Simba Queens yatupwa nje CECAFA
Muktasari:
- Timu hiyo imeondolewa baada ya Kenya Police Bullets kufuzu hatua ya nusu fainali kutoka Kundi C baada ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Top Girls Academy ya Burundi.
SIMBA Queens imeondolewa hatua ya makundi ya mashindano ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), yanayoendelea Kigali, Rwanda.
Timu hiyo imeondolewa baada ya Kenya Police Bullets kufuzu hatua ya nusu fainali kutoka Kundi C baada ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Top Girls Academy ya Burundi.
Katika michuano hiyo Simba ilianza kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Top Girls kisha ikapoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Police kwenye mechi ya pili.
Kutokana na hali hiyo pointi tatu ilizokusanya Simba hazikutosha, hivyo ikawa inasikilizia mechi ya mwisho kati ya Police dhidi ya Top Girls ambayo sare ingewapa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara nafasi ya kufuzu hatua ya nusu fainali.
Kwa Simba, matokeo hayo yamekuwa pigo jingine katika harakati za kurejesha taji linaloshikiliwa na JKT Queens ya Tanzania.
Kwa miaka ya hivi karibuni timu hiyo haijawa na wakati mzuri kwenye mashindano hayo kwani tangu ilipocheza nusu fainali mwaka 2022, lakini 2024 iliposhiriki kwa mara ya pili ilimaliza nafasi ya nne kwenye hatua za kufuzu CECAFA.
MAKUNDI YA CECAFA
Michuano ya mwaka huu imehusisha timu 10 kutoka ukanda wa CECAFA zilizogawanywa katika makundi matatu. Kundi A limekuwa na timu nne, wakati Kundi B na C yakiwa na timu tatu kila moja.
KUNDI A lilikuwa na wenyeji Rayon Sports ya Rwanda, Yei Joint Stars ya Sudan Kusini, Mafunzo Queens ya Zanzibar na Denden FC ya Eritrea.
Katika kundi hilo, Yei Joint Stars imekuwa miongoni mwa timu zilizofanya vizuri, ikifuzu hatua ya nusu fainali baada ya kumaliza kileleni. Rayon Sports na Yei Joint Stars zilitoka sare ya bao 1-1 katika mchezo wao wa mwisho, matokeo yaliyoiwezesha Yei kutangulia kufuzu hatua hiyo.
KUNDI B lina CBE ya Ethiopia, Kawempe Muslim Ladies ya Uganda na FC Ujeco ya Djibouti.
CBE iliingia kwenye mashindano ikiwa miongoni mwa timu zenye uzoefu mkubwa baada ya kutwaa ubingwa wa CECAFA mwaka 2024, huku Kawempe Muslim Ladies ikiwa inashiriki kwa mara ya pili.
KUNDI C, ambalo Simba Queens imeondolewa, lilikuwa na Simba Queens ya Tanzania, Kenya Police Bullets ya Kenya na Top Girls Academy ya Burundi.
Mfumo wa mashindano unaweka nafasi ya nusu fainali kwa vinara wa Kundi B na C pamoja na timu mbili bora kutoka Kundi A. Mshindi wa Kundi A anakutana na mshindi wa Kundi C, wakati mshindi wa Kundi B anakutana na mshindi wa pili bora wa Kundi A. Bingwa wa CECAFA ndiye atakayepata tiketi ya kuiwakilisha ukanda huo katika Ligi ya Mabingwa Afrika ya Wanawake.