Singida Black Stars yafuzu kibabe CAFCC ikishinda 10-1
Muktasari:
- Singida leo Jumapili imeendeleza ubabe huo baada ya kuichapa Al-Ghazal mabao 3-0 katika mchezo wa marudiano uliopigwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, huku ushindi huo ukiifanya timu hiyo kufikisha jumla ya mabao 10 katika mechi hizo mbili.
SINGIDA Black Stars imefuzu hatua ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kishindo baada ya kuiondosha Al-Ghazal FC ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 10-1 katika mechi mbili za raundi ya kwanza.
Singida leo Jumapili imeendeleza ubabe huo baada ya kuichapa Al-Ghazal mabao 3-0 katika mchezo wa marudiano uliopigwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, huku ushindi huo ukiifanya timu hiyo kufikisha jumla ya mabao 10 katika mechi hizo mbili.
Katika mchezo wa kwanza uliochezwa Sudan Kusini, Singida ilitoa kipigo cha mabao 7-1, kabla ya leo kushinda 3-0 na kutinga hatua inayofuata kwa jumla ya mabao 10-1.
Singida ilianza mchezo wa leo kwa kasi, huku Al-Ghazal ikianza kwa shambulizi la kushtukiza na kupata kona katika dakika ya kwanza, lakini haikuweza kuitumia vizuri nafasi hiyo.
Baada ya hapo, Singida ilichukua udhibiti wa mchezo na kuanza kuisakama ngome ya wageni, ambapo mshambuliaji wake, Jonathan Sowah, alifungua akaunti ya mabao mapema.
Sowah, ambaye katika mchezo wa kwanza nchini Sudan Kusini alitokea benchi na kufunga mabao mawili, leo amerudia kiwango hicho kwa kufunga mabao mawili ndani ya kipindi cha kwanza.
Alifunga bao la kwanza dakika ya tatu baada ya kumalizia pasi ya kiungo mkabaji, Seydou Sacko, kabla ya kuongeza la pili dakika ya 20 kwa shuti kali kutoka nje ya boksi.
Bao hilo lilitokana na beki wa Al-Ghazal kuurudisha nyuma mpira bila kuangalia, hali iliyompa Sowah nafasi ya kuupata na kuachia shuti lililokwenda moja kwa moja wavuni.
Singida ilikwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0, lakini ilipata pigo dakika ya 38 baada ya winga wake, Ladack Chasambi, kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo.
Kocha alilazimika kufanya mabadiliko ya lazima, huku Exauce Sagesse Nzaou akiingia kuchukua nafasi yake.
Kipindi cha pili, Singida iliendelea kutawala mchezo na jitihada zake zilizaa matunda dakika ya 66 baada ya winga Mnigeria, Henry David, kufunga bao la tatu.
David aliyetikisa nyavu pia katika mchezo wa kwanza, leo amefunga kwa shuti kali la mguu wa kushoto akiwa ndani ya boksi na kuhitimisha ushindi wa Singida wa mabao 3-0.
Kwa ushindi huo, Singida imefuzu hatua ya pili kwa kishindo baada ya kuifunga Al-Ghazal kwa jumla ya mabao 10-1 katika mechi mbili.
Katika mchezo wa kwanza uliochezwa Sudan Kusini na Singida kushinda 7-1, wafungaji wa mabao ya timu hiyo walikuwa Mathew Tegisi aliyefunga matatu, Jonathan Sowah mawili, Sheikhan Khamis moja na Henry David moja.
Sasa Singida inakwenda kukutana na Tusker ya Kenya katika kuwania kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika. Mechi ya kwanza itachezwa kati ya Oktoba 16 na 18, 2026 nchini Kenya, kisha marudiano Dar es Salaam kati ya Oktoba 23 na 25, 2026. Mshindi wa jumla atafuzu makundi.
MABADILIKO NANE
Katika mchezo wa leo, Singida imefanya mabadiliko ya wachezaji nane kutoka kikosi kilichoanza mchezo wa kwanza nchini Sudan Kusini.
Wachezaji walioanza leo na hawakuanza mchezo wa kwanza ni Abdulrahman Said Hemed, Dramane Kambou, Jonathan Sowah, Seydou Sacko, Ladack Chasambi, Abdalah Mirajy, Marcel Canadi na Hussein Kazi.
Wachezaji hao walichukua nafasi za Ibrahim Imoro, Ande Cirille Koffi, Exauce Sagesse Nzaou, James Mwashinga, Sheikhan Khamis, Ahmed Bakari Pipino, Abdulmalik Zakaria na Mathew Tegisi ambao hawakuanza mchezo wa leo.
Metacha Mnata, Benjamin Jonathan Tanimu na Henry David ndio wachezaji pekee walioanza mechi zote mbili.