Balaa la Sopu, Nado usipime Azam
Muktasari:
- Katika mechi tatu za ligi msimu huu, Sopu na Nado ndio wameonyesha matumaini makubwa kwa kikosi hicho cha Kocha Florent Ibenge kuwa na mchango mkubwa wa mabao.
VIWANGO bora vinavyoonyeshwa na wachezaji wa Azam FC, Abdul Suleiman ‘Sopu’ na Idd Seleman ‘Nado’ vimeanza kutoa mwanga mpya kwa kikosi hicho katika harakati za kusaka taji la Ligi Kuu Bara, baada ya kuchukua mara ya mwisho 2013-2014.
Katika mechi tatu za ligi msimu huu, Sopu na Nado ndio wameonyesha matumaini makubwa kwa kikosi hicho cha Kocha Florent Ibenge kuwa na mchango mkubwa wa mabao.
Azam katika mechi tatu ikishinda mbili na sare moja, Sopu amefunga mabao matatu, kwa maana ana wastani wa bao kila mechi, huku Nado akifunga moja na moja.
Nyota hao ambao wameongeza mikataba hadi Juni 30, 2028, wameonyesha kwa nini mabosi hawajakosea kuwaongezea kutokana na viwango wanavyoonyesha.
Katika mabao matano yaliyofungwa na Azam, Sopu amefunga matatu akiwa ndiye anayeongoza kwenye vita ya ufungaji bora, akiwa sawa na Mzambia Obrey Chirwa wa Geita Gold, huku kwa Nado akichangia mawili baada ya kufunga moja na kuasiti moja.
Nyota mwingine wa Azam FC aliyechangia mabao ni winga, Mkongomani Henoc Molia aliyefunga moja hadi sasa la Ligi Kuu Bara tangu atue Julai 18, 2026, akitokea FC Saint-Eloi Lupopo ya kwao DR Congo. Kwa upande wa eneo la kujilinda, nyota aliyechangia bao msimu huu katika kikosi hicho ni beki wa kushoto, Pascal Msindo aliyetoa asisti moja kwenye ushindi wa timu hiyo wa mabao 2-1 dhidi ya TRA United, mechi iliyopigwa Agosti 20, 2026.
Akizungumza, Ibenge alisema mwenendo wa kikosi hicho kiujumla bado sio wa kuridhisha kutokana na ushindani uliopo, ingawa kinachofanyika kwa sasa ni matokeo ya kujua malengo ya timu.
“Tuna wachezaji wengi wazuri ambao wanahitaji muda kuzoeana na wengine, Ligi Kuu ni ngumu na ili kupata ubora wao wote wanahitaji kuingia kikosini taratibu, wanaofanya vizuri wanajuana kwa sababu wako pamoja muda mrefu,” alisema Ibenge.