Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania v Burundi: Mechi ya kuitafuta tiketi ya AFCON U-20

CECAFA Pict

Muktasari:

  • Tanzania itaikaribisha Burundi saa 12 jioni, huku Uganda ikiumana na Sudan kwenye nusu fainali nyingine ya kutafuta zitakazokwenda fainali na mechi zote zikipigwa Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.

YULE mshindi atakayeuwakilisha Ukanda ya Afrika Mashariki na Kati kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana AFCON U-20 anapatikana leo kwenye mechi za nusu fainali.

Tanzania itaikaribisha Burundi saa 12 jioni, huku Uganda ikiumana na Sudan kwenye nusu fainali nyingine ya kutafuta zitakazokwenda fainali na mechi zote zikipigwa Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.

Timu mbili zitakazofika fainali ndizo zitapata tiketi za kuiwakilisha CECAFA kwenye AFCON U-20 2027 zitakazofanyika Ghana.

Kwa Ngorongoro Heroes, ilianza kampeni zake kwa kushinda Rwanda 3-0 na Ethiopia 4-0, ikifunga mabao saba bila kuruhusu bao ikionyesha inaweza kukabiliana na timu ngumu.


NGORONGORO Pict

ITAKAPOAMULIWA

Sehemu kubwa ya mechi hii inaweza kuamuliwa kwa namna Tanzania itakavyoweza kuvunja safu ya ulinzi ya Burundi bila kuacha mianya nyuma.

Burundi haijaruhusu bao katika mechi zake mbili za kundi, ikiifunga Sudan Kusini 4-0 na Kenya 2-0. Katika ushindi dhidi ya Kenya mabeki Cadeau Ndayishimiye na Radjabu Nzeyimana walikuwa sehemu muhimu ya safu ya ulinzi iliyowapa wapinzani wakati mgumu.

Hivyo, kasi ya Chugaboy, ubunifu wa Casemiro, nguvu ya Kibaila na uwezo wa Sagwe kutumia nafasi utakuwa muhimu.

Tanzania imeonyesha inaweza kufunga, lakini sasa inakutana na timu ambayo pia imeonyesha inaweza kulinda lango kwa nidhamu kubwa.

Ngorongoro haitakiwi kumpa Burundi nafasi ya kushambulia kwa urahisi. Takwimu ya mabao manne ya Amini Nshimirimana katika mechi mbili imetoa picha halisi. Nahodha huyo alifunga mara mbili katika ushindi wa 4-0 dhidi ya Sudan Kusini, kisha akafunga tena mabao mawili dhidi ya Kenya.


NGORO 02

WA KUANGALIWA

Nshim irimana ndiye jina linaloongoza kwenye kikosi cha Burundi baada ya kufunga mabao yote manne ya timu yake katika michezo miwili ya hatua ya makundi. Katika mechi dhidi ya Kenya, alifunga bao la kwanza dakika ya 10 na kuongeza la pili dakika ya 68, huku Burundi ikishinda 2-0.

Lakini Tanzania haitakiwi kumuangalia yeye pekee. Sympathque Majidi pia alionyesha uwezo mkubwa kwenye mechi ya kwanza dhidi ya Sudan Kusini, akifunga mabao mawili baada ya mapumziko na kukamilisha ushindi wa 4-0. 

Hivyo, Ngorongoro itakuwa na kazi ya kuwadhibiti wachezaji hao wawili huku ikihakikisha safu yake ya nyuma haivutwi nje ya nafasi.


CECA 01

BURUNDI JE?

Burundi imeingia nusu fainali ikiwa na rekodi safi ya ushindi wa mechi mbili, mabao sita ya kufunga ikiwa haijaruhusu bao. Ilianza kwa kuifunga Sudan Kusini 4-0 kabla ya kuifunga Kenya 2-0.

Kinachoonekana kwenye Burundi ni timu inayoweza kubadilika kutoka kujilinda kwenda kushambulia. Dhidi ya Kenya, ilifunga mapema na baadaye ikaendelea kuwa imara nyuma hadi kupata ushindi mwingine wa bila kuruhusu bao. Hilo linaifanya Tanzania kuwa na jukumu la kuwa makini katika kila vipindi vya mchezo.


NGORO 03

MTIHANI WA NGORONGORO

Kwa Tanzania, mchezo huu utahitaji zaidi ya ubora wa kufunga mabao. Ngorongoro itahitaji uvumilivu iwapo Burundi itakaa nyuma na kuilazimisha kutafuta nafasi katika maeneo yenye msongamano.

Kibaila anaweza kuwa muhimu kwenye eneo la mwisho, hasa kutokana na uwezo wake wa kuingia kwenye eneo la hatari. Sagwe tayari ameonyesha uwezo wa kufunga na kutengeneza nafasi, wakati Chuga Boy anaweza kutumia kasi yake pembeni kujaribu kuvunja safu ya ulinzi.

Casemiro naye atakuwa na jukumu la kuunganisha safu ya kiungo na washambuliaji, huku Ninju na walinzi wenzake wakibeba jukumu la kuhakikisha Nshimirimana na Majidi hawapati nafasi rahisi.


UGANDA V SUDAN

Nusu fainali nyingine itawakutanisha Uganda na Sudan, timu ambazo tayari zilicheza hatua ya makundi. Uganda iliibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Sudan na kumaliza kileleni mwa Kundi B.

Uganda, chini ya kocha Laryea Kingston, ilianza mashindano kwa kuifunga Djibouti 4-1, kabla ya kupata ushindi huo wa bao moja dhidi ya Sudan. Isima Magala alifunga mara mbili dhidi ya Djibouti, huku Uganda ikionyesha uwezo wa kupata mabao na pia kudhibiti mchezo.

Sudan itakuwa na kazi ya kurekebisha yaliyotokea kwenye hatua ya makundi. Kwa kuwa tayari wamekutana, kila upande unafahamu sehemu ambazo mwenzake anaweza kutumia, hivyo maandalizi ya kiufundi na utekelezaji uwanjani vitakuwa muhimu.


NGORO 04

SAFARI MUHIMU

Kwa Tanzania na Burundi, mchezo huu ni zaidi ya kutafuta ushindi wa nusu fainali. Ni hatua inayowapa tiketi ya AFCON U-20. Tanzania inaingia ikiwa na mashambulizi yaliyofunga mara saba bila kuruhusu bao, wakati Burundi imefunga sita bila kuruhusu bao katika michezo yake miwili.

Hapo ndipo kazi ya Ngorongoro itakapokuwa: kuvunja safu ya ulinzi ya Burundi huku ikimzuia Nshimirimana, Majidi na wenzake kupata nafasi. Tanzania ikidhibiti maeneo hayo mawili, itakuwa imeweka msingi mzuri wa safari yake kuelekea fainali; lakini Burundi nayo imeonyesha katika michezo miwili kwamba si timu rahisi kufunguka. Hivyo, Uhuru kesho utakuwa uwanja wa kuamua nani atasogea hatua moja zaidi kuelekea Ghana.


NGORO 01

WASIKIE HAWA

Nahodha wa timu hiyo,Arafat Ally alisema wanafahamu umuhimu na ugumu wa mechi kwani hiyo itawapa tiketi ya kufuzu kucheza mashindano ya Afrika.

“Ni mechi ngumu lakini tumejiandaa vizuri kuhakikisha tunashinda mechi hiyo japo sio rahisi kutokana na ubora wa wapinzani wetu, hatujapishana sana kwa sababu nayo haijaruhusu bao kwenye makundi lakini pia imefunga mabao mengi kwa hiyo tuna kazi ya ziada.”