Simba yaichakaza Mighty Wanderers, yatinga raundi ya pili kibabe
Muktasari:
- Ushindi huo unaifanya Simba kufuzu kwa jumla ya mabao 7-1 baada ya ushindi wa bao 1-0 kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza nchini Malawi.
SIMBA haina utani. Imefanikiwa kuitafuna Mighty Wanderers kwa ushindi wa mabao 6-1 ikitinga hatua ya pili ya mtoano wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ushindi huo unaifanya Simba kufuzu kwa jumla ya mabao 7-1 baada ya ushindi wa bao 1-0 kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza nchini Malawi.
Ni kama Simba jana ilikuwa inapeleka shule upande wa pili na mapema tu ndani ya dakika 35, ilijihakikishia ushindi huo kwa kutikisa nyavu za wageni mara tatu.
CHAMA WA MOTO
Mapema tu Simba ikapata bao la kuongoza dakika ya saba, likifungwa na Clatous Chama, akikimbia na mpira kisha kugongeana vizuri na mwenzake Anicet Oura na Mzambia huyo akafunga kwa shuti la mguu wa kushoto.
Chama akaweka bao la pili kwake lakini la tatu kwa Simba, akimalizia shambulizi zuri lililotengenezwa na Oura, akimalizia mpira uliotemwa na kipa Dalitso Phiri.
GUEYE TISHIO
Kama kuna mchezaji alikuwa mwiba kwa mabeki na viungo wa Mighty Wanderers ni winga Libasse Gueye ambaye naye alifunga mabao mawili kwenye mchezo huo.
Gueye alifunga bao la kwanza kwenye mchezo huo dakika ya 26 akimalizia krosi safi ya Oura kisha bao lake la pili na la nne kwa Simba akilifunga dakika ya 69 kwa shuti hafifu.
Achana na mabao hayo mawili, Gueye alikuwa moto kwa mbio zake akiwa na mpira ambazo wakati wote zilikuwa na faida kwa Simba kutengeneza mashambulizi makali.
SIMBA WABAYA ‘KAUNTA’
Mabao matatu ya Simba yametokana na mshambulizi ya haraka na wageni wakiwa wamepoteza mpira, zilipigwa pasi zisizozidi nne hadi bao linafungwa, wakifanya hivyo wakati wekundu hao wakifunga mabao matatu hayo ya kwanza.
MABADILIKO YAWAPA BAO WANDERERS
Baada ya kuruhusu mabao matatu, Mighty ilifanya mabadiliko manne wakitoka Blessings Singini, Lameck Mithi, Felix Zulu na Emmanuel Nyirenda.
Nafasi zao zilichukuliwa na Thiery Sama, Clement Nyondo, Mphatso Kamanga na Daniel Kudonto.
Mabadiliko hayo yakaipa nguvu kubwa Mighty Wanderers ilifanikiwa kupata bao dakika ya 34 likifungwa kwa mkwaju wa penalti kupitia Isaac Kaliati baada ya Gaddie Chirwa kuangushwa kwenye eneo la hatari na beki Rushine De Reuck.
KALETSO AMEANZA
Bao la tano na sita kwa Simba yalitokea benchi ambapo la tano lilifungwa na winga Kaletso Makgalwa aliyeingia dakika ya 76 akichukua nafasi ya Oura akitengenezewa pasi safi na Ismail Mgunda.
Bao hilo linakuwa la kwanza kwa Kaletso tangu asajiliwe Simba huku pia akitengeneza bao la sita dakika ya 90+3 akimpa pasi safi Morris Abraham ambaye aliingia dakika ya 63 akichukua nafasi ya Chama.
Ushindi huo unaipeleka Simba hatua ya pili ikienda kucheza na mshindi baina ya 15 de Agosto kutoka Equatorial Guinea na Fomboni ya Comoros.
Mechi ya kwanza ya wawili hao, 15 de Agosto ilishinda 4-0 nyumbani, marudiano ni Oktoba 3 na Simba atamfahamu mpinzani wake.