Prime
Jeuri ya Yanga iko hapa!
WAKATI Yanga wakianza vyema kampeni za kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa kushinda mechi mbili ilizocheza hadi sasa, ila moja ya wachezaji walioonyesha kiwango kizuri na cha kuvutia ni beki wa kushoto, Mkongomani Chadrack Boka ambaye kwa sasa anaonekana ndiye anawapa kiburi.
Nyota huyo hakuimbwa tangu msimu huu umeanza kutokana na maingizo ya wachezaji wapya wakiwemo, Albert Kangwanda, Seleman Mwalimu ‘Gomez’, Housseine Zakouani na Peter Shalulile, ingawa kiwango cha Boka kimeanza kuteka upya hisia za mashabiki.
Katika mechi tatu za Yanga msimu huu wa 2026-2027, ikianza na moja ya Kombe la Ngao ya Jamii na mbili za Ligi Kuu Bara, nyota huyo amechangia mabao manne na kuonyesha kiwango bora chini ya Kocha Mkuu, Manqoba Mngqithi raia wa Afrika Kusini ambaye ameanza na timu hiyo msimu huu.
Moto wa nyota huyo ulianza kuonekana katika mechi ya Ngao ya Jamii, Agosti 12, 2026 dhidi ya watani zao wa jadi Simba na alichangia bao la ushindi wa timu hiyo wa 1-0, lililofungwa na Albert Kangwanda dakika ya 31 na kutwaa taji hilo la kwanza kwa timu hiyo msimu huu.
Katika mechi hiyo ya ‘Kariakoo Derby’ iliyopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani Zanzibar, Agosti 12, 2026, nyota huyo alionyesha kiwango kizuri kilichochangia timu hiyo kutwaa Ngao hiyo kwa mara ya tatu mfululizo.
Kwa upande wa Ligi Kuu Bara, Yanga imecheza mechi mbili na kufunga mabao saba hadi sasa, japo kati ya hayo Boka amekuwa ni muhimili mkubwa tena, baada ya mchezaji huyo kuchangia matatu, akiwa amefunga moja na kutoa pasi mbili za mabao.
Yanga ilianza Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2026-2027, kwa ushindi wa mabao 3-1, dhidi ya Namungo FC, Agosti 15, 2026, huku Boka akiwa ndiye mchezaji wa kwanza wa kikosi hicho kwa kuifungia bao la kwanza la msimu huu alilolifunga dakika ya 68.
Mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Majaliwa, Lindi, mabao mengine yalifungwa na Maxi Nzengeli dakika ya 71 na Peter Shalulile dakika ya 89, huku la Namungo likifungwa na Herbert Lukindo dakika ya 75.
Katika mechi ya pili ya Ligi Kuu Bara ambayo Yanga iliifunga Coastal Union mabao 4-1, Agosti 20, 2026, kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge jijini, Dar es Salaam, Boka alichangia mawili, akianza na bao la Albert Kangwanda la dakika ya 38.
Nyota huyo akachangia tena bao la beki mwenzake anayecheza pia upande wa kushoto, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, dakika ya 90+3 na kuhusika na mabao matatu ya Ligi Kuu hadi sasa msimu wa 2026-2027, baada ya kufunga moja na kuasisti mawili.
Mabao mengine ya Yanga katika mechi hiyo yalifungwa na Maxi Mpia Nzengeli dakika ya 45+3 na Mudathir Yahya dakika ya 50, huku bao pekee la kufutia machozi kwa upande wa Coastal Union likifungwa na Mkongomani Lassa Gradi Kiala dakika ya 77.
Kwa maana hiyo tangu msimu huu wa 2026-2027, umeanza, Boka amechangia mabao manne katika mechi tatu alizoichezea Yanga, ikiwa ni kiwango bora kinachoonyesha jinsi timu hiyo inavyoweza kutengeneza mabao kutokea maeneo mbalimbali ya uwanjani lakini pia akiwa ndiye mchezaji ambaye amefanya kazi kubwa zaidi kwenye timu hiyo hadi sasa.
Urejeo wa kiungo mshambuliaji, Stephane Aziz KI aliyejiunga na Yanga akitokea Al-Ittihad SC ya Libya unatoa nafasi pia ya timu hiyo kutengeneza mabao mengi katikati, ingawa ikiwa itashindikana Boka ni chaguo lingine bora kupitia pembeni.
Kocha Mkuu wa Yanga, Manqoba Mngqithi ni kama amefufua upya kiwango cha nyota huyo kwani msimu wa 2025-2026, hakuwa na bao lolote alilofunga wala kutoa asisti, akikichezea kikosi hicho msimu wa tatu tangu alipojiunga nacho, Julai 7, 2024.
Beki huyo alijiunga rasmi na Yanga Julai 7, 2024, akitokea FC Saint Eloi Lupopo ya kwao DR Congo, akiendelea kuonyesha kiwango bora na cha kuvutia, licha ya uwepo wa beki mwenzake anayecheza upande wa kushoto, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.
Awali mashabiki walikuwa hawaridhishwi na kiwango cha staa huyo kutokana na kutokuwa na namba nzuri kwenye kila mchezo aliokuwa akicheza.
Hata hivyo tetesi zilikuwa zinasema alikuwa anaweza kuachwa kabla dirisha la usajili halijafungwa akiwa sasa anatumikia mkataba wake wa miezi sita uliobaki klabuni hapo.