Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania V Sudan... Vita ya taji CECAFA

Muktasari:

  • Ngorongoro ambayo inaingia kwenye fainali yake ya nne ya CECAFA U-20, inatafuta taji la pili mfululizo baada ya kulibeba mwaka 2024.

HATIMAYE leo mashindano ya Afrika Mashariki na Kati kwa vijana U-20, CECAFA yanahitimishwa huku ikipigwa fainali inayowakutanisha wenyeji Tanzania maarufu Ngorongoro Heroes dhidi ya Sudan, mechi itakayoanza saa 9 jioni kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Ngorongoro ambayo inaingia kwenye fainali yake ya nne ya CECAFA U-20, inatafuta taji la pili mfululizo baada ya kulibeba mwaka 2024.

Sudan ambayo hii ni fainali yake ya kwanza katika historia, inacheza na Ngorongoro iliyobeba mataji mawili mwaka 2019 na 2024.

Safari ya Ngorongoro Heroes ilianza kwa kuifunga Rwanda mabao 3-0, kabla ya kuichapa Ethiopia 4-0 katika mchezo wa pili wa Kundi A.

Katika nusu fainali, wenyeji waliendeleza rekodi ya ushindi kwa kuifunga Burundi 2-0 kwa mabao ya Juma Abushiri na Faraji Kayanda, hivyo kufikisha mabao tisa katika mechi tatu bila kuruhusu wavu wake kutikiswa. Rekodi hiyo ndiyo inayoiweka Tanzania kama timu yenye wastani wa kufunga mabao matatu katika kila mechi.

Kwa upande wa Sudan, safari yake ilikuwa na changamoto. Ilianza kwa ushindi wa 3-0 dhidi ya Djibouti, ikapoteza 1-0 mbele ya Uganda katika mchezo wa pili wa Kundi B.

Hata hivyo, ilifuzu nusu fainali baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye kundi B ikakutana tena na Uganda ilipoichapa mabao 3-2.

Hivyo, wakati Tanzania ikiingia fainali ikiwa haijaruhusu bao katika mechi zake zote, Sudan yenyewe imefunga mabao sita na nyavu zake kutikiswa mara tatu.

Timu hizo zinaingia kwenye fainali tayari zimekata tiketi ya kucheza AFCON U-20 mwakani nchini Ghana, baada ya kushinda nusu fainali zao. Tanzania iliichapa Burundi 2-0, huku Sudan ikiifunga Uganda 3-2.


VITA YA UFUNGAJI

Kwenye takwimu za mashindano, Tanzania inaingia fainali ikiwa na nguvu kubwa kwenye eneo la ushambuliaji. Ngorongoro Heroes imefunga mabao tisa katika mechi tatu, ikianza kwa 3-0 dhidi ya Rwanda, ikafuata 4-0 dhidi ya Ethiopia na 2-0 dhidi ya Burundi.

Tanzania haijaruhusu bao katika mechi hizo tatu. Hii inaipa Ngorongoro inayofundishwa na kocha Mario Rivera Campesino picha ya timu inayoweza kushambulia na wakati huo huo kulinda faida yake.

Sudan yenyewe imefunga mabao sita katika mechi zake tatu. Iliifunga Djibouti 3-0, ikapoteza 1-0 dhidi ya Uganda katika hatua ya makundi, kabla ya kuibuka na ushindi wa 3-2 dhidi ya Uganda kwenye nusu fainali.

Hapo ndipo kwenye vita yenyewe. Tanzania imeonyesha ubora wa kupata mabao bila kuruhusu, lakini Sudan imeonyesha uwezo wa kubadilisha mwelekeo wa mchezo inapopata nafasi. Dhidi ya Uganda, Sudan ilifungwa dakika ya saba, ikasawazisha ndani ya dakika tatu, kisha ikarudi kipindi cha pili ikiwa na nguvu na kufunga mabao mawili zaidi.

Mchezaji wa kuangaliwa upande wa Sudan ni Mazin Fadul Albahli Taowr, aliyefunga mabao mawili katika ushindi huo wa 3-2 dhidi ya Uganda, likiwamo bao la ushindi dakika za mwisho.

Kinara wa mabao hadi sasa ni mshambuliaji, Amini Nshimirimana wa Burundi ambaye chama lake litacheza mshindi wa tatu dhidi ya Uganda. Nyota huyo ana nafasi kubwa ya kuibuka mfungaji bora baada ya kupachaika mabao manne tofauti ya mabao mawili na nyota wa Tanzania.

Kwa Tanzania hadi sasa ni Bashiri Kibaila, Juma Sagwe, Juma Abushiri, Faraji Kayanda ndio wanaongoza wakipachika mabao mawili kila mmoja. Nyota hao ndio wanaongoza safu ya ushambuliaji ya Ngorongoro, hivyo kama watapata nafasi ya kuonyesha ubora wao wanayo nafasi ya kuibuka wafungaji.


ENEO LA KATI

Eneo muhimu zaidi leo linaweza kuwa kiungo cha kati na nafasi nyuma ya viungo wa Sudan. Sababu ni namna Tanzania ilivyoonyesha uwezo wa kushambulia.

Kocha Rivera ameeleza kuwa timu yake inaweza kucheza kwa kumiliki mpira, kupeleka presha, kujilinda kwenye block ya kati au chini na pia kutumia mabadiliko ya haraka kutoka ulinzi kwenda kushambulia.

Dhidi ya Ethiopia, alisema Tanzania ilipata mabao kupitia mipira ya kushtukiza wakati mpinzani akiwa amepanda.

Hiyo itakuwa silaha muhimu dhidi ya Sudan, timu hiyo imethibitisha kuwa inapenda kutumia kasi inapopata nafasi, huku kocha wake Salaheldin Ahmed akiiongoza timu iliyoweza kugeuza mechi dhidi ya Uganda kutoka 1-0 hadi 3-2.

Kwa hiyo, Tanzania ikipoteza mipira kirahisi katikati, Sudan inaweza kupata nafasi ya kukimbilia kwenye nafasi zilizoachwa nyuma. Lakini Tanzania ikidhibiti eneo hilo na kuzuia mipito ya haraka, inaweza kulazimisha Sudan kucheza mchezo wa kumiliki na kujenga mashambulizi taratibu.


RIVERA VS SALAHELDIN

Hii pia ni fainali ya mbinu za makocha. Rivera ameshaonyesha kwamba hataki timu yake iwe na mfumo mmoja tu. Baada ya Tanzania kufunga mabao mawili dhidi ya Burundi, alikiri kuwa kipindi cha pili kilibadilika na timu yake ikalazimika zaidi kujilinda na kusubiri nafasi za mipira ya kushtukiza.

Kwa upande mwingine, Sudan imeonyesha kutokata tamaa. Ilipofungwa na Uganda, haikuyumba, ilisawazisha haraka na baadaye ikapata mabao mawili ya ushindi. Kocha Salaheldin anaweza kuamini uwezo wa timu yake kubaki ndani ya mchezo hadi dakika za mwisho.


TAKWIMU ZINAIBEBA TANZANIA

Tanzania inaingia fainali ikiwa na mabao tisa ya kufunga, haijaruhusu bao katika mechi tatu. Sudan ina mabao sita ya kufunga na mtatau ya kufungwa katika mechi tatu. Lakini fainali mara nyingi haiamuliwi na rekodi na historia za nyuma.

Kipimo kikubwa kitakuwa nani atakayeshinda vita ya eneo la kati, nani atakayetumia nafasi chache vizuri na nani atakayekosea kidogo na nani atatumia makosa ya mwenzie.


WASIKIE HAWA

Kocha wa Ngorongoro, Mario Rivera Campesino, alisema kikosi chake kinaendelea kuimarika mchezo baada ya mchezo, huku wachezaji wakionyesha kujiamini zaidi uwanjani.

Rivera alisema maendeleo hayo ni ishara nzuri kwa vijana hao, akiamini baadhi yao wapo karibu kupata nafasi katika timu za kulipwa kutokana na kiwango wanachoendelea kukionyesha.

Kiungo mshambuliaji wa Ngorongoro, Juma Abushiri aliwataka mashabiki kufika kwa wingi uwanjani kuwasapoti ili kutimiza lengo lao la kubeba taji hilo ingawa anaamini sio rahisi kutokana na ugumu wa timu ya Sudan.