Hesabu za Serengeti Boys robo fainali
Muktasari:
- Mechi hiyo itapigwa Uwanja wa Mohammed VI Football, Morocco na mshindi atakutana na Ivory Coast au Misri katika hatua ya nusu fainali.
LEO saa 10 jioni kwa saa za Afrika Mashariki, timu ya Taifa ya Wavulana chini ya miaka 17, Serengeti Boys itaminyana na Algeria katika mechi ya robo fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON U-17), michuano inayoendelea nchini Morocco.
Mechi hiyo itapigwa Uwanja wa Mohammed VI Football, Morocco na mshindi atakutana na Ivory Coast au Misri katika hatua ya nusu fainali.
Serengeti Boys ambayo imeshafuzu kucheza Kombe la Dunia U-17 litakalofanyika Qatar kuanzia Novemba 19 hadi Desemba 13, mwaka huu, ilivuka hatua ya robo fainali baada ya kumaliza kileleni mwa kundi C ikusanya pointi sita.
Serengeti Boys ilianza vizuri kampeni zake Kundi C baada ya kuifunga Msumbiji na Angola kwa mabao 3-0 katika michezo miwili. Hata hivyo, katika mchezo wa mwisho wa kundi hilo, Tanzania ilipoteza kwa mabao 2-1.
Katika robo fainali nyingine, wenyeji Morocco watacheza dhidi ya Cameroon huku Senegal wakiikabili Mali ambapo washindi watakutana nusu fainali.
Mbali na Tanzania, timu nyingine ambazo tayari zimefuzu kucheza Kombe la Dunia U-17 kutoka Afrika ni Morocco, Senegal, Mali, Cameroon, Ivory Coast, Misri na Algeria. Zingine mbili zinasubiriwa kutimia timu kumi ambapo zinacheza play off ambapo ratiba inaonesha Ethiopia vs Msumbiji na Uganda vs Ghana.
Kocha mkuu wa Serengeti Boys, Elieneza Nsanganzelu, alisema: “Namna gani tunaweza kucheza na wapinzani wetu tumewaangalia na tumejifunza ni timu yenye wachezaji wazuri nusu yake wametoka Ulaya, wako vizuri kiufundi wana wachezaji wenye maumbo makubwa.
“Ili tuweze kufanikiwa kushinda tunatakiwa kucheza katikati yao tusipishane nao ili tuweze kutengeneza nafasi ya kufunga.”
Kwenye droo ya makundi ya Kombe la Dunia U-17 iliyochezeshwa jijini Zurich, Uswisi Mei 21, mwaka huu, Serengeti Boys imepangwa Kundi I pamoja na Brazil, Jamhuri ya Ireland na Costa Rica.
Kwa mujibu wa ratiba ya Kombe la Dunia U-17, Serengeti Boys itaanza kampeni zake Novemba 21 dhidi ya Costa Rica. Baada ya hapo, Tanzania itakuwa na kibarua kigumu dhidi ya mabingwa wa zamani, Brazil Novemba 24 kabla ya kuhitimisha hatua ya makundi dhidi ya Jamhuri ya Ireland Novemba 27.