Prime
Mpanzu, Edgar wana vita yao
SIMBA inarudi dimba la nyumbani Jumapili hii kuikaribisha Dodoma Jiji, ambayo siku chache zilizopita ilitoa shangwe kwa Wekundu hao waliposhinda mechi moja muhimu dhidi ya mtani wake na sasa zamu yao wakijua waliwahi kuwatibulia.
Mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara inayokwenda kuchezwa Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam kuanzia saa 12:15 jioni, ndani yake kuna vita ya eneo la ushambuliaji ambapo kila upande unataka kusaidia ushindi kwa kufunga mabao.
Hivi sasa Simba pale mbele, Kocha Steve Barker amekuwa akimuanzisha Elie Mpanzu kama mshambuliaji kinara, akimuacha Seleman Mwalimu nje. Kwa upande wa Dodoma Jiji, Edgar William ndiye kinara wao wa mabao akiifanya kazi yake vizuri akifunga saba, huku msimu huu akiwa tayari ameifunga Yanga pale KMC Complex wakati Dodoma Jiji ikifungwa 3-1.
Simba inataka kuendelea kuweka presha kwa Yanga na kama ikishinda mchezo huu itarudi tena juu ya msimamo itakapofikisha pointi 58 kama ambavyo ilivyofanya dhidi ya Coastal Union, kabla ya kushushwa na watani wao wa jadi, Yanga waliopo kileleni hivi sasa na pointi 57.
Wekundu hao kama watashindwa kushinda, maana yake watasalia nafasi hiyo ya pili, lakini matokeo hayo yatakuwa ahueni kwa Yanga ambayo itaendelea kusalia kileleni mwa msimamo wa ligi huku ikiongeza tofauti ya pointi kati yake na mtani wake huyo.
Simba inatambua kwamba Dodoma Jiji licha ya kwamba haijawahi kuonja ushindi mbele yake, lakini msimu huu iliwatibulia ikiwa kwao baada ya kulazimishwa matokeo ya bila kufungana Februari 25, 2026 kwenye mchezo ambao Wekundu hao walitengeneza nafasi nyingi za kufunga.
Kwenye mechi tano za mwisho, Simba imefanya vizuri ikishinda nne dhidi ya Coastal Union, Mashujaa, Prisons na JKT Tanzania, huku sare ikiwa moja dhidi ya Yanga.
Takwimu hizo zinaipendelea zaidi Simba ambapo kwenye mechi 11 ambazo timu hizo zimekutana, Wekundu hao wameshinda 10 na sare moja, huku wakifunga jumla ya mabao 22 wakati Dodoma ikifunga mawili pekee.
Kama kuna mchezaji ambaye atakuwa kwenye vichwa vya makocha na wachezaji wa Dodoma Jiji kutafuta namna ya kumzuia ni kiungo wa Simba, Clatous Chama ambaye yupo kwenye kiwango bora akibeba tuzo tano mfululizo za mchezaji bora wa mechi.
Chama ambaye amefanikiwa kufunga mabao manane akiwa na asisti sita, akihusika kwenye jumla ya mabao 14, amekuwa kwenye kiwango bora ambapo mchezo wa mwisho dhidi ya Coastal aliyatengeneza yeye, Simba ikishinda 2-1.
Kocha msaidizi wa Simba, Suleiman Matola akizungumzia mchezo huo, alisema: “Haitakuwa mechi rahisi, ukiangalia matokeo ya mechi iliyopita tulipokutana nao walitupa wakati mgumu pamoja na upinzani mkubwa lakini pamoja na ugumu na ubora wao, tumejipanga kuhakikisha tunapata pointi tatu katika mchezo wa kesho (leo).”
Dodoma Jiji iliyo nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi ikikusanya pointi 33, kama ikifanikiwa kupata angalau pointi moja itaishusha Pamba Jiji ambapo zimelingana pointi.
Timu hiyo haijawahi kuifunga Simba lakini itaringia matokeo baada ya kuifunga Yanga kwa mabao 3-2, matokeo ambayo yalikuwa ni ushindi wake wa kwanza dhidi ya mabingwa hao watetezi lakini ikisitisha ubabe wa ushindi wa vinara hao.
Dodoma kwenye mechi tano za mwisho imeshinda mbili ikizifunga Yanga na Mtibwa Sugar lakini ikatoa sare tatu ikikutana na Simba ambayo kiwango chao kimeimarika vizuri kwasasa ikionyesha inataka ubingwa.
Kocha wa Dodoma Jiji, Amani Josiah akizungumzia mchezo huo alisema: “Tumejiandaa vizuri kwenda kukutana na Simba, tutaingia tukiwa kama timu ya pili lakini mchezo utakuwa wa presha kubwa kwa Simba, tunawaheshimu ni timu nzuri lakini watahitaji matokeo kutokana na malengo yao lakini na sisi tunataka matokeo kujiweka sehemu nzuri zaidi.”
Kabla ya mechi hiyo, mapema saa 10:00 jioni kuna mitanange miwili, TRA United itaikaribisha Fountain Gate kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid uliopo Arusha ambao timu hizo zinautumia kwa mechi za nyumbani.
Ni mechi ambayo TRA inahitaji kushinda ili kupanda hadi nafasi ya nne ikifikisha pointi 40 ikizishudha JKT Tanzania (pointi 37) na Singida Black Stars (pointi 38).
Fountain Gate ambayo ipo nafasi ya 11 ikikusanya pointi 26, inahitaji kushinda ili kupanda hadi nafasi ya tisa ikizishusha Mtibwa Sugar (point 26) na Mashujaa (pointi 27).
Kocha wa Fountain Gate, Fred Felix Minziro, alisema: “Tumejiandaa Vizuri na mchezo na vijana wapo tayari kwa kupambana, siyo mechi rahisi lakini hakuna kuingia kinyonge, tunazihitaji alama tatu kesho (leo).”€
Mechi nyingine itakayochezwa saa 10:00 jioni ni Mtibwa Sugar ikiikaribisha JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro. Hii pia ni mechi ambayo kila timu inahitaji ushindi kujiweka pazuri. Mtibwa baada ya kutoka kufungwa na TRA United 2-1 ugenini, inarudi nyumbani ambapo tangu ilirejea hapo kwa mara ya kwanza Mei 14, 2026 na kuifunga KMC mabao 4-3. Leo ni wakati mwingine kupata ushindi na kukaa pazuri.
Usiku saa 2:30, Coastal Union yenye pointi 25, inacheza dhidi ya Mashujaa inayoshika nafasi ya nane kwa pointi 27. Tofauti ya pointi mbili tu inazitenganisha timu hizi. Mechi inakwenda kupigwa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.