Fountain Gate yazidi kuiweka pabaya KMC
Muktasari:
- Kabla ya hapo, KMC ilipokwenda Tanzanite Kwaraa Oktoba 25, 2025 kukabiliana na Fountain Gate, ilichapwa pia 1-0.
KMC imeendeleza uteja mbele ya Fountain Gate katika Ligi Kuu Bara baada ya leo Mei 10, 2026 kuchapwa mabao 3-2 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.
Kabla ya hapo, KMC ilipokwenda Tanzanite Kwaraa Oktoba 25, 2025 kukabiliana na Fountain Gate, ilichapwa pia 1-0.
Kwa matokeo hayo, Fountain Gate imefikisha pointi 25 ikipanda nafasi mbili kutoka ya 12 hadi ya 10 ikizishusha Mtibwa Sugar (pointi 23) na Namungo (pointi 24), huku KMC ikiendelea kudidimia na kusogea zaidi kushuka daraja ikibaki na pointi tisa baada ya mechi 22.
Sadick Ramadhan aliipa Fountain Gate bao la kuongoza dakika 28 akipokea pasi ya Issa Juma Abushiri, dakika chache baadaye likasawazisha na winga wa KMC, Erick Mwijage akipokea pasi ya Rashid Chombo. Zikaenda mapumziko matokeo yakiwa sare ya 1-1.
Kipindi cha pili dakika ya 61, Chukwunonye Obasi raia wa Nigeria, alifunga bao la pili akipokea krosi ya Ismail Aziz Kader, baadaye dakika ya 68, Chombo ambaye ndiye aliyetoa pasi ya bao la kwanza kwa KMC, alisawazisha na kufanya matokeo kuwa 2-2.
Wakati ikionekana mechi inaweza kumalizika kwa sare, dakika ya 86, Henry David aliifungia Fountain Gate bao la tatu, ambapo alianza kuukokota mpira mbali, akamfinya Suleiman Juma Kidawa wa KMC na kuwazidi mabeki wengine wawili kisha akapiga shuti na kufunga akiihakikishia Fountain Gate ushindi huo.
Fountain Gate huo ni ushindi wa saba katika mechi 22, ikitoka sare nne na kupoteza 11, inamiliki mabao ya kufunga 17, imetikiswa nyavuni mara 32.
KMC inaendelea kushika mkia kwa pointi tisa ilizozikusanya katika mechi 22, ikishinda mbili, sare tatu na kupoteza 17, ikiwa na mabao ya kufunga 10 na mabao ya kufungwa 35.
Katika msako wa kujinasua na janga la kushuka daraja, KMC imebakiwa na mechi nane zenye poiti 24 ambapo ikizikusanya hizo, itamaliza msimu na pointi 33 ambazo hivi sasa inazo TRA United iliyopo nafasi ya sita kwenye msimamo.
Hata hivyo, KMC inakabiliwa na changamoto kubwa ya kupata matokeo mazuri kwani mechi tisa za mwisho katika ligi, imepoteza nane na sare moja.
Hesabu zinaonyesha KMC ikipoteza mechi tano kati ya nane zilizobaki, halafu ikashinda hizo zingine, itafikisha pointi 18 ambazo zitaibakisha kwenye mstari mwekundu wa kushuka daraja.
Ratiba yao pia haionekani kuwa rafiki. Bado inakutana na vigogo wawili wa ligi, Azam na Simba huku pia ikiwa na mechi ngumu dhidi ya TRA United na Mashujaa.
Mechi zingine ni dhidi ya Mtibwa Sugar, Coastal Union na Namungo ambazo zote zinapambana kwenye ukanda wa chini. Pia mpinzani mwingine aliyebaki kwao ni Pamba Jiji.