeraha yamenitibulia, lakini hayawezi kunikatisha tamaa, mpira ni kazi yangu, najipanga kama nitapata muda wa kucheza mechi hata mbili za mwisho sawa na kama sitapata pia najiweka sawa kwa ajili ya msimu mpya."
Alisema japokuwa alikuwa nje ya kazi hiyo, hakukumzuia kufuatilia Ligi Kuu aliyoiona ina ushindani mkubwa na ilipofikia presha ipo juu kwa timu zinazowania ubingwa na zile zinazojikwamua na kushuka daraja.