Kwa Simba Queens zinabondwa tu, yaitandika JKT na kutwaa ubingwa
Muktasari:
- Pambano hilo lililokuwa la vuta nikuvute na presha kubwa, lilishuhudia Simba Queens ikionyesha madhara makubwa kipindi cha pili na kufanikiwa kupata bao pekee lililowapa ndoo hiyo ya heshima.
SIMBA Queens imerejesha heshima na kutawazwa mabingwa wapya wa Ngao ya Jamii baada ya kuichapa JKT Queens bao 1-0 kwenye fainali iliyopigwa Uwanja wa KMC Complex jioni hii.
Pambano hilo lililokuwa la vuta nikuvute na presha kubwa, lilishuhudia Simba Queens ikionyesha madhara makubwa kipindi cha pili na kufanikiwa kupata bao pekee lililowapa ndoo hiyo ya heshima.
Mchezo huo ulianza kupata joto katika dakika ya 59 baada ya mchezaji wa JKT Queens, Ester Maseke, kumvuta jezi mshambuliaji hatari wa Simba Queens, Aisha Mnunka na kuonyeshwa kadi nyekundu.
Baada ya kucheza pungufu Simba Queens ikapata bao kupitia kwa Mnunka dakika ya 62 baada ya Simba kufanya shambulio la kushtukiza ambapo Mary Siyame alitoa pasi iliyowekwa kambani kiufundi.
Pasi hiyo ya Siyame ilimkuta mfungaji aliyekuwa kwenye nafasi nzuri na kuujaza mpira kimiani kwa umakini mkubwa, bao lililolipua shangwe kubwa kutoka kwa mashabiki wa Msimbazi waliokuwa wakishangilia muda wote.
Ushindi huo wa bao 1-0 una maana kubwa kwa Simba Queens kwani rasmi imewapokonya JKT Queens ubingwa huo waliokuwa wakiutetea, na kudhihirisha ubora wao baada ya mapambano ya muda mrefu ya kusaka heshima ya soka la wanawake.
Hii ni mara ya pili kwa Simba Queens kutwaa taji hilo tangu mashindano hayo yalipoanzishwa, ambapo ilibeba ubingwa kwa mara ya kwanza mwaka 2023 baada ya kuitoa JKT Queens kwa mikwaju ya penalti 5-4 baada ya sare ya 1-1 kwenye fainali iliyokuwa na msisimko wa aina yake.
Hata hivyo, rekodi zinaonyesha kuwa mwaka 2024 JKT Queens ilirejea kwa kasi na kubeba ubingwa huo baada ya kuitandika Yanga Princess bao 1-0 kwenye mchezo wa fainali.
JKT Queens iliendelea kudhihirisha ubabe wake mwaka 2025 kwa kubeba taji hilo kwa mara ya pili mfululizo pale ilipoichapa Simba Queens mabao 2-1, kabla ya jioni ya leo Simba Queens kulipa kisasi .
Kwa matokeo haya, sasa miamba hiyo ya soka la wanawake inalingana mataji hayo wote wawili wakibeba mara mbili.