Dakika 90 za presha Ligi Kuu
Muktasari:
- Wakati msimu huu ulipoanza hadi kumalizika raundi ya nne, haijawahi kushuhudia Yanga, Simba na Azam zote zikicheza siku moja. Ilitokea mara tatu Yanga na Azam zikicheza siku moja, huku nyingine ilikuwa Simba na Azam nazo zikicheza siku moja kwenye viwanja tofauti.
KWA mara ya kwanza leo tunakwenda kushuhudia timu zilizomaliza nafasi tatu bora juu ya msimamo wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita, zikiwa uwanjani siku moja zikisaka pointi za kujiweka pazuri.
Wakati msimu huu ulipoanza hadi kumalizika raundi ya nne, haijawahi kushuhudia Yanga, Simba na Azam zote zikicheza siku moja. Ilitokea mara tatu Yanga na Azam zikicheza siku moja, huku nyingine ilikuwa Simba na Azam nazo zikicheza siku moja kwenye viwanja tofauti.
Haijawahi kuzikutanisha timu hizo uwanjani siku moja, lakini leo tunakwenda kushuhudia kitu hicho. Hivyo kuna dakika 90 za presha kubwa.
Huu ukiwa ni mzunguko wa tano wa Ligi Kuu Bara, leo kuna mechi tatu, huku presha kubwa ikiwa kwa wakongwe, Yanga na Simba ambao wanavimbiana pale kileleni mwa msimamo wote wakiwa na pointi 12, tofauti yao ni mabao pekee ambapo Yanga imefunga 13 na Simba saba. Kwenye kuruhusu zote zina mbili.
Timu hizo ambazo ndizo pekee zilizoshinda mechi zote nne za kwanza za Ligi Kuu Bara msimu huu, zinashuka dimbani kwenye viwanja tofauti.
FOUNTAIN GATE VS YANGA
Mabingwa watetezi Yanga itakuwa ugenini dhidi ya Fountain Gate leo saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Yanga inaingia kwenye mechi hiyo ikiwa na mwanzo mzuri baada ya kushinda mechi zote nne ilizocheza.
Ilianzia ugenini kuifunga Namungo 3-1, kisha ikarudi nyumbani na kuzifunga Coastal Union (4-1), JKT Tanzania (4-0) na Pamba Jiji (2-0).
Matokeo hayo yameifanya Yanga kuwa miongoni mwa timu zilizoonyesha kiwango bora mwanzo wa msimu, huku ikifunga mabao 13 na kuruhusu mawili pekee.
Hata hivyo, Fountain Gate itatumia faida ya kucheza nyumbani mbele ya mashabiki wake Arusha kujaribu kuzuia mwendo wa mabingwa hao na kusaka matokeo yatakayowapa pointi.
Fountain Gate haina mwendo mzuri kwenye ligi, baada ya msimu uliopita kumaliza nafasi ya 12, imeanza safari mpya kwa kusuasua na hadi sasa ina pointi tatu kutokana na kushinda mechi moja pekee ikiwa nafasi ya 12.
Timu hiyo ilianza kwa kichapo cha mabao 3-0 ugenini dhidi ya Singida Black Stars, ikarudi nyumbani kuichapa Mashujaa 1-0, ikaenda ugenini kwa Namungo ikafungwa 1-0, ikarudi nyumbani na kukubali kichapo cha 2-0 dhidi ya Mbeya City.
Ushindi pekee dhidi ya Mashujaa ndiyo umewapa pointi hali inayoonyesha timu hiyo haijaanza vizuri, hivyo ina kazi kubwa inapokabiliana na Yanga.
Rekodi zinaonyesha, Fountain Gate mbele ya Yanga haina makali. Timu hizo zimekutana mara nane tangu Fountain Gate ilipokuwa ikiitwa Singida Big Stars, kisha Singida Fountain Gate.
Katika mechi hizo nane, Yanga imeshinda zote na kupata clean sheet saba, huku ikifunga mabao 24 na kuruhusu moja pekee. Bao ililofunga Fountain ilikuwa ni mechi ya kwanza iliyomalizika kwa Yanga kushinda 4-1, ilikuwa Novemba 17, 2022.
Yanga leo inahitaji kupata ushindi mwingine ili kuendelea kukaa kileleni huku ikifahamu, kupoteza au kuambulia sare, kutatoa nafasi kwa Simba kupanda juu hapo baadaye itakaposhinda.
SIMBA VS GEITA GOLD
Baada ya Yanga kumalizana na Fountain Gate, saa 12:30 jioni Simba itakuwa mwenyeji wa Geita Gold kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo jijini Dar es Salaam.
Simba inaingia uwanjani ikiwa na morali baada ya mechi yake ya kwanza nyumbani kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union. Kabla ya hapo, ilishinda mechi tatu ugenini dhidi ya Kagera Sugar (2-0), Pamba Jiji (2-1) na Singida Black Stars (2-1).
Geita Gold, iliyopanda daraja, imekusanya pointi saba katika mechi nne. Hata hivyo, safari yake ya ugenini imekuwa ya ushindi na kipigo ikianza kuifunga Mbeya City 1-0, kisha kupoteza kwa idadi hiyo mbele ya Namungo. Nyumbani imeshinda 6-2 dhidi ya Kagera na sare ya 2-2 dhidi ya Azam.
Rekodi ya Geita dhidi ya Simba nayo si nzuri. Katika michezo sita ya Ligi Kuu iliyokutana, haijawahi kushinda zaidi ya kuambulia sare moja, huku Simba ikishinda mara tano.
Katika mechi hizo, Simba imefunga mabao 19 dhidi ya matatu ya Geita. Ushindi mkubwa zaidi ulikuwa wa mabao 5-0, Desemba 18, 2022, huku mchezo wao wa mwisho Mei 21, 2024 ukimalizika kwa Simba kushinda 4-1.
Simba itakuwa inaingia uwanjani ikiwa tayari inafahamu matokeo ya mtani wake, Yanga, hivyo kwao itakuwa na presha kubwa.
Kwa matokeo yoyote ambayo Yanga itakuwa imeyapata, Simba itahitaji ushindi wa lazima, kwani ikitokea Yanga imepoteza, Wekundu hao wa Msimbazi watataka kushinda ili kukaa kileleni, lakini kama Wanajangwani watashinda, basi itazidi kuwafanya vijana hao wa Steve Barker nao kusaka ushindi kwa namna yoyote ile ili kutowaacha mbali wapinzani katika mbio za ubingwa.
KAGERA SUGAR VS AZAM
Siku itafungwa kwa kushuhudia Azam itakayokuwa kwenye Uwanja wa Kaitaba ikiwakabili wenyeji Kagera Sugar kuanzia saa 2:30 usiku.
Azam chini ya Kocha Florent Ibenge, inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya sare ya 2-2 dhidi ya Geita Gold, matokeo yaliyoongeza umuhimu wa kutafuta ushindi leo.
Kagera Sugar, iliyorejea Ligi Kuu msimu huu, imeanza kwa kusuasua. Katika michezo minne, imepata sare moja ya 1-1 dhidi ya Singida Black Stars na kupoteza mitatu, ikifungwa 2-0 na Simba, kisha 6-2 na Geita Gold, ikaja kupasuka tena 2-1 kwa Mashujaa.
Azam imecheza michezo minne, ikishinda miwili na kutoka sare miwili. Mbali na sare ya 2-2 dhidi ya Geita Gold, ilitoka 1-1 na Polisi Tanzania. Imezifunga TRA United 2-1 na Pamba Jiji kwa matokeo kama hayo.
Hivyo, Kaitaba inaweza kuwa uwanja wa vita kwa timu zote mbili. Kagera itatumia faida ya nyumbani kusaka pointi, wakati Azam ikihitaji ushindi ili kujiimarisha zaidi kwenye msimamo.
Kwa sasa, Azam ina pointi nane kwenye nafasi ya nne, kama itashinda, maana yake itakamata nafasi ya tatu na kuishusha Mbeya City yenye pointi tisa ambayo itacheza keshokutwa Jumatano.
Lakini kama itapoteza, kisha Geita ikapata angalau sare mbele ya Simba, basi Azam itashuka nafasi moja kuipisha Geita.
Kagera yenyewe ipo mkiani na pointi moja, hali si nzuri hivyo inahitaji kuamka na kuibua matumaini ya kutorudi ilipotoka.
MAKOCHA WANENA
Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker amesema ana heshima kwa Geita Gold kutokana na kiwango ilichoonyesha katika michezo yake ya mwanzo.
Barker amesema wamejiandaa vizuri kwa mchezo huo na kufanya maandalizi maalumu, akisisitiza kuwa Geita si timu ya kubeza.
“Geita ni timu nzuri, tumeiona namna ilivyocheza na kiwango walichoonyesha hadi sasa. Tunaiheshimu, lakini sisi tumejiandaa kuhakikisha tunapata matokeo mazuri,” amesema Barker.
Kiungo wa Simba, Daudi Semfuko amesema kikosi kiko katika hali nzuri na kila mchezaji anatambua umuhimu wa mchezo huo.
“Wachezaji wote tuko fiti na tumejiandaa kwa mchezo huu. Tunajua Geita ni timu nzuri na itakuwa mechi ngumu, lakini tunachotaka ni kupambana kwa nguvu zetu zote kuhakikisha tunapata pointi tatu,” amesema na kuongeza.
“Mchezo uliopita umeshapita, hatuna presha. Tumeangalia tulipokosea na kocha amefanya marekebisho makubwa kwenye mazoezi. Sasa tunakwenda uwanjani kutekeleza mipango tuliyopewa ili kupata ushindi.”
Kwa upande wa Geita, Kocha Zuberi Katwila amesema wanatambua ukubwa wa Simba na uwezo wa wachezaji wake, lakini wameichukulia mechi hiyo kama fursa ya kuonyesha ubora wao wa kimbinu.
“Simba ni timu kubwa na nzuri, ina wachezaji wenye uwezo wa kubadilisha matokeo wakati wowote. Lakini kucheza dhidi ya timu kama Simba ni nafasi kwetu kuonyesha ubora wetu wa kimbinu.
“Tunataka kupambana nao kwenye maeneo yao ya ubora na kuwalazimisha kufanya makosa. Tukipata makosa hayo, tunataka kuyatumia kupata pointi tatu,” amesema Katwila.
Nahodha wa Geita, Yusuph Mhilu, amesema pointi moja waliyoipata dhidi ya Azam imeongeza morali ndani ya kikosi.
“Tumepata motisha kubwa baada ya kupata pointi dhidi ya Azam. Hilo limetupa nguvu zaidi kisaikolojia na kiupambanaji, lakini tunajua dhidi ya Simba tunahitaji nidhamu na umakini mkubwa ili kutekeleza maelekezo ya kocha.
“Mwalimu ametuambia mchezaji mkubwa anaonekana kwenye mechi kubwa. Hii ni fursa kwetu kujitangaza, kila mmoja anataka kuonyesha uwezo wake na kujitengenezea soko,” amesema Mhilu.
Kocha Mkuu wa Fountain Gate, Fred Felix Minziro, amesema: “Siyo rahisi kucheza na timu kama Yanga, imefanya usajili mzuri sana na wana wachezaji bora, lakini mpira ni mchezo wa maandalizi, tumejiandaa kukabiliana nao.
“Tunakwenda kujitahidi kupunguza spidi yao, lazima tupambane kulifanikisha hilo na naamini tunaweza kufanikiwa.”
Kocha Mkuu wa Yanga, Manqoba Mngqithi, amesema: “Hizi ni miongoni mwa mechi ngumu na ni muhimu sana kushinda, tunafahamu Fountain Gate wana mwalimu mzuri ambaye amewahi kuwa sehemu ya benchi la Yanga, hivyo anajua tamaduni za klabu, ni mzoefu na ana wachezaji wazuri, sisi kama Yanga tunapaswa kufanya kazi kubwa ili kushinda kesho (leo).
“Tunafahamu wapinzani wetu wamepoteza michezo kadhaa hapo nyuma, lakini jukumu letu ni kuheshimu kila mchezo, tumewaangalia Fountain Gate namna wanavyocheza na leo (jana) tunakwenda kufanya maandalizi ya mwisho ya kucheza nao, naamini tutakuwa na mechi nzuri.”
Winga wa Yanga, Issa Abushiri ambaye msimu uliopita alikuwa Fountain Gate, amesema: “Sisi wachezaji tuna morali na tunahitaji ushindi kwasababu tunataka kusogea mbele zaidi ya alama tulizokuwa nazo, tumejiandaa vizuri na tunaamini tutakuwa na mechi nzuri kesho (leo).”