Prime
Manqoba afichua siri ya Boka kutikisa Yanga
BEKI wa kushoto wa Yanga, Chadrack Boka ameanza msimu kibabe mpaka sasa ameshaweka namba sawa katika mechi ambazo amecheza, huku kocha wa kikosi hicho Manqoba Mngqithi amefunguka akitaja kiwango cha Mkongomani huyo.
Boka kwenye mechi tatu ukinzia ile ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba krosi yake ilitengeneza bao pekee, lakini kama haitoshi ndani ya Ligi Kuu Bara ambapo Yanga imecheza mechi mbili, ameshatengeneza asisti mbili na kufunga bao moja.
Itakumbukwa baada ya msimu uliopita kumalizika, ilikuwa kama Yanga inapiga hesabu za kumuacha beki huyo wa zamani wa FC Lupopo, wakiona kama kiwango chake hakitoshi kuendelea kuvaa jezi za njano na kijani, lakini amebaki na kuuwasha moto.
Akizungumza na Mwanaspoti, Manqoba amesema Boka yupo kwenye kiwango bora kutokana na namna anavyotekeleza majukumu yake uwanjani ambapo hatua hiyo imemfanya kuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi hicho.
Manqoba amesema Boka amekuwa mzuri wa kupandisha mashambulizi lakini pia mara timu inapopoteza mpira amekuwa na kasi ya kurudi kuzuia huku kimo chake na nguvu vikimbeba zaidi.
“Unataka nimzungumzie Boka, kila kitu kipo wazi, naridhishwa sana na namna alivyoimarika, yupo kwenye kiwango, unaona namna alivyo na msaada kwenye kikosi chetu,” amesema Manqoba.
“Angalia namna anavyoweza kupandisha mashambulizi mbele lakini tunaposhambuliwa unamuona haraka amesharudi kwenye eneo lake, ana nguvu, kasi na anatumia kimo chake vizuri, yupo kwenye kiwango bora."
Boka amefanikiwa kucheza dakika 180 kwenye mechi tatu za timu hiyo msimu huu zikiwemo mbili za ligi na moja Ngao ya Jamii. Leo Jumatatu Yanga inashuka uwanjani kucheza dhidi ya JKT Tanzania, itakayopigwa Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam ikiwa mechi ya tatu ya Ligi Kuu Bara.
Aidha Manqoba amesema ubora wa Boka ndio umemfanya wakati mwingine kumuhamisha nafasi na kumpeleka mbele beki mwenzake, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye kwa sasa amekuwa akitumika kama kiungo mshambuliaji akitokea kushoto.
“Tshabalala ni mchezaji mzuri lakini unaona anatumika kama kiungo mshambuliaji, hii ni kutokana na anajua sana kupiga krosi, nadhani uliona mchezo uliopita alitupa bao la nne.”