Okello, Pedro waibuka vinara Ligi Kuu ya NBC mwezi Aprili
Muktasari:
- Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Mei 13, 2026 na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Okello alimshinda mchezaji mwenzake wa Yanga, Pacome Zouzoua na Idd Selemani wa Azam baada ya kuonyesha kiwango bora ndani ya mwezi huo.
KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Allan Okello, ametwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwezi Aprili 2026 huku aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Pedro Goncalves akiibuka kocha bora wa mwezi huo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Mei 13, 2026 na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Okello alimshinda mchezaji mwenzake wa Yanga, Pacome Zouzoua na Idd Selemani wa Azam baada ya kuonyesha kiwango bora ndani ya mwezi huo.
Nyota huyo wa Yanga alihusika moja kwa moja katika mabao saba ndani ya mechi tatu kwa dakika 320 alizocheza mwezi huo, akifunga bao moja na asisti sita.
Kwa upande wa makocha, Pedro ambaye kibarua chake kiliota nyasi Mei 6, 2026, aliwashinda Steve Barker wa Simba na Etienne Ndayiragije wa TRA United. Ametwaa tuzo hiyo baada ya kuiongoza Yanga kushinda michezo yote mitatu iliyocheza mwezi Aprili.
Yanga pia ilifunga mabao 12 bila ya kuruhusu nyavu zake kutikiswa katika kipindi hicho, ikizifunga Tanzania Prisons (3-0), Mbeya City (6-0) na Pamba Jiji (3-0).
Kwa upande wa Ligi ya Championship, mshambuliaji Hassan Mwatarema wa Kagera Sugar ametajwa kuwa mchezaji bora wa mwezi huku Juma Kaseja wa Kagera Sugar akitwaa tuzo ya kocha bora.
Mwatarema aliwashinda Japhet Manyungu wa TMA na Salum Mlemwa wa Gunners kutokana na mchango wake mkubwa wa kuisaidia Kagera Sugar, akifunga mabao mawili ndani ya dakika 139 alizocheza.
Naye Kaseja aliwashinda Zuberi Katwila wa Geita Gold na Mbwana Makata wa Polisi Tanzania baada ya kuiongoza Kagera Sugar kushinda michezo yote miwili iliyocheza mwezi huo na kuendelea kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi ya Championship.
Pia Kamati ya Tuzo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imeteua mabao matatu yaliyoingia fainali katika kinyang'anyiro cha bao bora la mwezi ambalo litapigiwa kura. Mabao hayo ni lile la PacomeZouzoua wa Yanga dhidi ya Mbeya City, Idd Kipagwe wa Dodoma Jiji dhidi ya Fountain Gate na Grayson Gwalala wa Coastal dhidi ya Dodoma Jiji.