Tanzania yafuzu AFCON U-20, ikiichapa Burundi
Muktasari:
- Ngorongoro Heroes ilianza mchezo huo kwa kasi, ikionyesha mapema nia ya kutaka kupata matokeo yatakayoipeleka kwenye fainali na kufanikisha lengo la kufuzu AFCON U-20.
TIMU ya Taifa ya Tanzania imeungana na Sudan kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 20 (AFCON U-20) 2027, baada ya Ngorongoro Heroes kuichapa Burundi mabao 2-0 kwenye nusu fainali ya pili ya michuano ya CECAFA iliyopigwa Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.
Ngorongoro Heroes ilianza mchezo huo kwa kasi, ikionyesha mapema nia ya kutaka kupata matokeo yatakayoipeleka kwenye fainali na kufanikisha lengo la kufuzu AFCON U-20.
Dakika ya 16, Juma Abushiri ‘Chugaboy’ ameifungia Tanzania bao la kwanza na kuamsha shangwe kwenye Uwanja wa Uhuru, huku Ngorongoro Heroes ikiendelea kutawala mchezo na kutengeneza nafasi zaidi mbele ya lango la Burundi.
Tanzania iliendelea kulazimisha mashambulizi na dakika ya 33, Faraji Kayanda akafungia bao la pili na kuifanya Ngorongoro Heroes kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0.
Kipindi cha pili Burundi ilijaribu kurudi mchezoni kwa kuongeza mashambulizi, lakini safu ya ulinzi ya Tanzania inayoongozwa na Abubakar Nizar 'Ninju' iliendelea kuwa imara na kuzuia juhudi za wapinzani hao kupata bao la kurejesha matumaini.
Licha ya Burundi kujaribu kulazimisha mashambulizi kipindi cha pili lakini Tanzania ilipambana haswa.
SUDAN V UGANDA
Sudan nayo imefuzu AFCON U-20 2027, baada ya kuichapa Uganda mabao 3-2 katika nusu fainali ya michuano hiyo
Mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, ulikuwa wa kusisimua baada ya Uganda kuanza kwa kasi na kupata bao la kuongoza dakika ya saba kupitia Richard Okello.
Hata hivyo, Sudan haikukaa muda mrefu, kwani Rudwan Yahya Mohamed Ishag aliisawazishia timu hiyo dakika ya 10, kabla ya timu hizo kwenda mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1.
Sudan ilirejea kipindi cha pili ikiwa na nguvu zaidi na dakika ya 47 ikapata bao la pili kupitia Mazin Fadul Albahi Taoer, aliyemalizia mpira uliomfikia akiwa karibu na lango la Uganda.
Uganda ilionyesha kutokata tamaa na juhudi zake zilizaa matunda dakika ya 65, Derrick Sssozi alipofunga bao la kusawazisha na kufanya mchezo huo kuwa 2-2.
Wakati kila upande ukionekana kusaka bao la ushindi, Sudan ilipigwa dakika ya mwisho dakika ya 83 kupitia Albahi Taoer, aliyefunga bao lake la pili katika mchezo huo na kuipa Sudan ushindi wa mabao 3-2.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Taoer amesema alifurahishwa na kufunga mabao mawili yaliyoiwezesha Sudan kutinga AFCON U-20.
“Nina furaha sana kwa sababu nimefunga mabao mawili na kusaidia Sudan kufuzu AFCON,” amesema Taoer.
Kocha wa Sudan, Salaheldin Ahmed Nuoreldin Ahmed, amewashukuru wachezaji wake kwa kazi kubwa waliyoifanya katika mchezo huo, akisema hawakuwa na kazi rahisi dhidi ya Uganda.
“Haikuwa mechi rahisi, lakini tunamshukuru Allah kwa kutuongoza kufuzu AFCON U-20,” amesema Ahmed.