Prime
Simba, Yanga, Azam kupindua meza 2026/27
SIO kinyonge! Unaweza kusema hivyo kwani dirisha la usajili la msimu wa 2026-2027 lililofunguliwa Julai 6 mwaka huu, limeonyesha wazi vita ya ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara haitakuwa ya kawaida.
Yanga, Simba na Azam ambazo zilimaliza nafasi tatu za juu msimu wa 2025-2026 kama ilivyokuwa msimu wa nyuma yake, zimeingia sokoni zikiwa na lengo moja tu, kujenga vikosi vitakavyotawala ndani na kuleta ushindani mkubwa katika michuano ya CAF.
Usajili huu unaofanyika, dirisha litafungwa Agosti 15, 2026 na unatoa picha ya ushindani mkubwa ndani ya timu ambao matokeo yake utazidisha vita ya kuwania mafanikio msimu ukianza.
Hadi kufikia sasa, Yanga na Azam ndiyo timu zilizosajili wachezaji wengi zaidi ambao ni tisa kuliko Simba iliyotambulisha watano.
Mwanaspoti linakuchambulia ujio wa wachezaji hao na namna wanavyoweza kutoa changamoto kwa waliopo kwani kwa mujibu wa viongozi wa klabu, wamebakisha wachezaji wanaoamini waliokuwa bora msimu uliopita, hivyo wameleta wapya wa kuongeza nguvu ya ushindani.
YANGA
Tayari Yanga imemtambulisha mshambuliaji Cheikh Ibrahima Toure na mawinga Housseine Zakouani na Albert Kangwanda wakiwa nyota wa kimataifa, huku rais wa klabu hiyo, Injinia Hersi Said, akithibitisha kuwa bado kuna nyota wawili wa kigeni watakaotambulishwa.
Kwa wazawa ambapo Yanga imesema imeshamaliza, maingizo mapya ni winga Juma Issa Abushiri, mshambuliaji Hussein Mihambo, beki wa kulia Abdulnasir Muhamed, beki wa kati Mohamed Mussa, winga Erick Mwijage na kiungo mshambuliaji Suleiman Mbarouk maarufu Mpemba D.
Usajili huo unaonekana kufanyika baada ya tathmini ya maeneo yaliyohitaji kuongeza makali zaidi kuliko kubadilisha msingi wa kikosi. Kumbuka pia Hersi amesema katika idadi ya wachezaji 12 waliokuwa nao msimu uliopita, wamewaacha watano. Wamebaki saba ambao wanaokuja wengine watano watakamilisha idadi hiyo.
Katika safu ya ushambuliaji, Yanga kwa sasa ina Laurindo Aurelio ‘Depu’ na Emmanuel Mwanengo baada ya Prince Dube kuondoka, huku Clement Mzize akiwa bado majeruhi, ndiyo kwanza ameanza kurejea.
Depu ni mshambuliaji anayependa kucheza ndani ya boksi, lakini mara kadhaa amekuwa akihitaji kutengenezewa nafasi nyingi kabla ya kufunga.
Cheikh Ibrahima Toure anatua akiwa na sifa ya nguvu za mwili, uwezo wa kucheza karibu na lango na kushambulia mipira ya juu. Kwa mfumo ambao kocha wa Yanga, Manqoba Mngqithi kutumia maeneo ya pembeni na kati kujenga mashambulizi, mshambuliaji mwenye uwezo wa kumalizia krosi anaweza kuwa silaha kubwa.
Iwapo ataonyesha ubora aliouonyesha Saudi Arabia na Ufaransa, nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza ni kubwa. Depu atalazimika kupambana zaidi kuthibitisha thamani yake, huku Mwanengo akionekana kuwa chaguo la tatu kwa sasa.
Ukija kwenye eneo la winga, Yanga tayari ina Maxi Nzengeli na Allan Okello ambao msimu uliopita walikuwa wakicheza kikosi cha kwanza. Wakati mwingine, Pacome Zouzoua naye alikuwa akicheza kutokea pembeni kabla ya kuumia na taarifa zinasema anaweza kukosa nusu ya duru la kwanza la ligi.
Ujio wa Housseine Zakouani ambaye ni aina ya mchezaji anayependa kucheza kati ya mistari ya wapinzani, kutoa pasi za mwisho na kutengeneza nafasi, anakuja kutoa changamoto mpya baada ya Celestine Ecua kuonekana kufeli na hesabu za kuendelea kuwa hapo hazipo.
Kama kocha atahitaji ubunifu zaidi mbele ya timu zinazocheza kwa kujihami, Zakouani anaweza kuanza, lakini pia kuna ingizo jipya la Albert Kangwanda.
Kangwanda ni winga anayependa kushambulia moja kwa moja, kutumia kasi na kupiga mashuti ya mbali. Kama ataonyesha ufanisi mkubwa katika kufunga na kutoa asisti, anaweza kuanza.
Hii inatoa tafsiri kwamba, yeyote ambaye atazembea, tunaweza kuona akaonyeshwa mlango wa kutokea dirisha dogo kama ilivyokuwa kwa wachezaji waliosajiliwa dirisha kubwa Andy Boyel, Ecua na Mousa Balla Conte.
Changamoto zaidi hapa inakwenda kumkumba Edmund John na Denis Nkane aliyerejea kutokea TRA United alipokwenda kucheza kwa mkopo. Nafasi ya wazawa hawa itakuwa ndogo zaidi. Kumbuka pia kuna Mwijage, Abushiri na Mpemba D nao ni wazawa wakiwa maingizo mapya.
Hata hivyo, Maxi amekuwa mmoja wa wachezaji muhimu kutokana na uwezo wake wa kutembea na mpira na kutengeneza nafasi. Pia Okello ni fundi katika kufunga na kutengeneza nafasi, hivyo ujio wa majembe hayo mawili mapya, unaongeza ushindani mkubwa.
Kwa kuwa hadi sasa Yanga haijatambulisha mabeki katika kundi hili la wageni, nafasi za Mohamed Hussein, Chadrack Boka, Kouassi Yao, Ibrahim Hamad na Dickson Job (atakaporejea kutoka majeruhi) zinaonekana kuwa salama.
SIMBA
Simba imewasajili mshambuliaji Ibrahim Doumbia, kiungo mkabaji Kelvin Nashon, beki wa kulia Nathaniel Chilambo na kiungo mshambuliaji Bakari Msimu.
Usajili wa Doumbia umefanyika kuziba eneo la ushambuliaji baada ya Jonathan Sowah kuondoka, huku akibaki Selemani Mwalimu ambaye naye katika kumalizia msimu hakuwa akianza kikosi cha kwanza.
Doumbia anatua akiwa na jukumu la kuongeza mabao ambayo Simba imekuwa ikiyahitaji. Kutokana na kukosekana kwa washambuliaji wengi wa asili, nafasi ya Doumbia kuanza kikosi cha kwanza ni kubwa sana.
Akiwa na uwezo wa kucheza ndani ya boksi, kumiliki mipira na kuwapa nafasi mawinga kama Libase Gueye, Elie Mpanzu na Anicet Oura, anaweza kuwa silaha kuu ya Simba.
Katika kiungo cha ukabaji, Yusuph Kagoma amekuwa mhimili mkubwa. Ameongezwa Kelvin Nashon ambaye ni kiungo mwenye nguvu za mwili, uwezo wa kushinda mipira ya pili na kuanzisha mashambulizi.
Katika mechi zinazohitaji nguvu kubwa katikati, Nashon anaweza kuanza sambamba na Kagoma au hata kuchukua nafasi yake kulingana na mpinzani.
Faida yake kubwa ni kwamba anaijua vizuri Ligi Kuu Tanzania, hivyo hatahitaji muda mwingi wa kuzoea.
Usajili wa Nashon ni kuimarisha eneo hilo baada ya kuonekana kulegalega kwani Alassane Kante hakuaminiwa zaidi, pia Naby Camara hadi ameachwa.
Upande mwingine kuna mtihani anao Bakari Msimu ambaye anakuja kutoka Coastal Union akiwa mmoja wa viungo wabunifu zaidi nchini. Mbele yake wapo Clatous Chama na Morice Abraham.
Kama kocha Steve Barker atatumia mfumo wa viungo wawili washambuliaji, Bakari anaweza kupata nafasi nyingi kwa sababu Neo Maema kuna asilimia kubwa ya kutorudi baada ya mkataba wake wa mkopo kumalizika.
Lakini kama mfumo utahitaji kiungo mmoja tu wa ubunifu, atalazimika kupambana na Chama ambaye ana uzoefu mkubwa katika mechi za ushindani.
Nathaniel Chilambo amejiunga akitokea Azam FC akiwa beki wa kulia mwenye uwezo wa kushambulia. Kwa sasa Simba ina Shomari Kapombe na David Kameta ‘Duchu’.
Kapombe bado ana uzoefu mkubwa, lakini umri na ratiba ngumu vinaweza kumfanya Chilambo apewe dakika nyingi zaidi.
Iwapo ataonyesha ubora wa kupanda kushambulia na kurudi haraka kukaba, ana nafasi ya kuwa chaguo la kwanza akimuacha Duchu kusugua benchi.
AZAM
Azam ndiyo timu iliyoingia sokoni kwa nguvu zaidi. Imewasajili Taiwo Abdulrafiu, Donovan Makoma, John Mano, Hassan Mubiru, Henoc Molia, Lupini Dieumerci, Henri Stanic pamoja na kumrejesha Kipre Junior. Pia imempandisha Caleb Ilese kutoka timu ya vijana.
John Mano anatarajiwa kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji akiwa na Jean-Jacques Ngita baada ya kuondoka Jephte Kitambala.
Iwapo ataanza vizuri katika mechi za mwanzo, Mano ana nafasi kubwa ya kuwa mshambuliaji namba moja wa Azam na kuziba kabisa pengo la Kitambala.
Kiungo Donovan Makoma ni mmoja wa usajili unaovutia zaidi. Lakini eneo analokuja lina Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Yahya Zayd, huku Sadio Kanouté na Himid Mao wakicheza chini. Hii ina maana ushindani utakuwa mkubwa sana.
Makoma anaweza kucheza kama kiungo mshambuliaji au namba nane anayesukuma mashambulizi.
Katika mechi ambazo Azam itahitaji ubunifu zaidi, anaweza kuanza sambamba na Fei Toto huku Himid Mao akicheza nafasi ya kiungo wa ulinzi. Lakini kama kocha Florent Ibenge atahitaji nguvu zaidi katikati, Makoma anaweza kuanzia benchi.
Henoc Molia, KIpre Junior na Hassan Mubiru ni mawinga wanaopenda kucheza kwa kasi na kuwavaa mabeki. Kabla ya ujio wa nyota hao, Azam haikuwa na ushindani mkubwa sana kwenye maeneo ya pembeni ukilinganisha na kiungo cha kati.
Abdul Sopu, Zidane Sereri na Idd Nado ni wachezaji ambao walikuwa wakishambulia kutokea pembeni huku wakiwa wazuri katika kufunga,
Ujio wa nyota hao, kuna namna unaiona Azam ilivyoibua changamoto ya ndani ya klabu, lakini pia nje kwa wapinzani wanapokwenda kukabiliana na matajiri hao wa Chamazi, watakuwa na kazi ya ziada ya kufanya kuwazuia.
Kipre Junior anaijua Azam, anaijua ligi na anafahamu asilimia kubwa mazingira ya klabu anazokwenda kukabiliana nazo katika mashindano ya ndani.
Tofauti na wageni wengine, hatahitaji muda wa kuzoea, jambo linalompa nafasi kubwa ya kuanza mapema. Kama atakuwa na makali yaleyale, ni wazi atasumbua sana.
Kidogo kwa Caleb Ilese, kiungo huyo kijana aliyepandishwa kutoka akademi, anaweza asianze mara moja kutokana na ushindani mkubwa uliopo. Pia ndani ya Azam kuna vijana walioonesha uwezo wao msimu uliopita akiwemo Ashrafu Kibeku na Mzee Hassan.
Beki wa kushoto Taiwo Abdulrafiu atakutana na Pascal Msindo ambaye alikosa mshindani eneo hilo, hivyo kuna uwezekano Msindo akaendelea kucheza kikosi cha kwanza, au Taiwo kumpa wakati mgumu iwapo ataonyesha ubora wa kushambulia na kutoa krosi zenye ubora, ana nafasi ya kutwaa jezi mapema.
Henri Stanic na Lupini Dieumerci wanakuja kuongeza ushindani dhidi ya Twalibu Nuru Twalib, Lameck Lawi, Yoro Diaby na Yeison Fuentes katika eneo la beki wa kati.
Kutokana na ratiba ya ligi na michuano ya kimataifa, Azam itahitaji mabeki wengi wenye uwezo wa kucheza kwa kiwango sawa.
Kinachoonekana hapa, Azam eneo la beki wa kulia ni kama hawajaligusa anapocheza Lusajo Mwaikenda, lakini kwa mabeki waliowasajili, wapo wenye uwezo wa kumsaidia nahodha huyo.
Kwa mtazamo wa kiufundi, Azam ndiyo timu iliyoongeza ushindani mkubwa zaidi kwa sababu imeboresha karibu kila idara ya uwanja.
Yanga imewekeza zaidi kwenye kuongeza makali ya safu ya ushambuliaji na ubunifu wa maeneo ya mbele, huku msingi wa kikosi uliokifanya kitawale misimu iliyopita ukiendelea kubaki.
Simba nayo imejikita kujaza mapengo muhimu kwa kuleta mshambuliaji, kiungo mkabaji, beki wa kulia na kiungo mshambuliaji, usajili ambao unaweza kuifanya iwe na uwiano mzuri kati ya uzoefu na nguvu mpya.
Kinachofanya msimu wa 2026-2027 kusubiriwa kwa hamu ni kwamba hakuna tena mchezaji anayetarajiwa kupewa nafasi kwa jina pekee. Kila mmoja atalazimika kupambana mazoezini na kutumia vizuri dakika atakazopewa.
Hilo linathibitishwa na Kocha wa Yanga, Manqoba Mngqithi kwani wachezaji wa kikosi hicho wamefichua kwamba Msauzi huyo amesisitiza kuwa hakuna staa kikosini kwake, anaangalia
kiwango bora cha mchezaji, hapangiwi, kubwa zaidi anataka utimize wajibu wako.
“Kocha anataka mchezaji anayeanza au yule atakayeingia, kusiwe na tofauti ili timu icheze kwa kiwango bora, anasema atakachofanya mazoezi atakayotupa yatatusaidia kushindana uwanjani ili tuwe sawa,” alisema mmoja wa wachezaji wa Yanga.
“Kocha kashanyoosha, hata sisi ambao hatuna mwili mkubwa nafasi tunayo, jukumu letu ni kujituma tu uwanjani hana lingine, yaani kauli hii imenipa moyo sana nadhani ni kocha wa tofauti kabisa na wengine sasa nitapambana,mkubwa Mungu,” alisema mchezaji mwingine ambaye hakuwa anapata nafasi msimu uliopita.
“Tena ameongeza kuwa yeye ndio kocha mkuu, anakubali kushauriwa lakini yeye sio kocha wa kupangiwa kitu, anasema Kila kitu kitaamuliwa na benchi lake kuhusu ufundi uwanjani akishirikiana na wasaidizi wake.”