Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

BMT wapongeza ujio wa kocha mbobevu wa kuogelea

BMT Pict

Muktasari:

  • Kocha Lee, ambaye ana uzoefu mkubwa wa kufundisha waogeleaji katika ngazi za NCAA na Olimpiki, ataongoza programu maalumu ya maendeleo ya uogeleaji katika Shule ya Kimataifa ya Monti jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuboresha viwango vya ushindani wa Tanzania kwenye mashindano ya kimataifa na kuweka msingi wa maendeleo endelevu ya mchezo huo.

BARAZA la Michezo la Taifa (BMT), limesema ujio wa kocha wa kimataifa wa mchezo wa kuogelea, Ben Lee kutoka Marekani ni fursa kubwa kwa makocha na waogeleaji wazawa kujifunza ujuzi wa viwango vya kimataifa katika mchezo huo hivyo wanapaswa kuhudhuria mafunzo maalumu yatakayotolewa kwa muda wa wiki tatu.

Kocha Lee, ambaye ana uzoefu mkubwa wa kufundisha waogeleaji katika ngazi za NCAA na Olimpiki, ataongoza programu maalumu ya maendeleo ya uogeleaji katika Shule ya Kimataifa ya Monti jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuboresha viwango vya ushindani wa Tanzania kwenye mashindano ya kimataifa na kuweka msingi wa maendeleo endelevu ya mchezo huo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika mapokezi ya kocha huyo jijini Dar es Salaam, Afisa Michezo wa BMT, Petro Gallos mbali na kupongeza ujio wake, amesema wakufunzi wa ndani wa mchezo huo wanapaswa kutumia mwanya huo adhimu kwa kuchota ujuzi wenye manufaa.

BM 01

Naye Mkurugenzi wa Ufundi wa Chama cha Uogeleaji Tanzania (TSA), Amina Mfaume, amesema: "Mafunzo yatakayotolewa na kocha huyu yataongeza ufanisi wa makocha wetu na kutusaidia kuangalia maendeleo ya waogeleaji kwani wale watakaoshiriki wataona jinsi gani makocha wa kimataifa wanavyofanya mafunzo yao.”

Aidha, Mkurugenzi wa Shule ya Kimataifa ya Monti ambao ndio waandaaji wa mafunzo hayo, Fatma Fernandez, amesema programu hiyo ni sehemu ya jitihada za kukuza vipaji vya waogeleaji wa Kitanzania na kuijenga Tanzania kuwa kitovu cha maendeleo ya mchezo wa uogeleaji katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Amesema ujio wa Lee umefika katika kipindi muhimu ambacho Tanzania inajiandaa kushiriki mashindano mbalimbali ya kimataifa, yakiwemo Mashindano ya CANA Zone 3, ambapo takribani waogeleaji 40 wanatarajiwa kuiwakilisha Tanzania.

"Hatutaki tu kuwaandaa waogeleaji kwa mashindano ya sasa, bali tunajenga mfumo wa muda mrefu utakaowezesha Tanzania kuzalisha waogeleaji wenye uwezo wa kushindana kimataifa. Ili kufanikisha hilo ni lazima tuwaimarishe pia makocha na kuwashirikisha wazazi katika safari ya maendeleo ya wanamichezo," amesema Fernandez.

Ameeleza kuwa programu hiyo imegawanywa katika maeneo matatu muhimu yanayowahusu makocha, waogeleaji na wazazi, kwa kuamini kuwa maendeleo ya mwanamichezo yanategemea ushirikiano wa wadau wote.

BM 02

Kwa mujibu wa ratiba ya programu hiyo, mafunzo kwa makocha yatafanyika kuanzia Julai 28 hadi Julai 30, 2026 yakifuatiwa na kambi za mafunzo kwa waogeleaji wa makundi mbalimbali ya umri, huku mafunzo ya juu yakihitimishwa Agosti 14, 2026.

Fernandez amesema mafunzo yatatolewa bure kwa makocha wote waliosajiliwa na Chama cha Uogeleaji Tanzania (TSA), licha ya gharama za kumleta kocha huyo wa kimataifa kugharamiwa kikamilifu na Shule ya Kimataifa ya Monti.

Ameongeza kuwa, mafunzo hayo yatafanyika katika bwawa la kisasa la kuogelea la Shule ya Kimataifa ya Monti, Mikocheni, kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 5:00 asubuhi kila siku.

Kwa upande wake kocha Ben Lee ambaye pia ni mwanzilishi wa taasisi ya RaceBetter, mbali na kushukuru kwa mapokezi makubwa, amesema ujio wake unalenga kusaidia kuendeleza vipaji vya wazawa kuanzia ngazi za chini na kuweka misingi kwa makocha na waogeleaji kupata mafanikio ya muda mrefu.