BMT yavuna Sh129 milioni nyota wapya wa kigeni Ligi Kuu
Muktasari:
- Kwa mujibu wa taratibu za baraza hilo,kila mchezaji wa kigeni akakayesajiliwa na klabu za hapa nchini atalazimika kulipiwa Dola 500 za Marekani.
Wakati wingi la wachezaji wa kigeni kusajili na klabu mbalimbali za Ligi Kuu Tanzania Bara likizidi kuongezeka msimu baada ya msimu,kwa Baraza la Michezo la Taifa(BMT)mambo ni mazuri,kwani limeingiza kitita cha dola elfu 49(Sh129.7 milioni)kupitia tozo.
Kwa mujibu wa taratibu za baraza hilo,kila mchezaji wa kigeni akakayesajiliwa na klabu za hapa nchini atalazimika kulipiwa Dola 500 za Marekani.
Pia mchezaji wa kigeni atakayehama timu moja kwenda nchini ndani ya Tanzania atalazimika kulipiwa Dola 1000 za Marekani.
Kwa mujibu wa kanuni za usajili za Ligi Kuu Tanzania Bara za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),klabu inaruhusiwa kusajili wachezaji wa kigeni wasiozidi 12.
Simba,Yanga, Azam FC na Singida Black Stars ndio klabu pekee miongoni mwa timu 16 zinazoshiriki ligi hiyo zilizokamilisha idadi ya wachezaji 12 wakigeni wanaruhusiwa kusajiliwa kwa mujibu wa kanunu.
Kwa upande mwingine,kwa mujibu wa sheria za BMT Kifungu cha 31(2)(c), maombi ya idhini ya kuajiri mchezaji au mtaalamu wa michezo kutoka nje ya nchi yana tozo ya Dola 500, na maombi hayo yanafanywa na klabu, chama au shirikisho linalomwajiri.
Kwa mujibu wa BMT, hakutakuwa na tozo nyingine yoyote ikiwa mchezaji ataendelea kusalia kwenye klabu yake, lakini kama ajiunga na nyingine ya hapa hapa nchini atatoza mara mbili ya tozo ya mwanzo na kuwa Dola 1000.
Kwa msimu huu, timu tisa kati ya 16 zimesajili wachezaji wa kigeni 49 kutoka mataifa mbali mbali.
Idadi hiyo inafanya BMT kukusanya Dola 49,000 sawa na Sh.129.7 milioni kupitia dirisha lililopita la usajili.
Yanga imesajili nyota sita wa kigeni katika msimu huu wa Ligi Kuu unaoendelea, akiwemo mshambuliaji Peter Shalulile.
Shalulie kabla ya kutua Yanga alikuwa akikipiga Mamelodi Sundowns ya Ligi Kuu Afrika Kusini,huko alifanikiwa kuibuka mfungaji bora kwa misimu mitatu.
Yanga pia imemsajili Cheikh Ibrahima Touré, mshambuliaji wa kati raia wa Senegal aliyekuwa akicheza Al-Jabalain FC ya Saudi Arabia.
Housseine Zakouani ni winga wa kulia raia wa Comoros,ambaye naye ametua Yanga msimu huu akitokea Al-Zulfi FC ya Saudi Arabia, pia yuko winga Albert Kangwanda, aliyejiunga na miamba hiyo akitokea Red Arrows FC.
Yanga pia imewaongeza Oumar Comara kutoka Golden Arrows ya Afrika Kusini, huku ikimtwaa Fred Ngoma kutoka na Olympique Club de Safi
Hii ina maana kwamba wachezaji hawa sita wanaigharimu Yanga kitita cha Dola 3000(Sh.7 milioni).
Wekundu wa Msimbazi, Simba nao hawakuacha kulitumia dirisha la usajili baada ya kushusha nyota wapya watano.
Usajili huo mpya ni Keletso Makgalwa, ambaye amesajiliwa kutoka Sekhukhune United FC ya kwao Afrika Kusini,Mnigeria Ibraheem Jabaar aliyetua kutoka Stellenbosch, pia ya Afrika Kusini, Ibrahim Doumbia kutoka AS Kôrôfina ya Mali na Serge Badjo, aliyesajiliwa kutoka MC Alger ya Algeria.
Wachezaji hao wanne wanaigharimu Simba Dola 2000(Sh.3.2 milioni).
Azam haikufanya mzaha katika dirisha hilo iliendelea kusuka kikosi chake kwa kuongeza wachezaji wapya kutoka mataifa mbalimbali.
Kiungo mshambuliaji Kipre Junior,alirejea katika kikosi hicho akitoke MC Alger kama ilivyo kuwa kwa Gibril Silla waliyemrejesha kikosini kutoka Al Ahly Benghazi ya Libya .
Wengine ni Henri Stanic,aliyesajiliwa kutoka Stellenbosch FC ya Afrika Kusini,Nathan Idumba,aliyetua Chamazi kutoka Cape Town City na Henoc Molia aliyejiunga na timu hiyo kutoka Saint Eloi Lupopo.
Azam ilimsainisha pia Hassan Mubiru kutoka SC Villa ya Uganda, Donovan Makoma kutoka Birkirkara ya Visiwa vya Malta.
Pia ilikamilisha usajili wa Taiwo Abdulrafiu kutoka Rivers United ya Nigeria, naye ni sehemu ya usajili huo.
John Mano anakamilisha orodha ya wachezaji tisa wa kigeni waliosajiliwa na Azam msimu huu.
Idadi hiyo ya wachezaji inaigharimu Azam Dola 4500(Sh.11 milioni).
Hii si fedha inayotokana na ada ya uhamisho wa mchezaji, mshahara wake au thamani ya dili. Ni tozo ya maombi ya idhini ya kuajiri mchezaji au mtaalamu wa michezo kutoka nje ya nchi.
BMT inaeleza wazi kwenye mfumo wake wa vibali kwamba klabu inayomwajiri mchezaji kutoka nje ndiyo inayoomba idhini hiyo, huku kiwango cha tozo kikiwa Dola 500.
Pia, BMT imeweka Dola 500 kama faini kwa klabu, chama au shirikisho litakalokiuka masharti ya kuajiri mchezaji au mtaalamu kutoka nje. Hii ni tofauti na Dola 500 ya maombi ya idhini.
Pamba Jiji imeongeza wachezaji saba wa kigeni ambao ni Steve Ochieng(Shabana FC), Nonyem Okorocha(Mlandege FC), John Ochieng, Morice Sichone(Gulf United FC),Idrisa Diomande(Singida BS), Malanga Mwaku(Singida BS) na Nathaniel Ndwangou(AS Stade Mandji).
Singida BS imesajili wachezaji saba wakigeni ambao ni Jonathan Sowah(Simba), Benjamin Tamim(Maghreb Fez), Marcel Canadi(Enosis Neon Paralimni FC),Dramane Kambou(FC Saint-Eloi Lupopo),Exauce Sagesse Nzaou(AS Otoho d'Oyo),Candidat Mapendo(AS Dauphins Noirs)na Seydou Sacko kutoka ASEC Mimosas.
Coastal imesajili mchezaji mmoja ambaye Steven Bulugu kutoka Nairobi City Stars FC ya Kenya.
TRA United imewasajili wachezaji nane wakigeni ambao ni Ani Prince Elijah(Police FC),Daniel Mgore(Dodoma Jiji),Venold Dzaba Kouakou (AS Otoho d'Oyo),Arnauvy Princide Mombouli (Dynamo FC de Douala),Thobias Otieno(Kenya Police FC,Bryson Wangai(Gor Mahia FC),Shariff Majabe(Bandari FC) na Franck Steve Belobo kutoka Canon Sportif de Yaounde.
Geita Gold yenyewe imefanikiwa kuwanasa wachezaji watano, Christopher Tebandeke(TRA United),Obrey Chirwa(Kagera Sugar),Kayode Bankole Iyanu(TS Galaxy FC),Franck Olivier Nya Tenke(Les Astres FC De Douala)na Fabrice Ngoy kutoka Namungo.
Kagera Sugar imesajili wanne wakiwemo Collins Maina(Fortune Sacco FC),Emmanuel Mvuyekule(Vision FC) na Ally Salum kutoka Kariobangi Sharks ya Kenya.