Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba Queens inahesabu mbili kubeba ubingwa

Muktasari:

  • Simba Queens imefikisha pointi 52 ikiwa tofauti ya pointi 10 na JKT Queens na Yanga Princess zenye 42 katika nafasi ya pili na tatu, hivyo ikishinda mechi mbili itafikisha pointi 58 ambazo hazitafikiwa na timu yoyote ndani ya ligi hiyo msimu huu.

ZIMEBAKI sita! Ndivyo wanavyosema mashabiki wa Simba Queens wakimaanisha wanahitaji kushinda mechi mbili kati ya nne zilizobaki ili kutangazwa kuwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) msimu huu.

Simba Queens imefikisha pointi 52 ikiwa tofauti ya pointi 10 na JKT Queens na Yanga Princess zenye 42 katika nafasi ya pili na tatu, hivyo ikishinda mechi mbili itafikisha pointi 58 ambazo hazitafikiwa na timu yoyote ndani ya ligi hiyo msimu huu.

Hilo linakuja baada ya leo Mei 23, 2026, Simba Queens kuitandika JKT Queens kwa mabao 2-1 katika mechi ya raundi ya 18 iliyopigwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo jijini Dar es Salaam.

Baada ya kipindi cha kwanza kumalizika kwa sare tasa, Simba Queens ilirejea kwa kasi kipindi cha pili na kiungo mshambuliaji, Aisha Mnunka aliiandikia bao la kwanza dakika ya 50 na kuamsha shangwe kubwa kwa mashabiki.

Dakika nne baadaye, Fasila Adhiambo aliandika bao la pili lililoonekana kuimaliza nguvu JKT Queens baada ya kutumia vyema nafasi iliyotengenezwa na Elizabeth Wambui.

JKT Queens ilijaribu kurejea mchezoni dakika ya 62 kupitia kwa Asha Mwalala aliyefunga bao la kufutia machozi baada ya winga Winifrida Gerald kupiga shuti kali lililoshindwa kudhibitiwa vizuri na kipa wa Simba Queens, Ruth Aturo kabla ya mpira kumkuta Mwalala aliyeukwamisha wavuni.

Licha ya juhudi za JKT Queens kusaka bao la kusawazisha katika dakika zilizobaki, Simba Queens ilionyesha uimara mkubwa katika safu ya ulinzi na kufanikiwa kulinda ushindi huo muhimu.

Matokeo hayo yanaifanya Simba Queens kuukaribia zaidi ubingwa wa WPL msimu huu ambapo ikishinda mechi mbili zijazo dhidi ya Tausi FC itakayochezwa Mei 27, 2026 na Mashujaa Queens (Mei 31, 2026), shughuli itakuwa imefika mwisho.

Mechi zingine za raundi ya 18 zilizochezwa leo, Yanga Princess imekubali kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Mashujaa Queens, mechi iliyopigwa Uwanja wa TFF Kigamboni, Tausi FC imezidi kuikandamiza Ruangwa Queens mkiani baada ya kuitandika mabao 4-0.

Fountain Gate Princess imeichapa Ceasiaa Queens mabao 3-1, mechi iliyopigwa Uwanja wa Tanzanite Kwaraa mkoani Manyara.