Kocha Mtanzania aula Leicester City
Muktasari:
- Mashindano hayo yalihudhuriwa pia na wachezaji wa zamani wa Leicester City, Wes Morgan, Liam Moore na Jeffrey Schlupp, pamoja na mchezaji wa sasa wa klabu hiyo, Misrad Ali.
MSHAMBULIAJI wa zamani wa akademi ya Leicester City, Adi Yussuf, ameendelea na safari yake ya ukocha ndani ya klabu hiyo baada ya kuteuliwa kuwa kocha msaidizi wa kikosi cha vijana chini ya miaka 21 (U21).
Yussuf ambaye ni Mtanzania, ambaye awali alikuwa kocha msaidizi wa kikosi cha Leicester City chini ya miaka 18 (U18), amepandishwa baada ya kustaafu kucheza soka. Alianza safari yake ya soka katika klabu hiyo na alikuwa akicheza mara kwa mara katika kikosi cha akiba, ingawa hakuwahi kupata nafasi ya kucheza mechi ya timu ya wakubwa.
Baadaye alizitumikia klabu mbalimbali zikiwemo Burton Albion, Mansfield Town, Solihull Moors, Crawley Town na Oxford City, huku akiichezea timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, mechi nne za kimataifa baada ya kucheza mechi yake ya kwanza Juni 2019.
Yussuf alirejea Leicester City akiwa bado anacheza soka katika klabu ya Halesowen Town, alipojiunga na programu ya Premier League ya Professional Player to Coach Scheme (PPCS) inayowasaidia wachezaji kuingia katika taaluma ya ukocha. Mwaka uliopita alianza kufanya kazi na kikosi cha U18 chini ya kocha Adam Barradell.
Kupitia ujumbe wake kwenye Instagram, Yussuf alieleza furaha yake baada ya kupata nafasi hiyo mpya akisema: “Nina furaha kutangaza kwamba nimeanza nafasi mpya ya kocha msaidizi wa U21 katika klabu ya Leicester City. Nashukuru kwa fursa hii ya kupiga hatua nyingine katika safari yangu ya ukocha.”
Yussuf ni mtu anayependwa ndani ya Leicester City kutokana na uhusiano wake na wachezaji kadhaa waliopitia mfumo wa akademi ya klabu hiyo. Miongoni mwa wachezaji walioonyesha kumuunga mkono baada ya kutangaza nafasi hiyo ni Bade Aluko, Jayden Joseph, Ben Nelson, Kasey McAteer na Tom Wilson-Brown.
Kocha wa timu ya kwanza ya Leicester City, Andy King, ambaye aliwahi kufanya kazi katika akademi ya klabu hiyo, pia alitoa pongezi kwa kuandika neno “Top” kwenye ujumbe wa Yussuf.
Mbali na soka, Yussuf ni mwanzilishi na mtendaji mkuu wa kampuni ya nogoalsnosleep, inayojihusisha na mavazi ya mic hezo. Mw ezi Septemba, kampuni hiyo iliandaa mashindano katika kituo cha WhatAGoal, karibu na Hamilton, yaliyovutia zaidi ya watu 300.
Mashindano hayo yalihudhuriwa pia na wachezaji wa zamani wa Leicester City, Wes Morgan, Liam Moore na Jeffrey Schlupp, pamoja na mchezaji wa sasa wa klabu hiyo, Misrad Ali.