Dk Mwinyi aridhishwa maandalizi AFCON 2027
Muktasari:
- Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji mwenza wa AFCON 2027 pamoja na Kenya na Uganda. Fainali hizo zitaanza Juni 19, 2027 hadi Julai 17, 2027.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali imeridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi ya miundombinu kuelekea Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
Dk Mwinyi amesema hayo Oktoba 3, 2026 Ikulu Zanzibar wakati akizungumza na vyombo vya habari, akibainisha kuwa maandalizi hayo hayahusishi uwanja pekee, bali pia maboresho ya miundombinu mingine, ikiwemo barabara katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar.
“Tunaridhika sana na kasi ya ujenzi wa miundombinu yote, si uwanja peke yake. Barabara ukitembea hivi sasa unaona kabisa kuna mabadiliko makubwa ya barabara,” amesema Dk Mwinyi.
Amesema maendeleo hayo yanaendelea kuimarisha maandalizi ya Zanzibar kuelekea mashindano hayo, huku wakaguzi kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF) wakipongeza hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa uwanja huo.
“Na kwa kweli hata wakaguzi wanapokuja hapa kutoka CAF, wanapongeza sana Zanzibar kwa hatua tuliyofikia. Tunaenda vizuri,” amesema.
Amesema wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo wameahidi kukamilisha na kukabidhi kazi hizo ifikapo Desemba mwaka huu, jambo litakaloipa Zanzibar muda wa kutosha kujiandaa kabla ya mashindano kuanza Juni 19, 2027.
Amesema Serikali itaendelea kufuatilia utekelezaji wa miradi hiyo ili kuhakikisha miundombinu inakidhi mahitaji ya mashindano pamoja na wageni watakaofika Zanzibar.
Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji mwenza wa AFCON 2027 pamoja na Kenya na Uganda. Fainali hizo zitaanza Juni 19, 2027 hadi Julai 17, 2027.