Tanzanite Queens yaandika rekodi ikifuzu Kombe la Dunia
Muktasari:
- Kwenye mechi hiyo, Tanzanite Queens iliingia ikiwa nyuma kwa mabao 3-1 dhidi ya Cameroon ambao walicheza vyema mechi ya kwanza iliyopigwa Mei 2, 2026 kwenye Uwanja wa Ahmadou Ahidjo, Yaounde nchini Cameroon, hivyo leo ilikuwa kufa kupona timu hiyo ishinde mabao 2-0 ili ifuzu.
HATIMAYE Timu ya Soka ya Taifa Wanawake Tanzania chini ya miaka 20, Tanzanite Queens, imefuzu kushiriki Kombe la Dunia, baada ya kuitandika Cameroon mabao 2-0 mechi iliyopigwa leo Mei 10, 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Kwenye mechi hiyo, Tanzanite Queens iliingia ikiwa nyuma kwa mabao 3-1 dhidi ya Cameroon ambao walicheza vyema mechi ya kwanza iliyopigwa Mei 2, 2026 kwenye Uwanja wa Ahmadou Ahidjo, Yaounde nchini Cameroon, hivyo leo ilikuwa kufa kupona timu hiyo ishinde mabao 2-0 ili ifuzu.
Mabao mawili ya Tanzanite Queens yalifungwa na Mary Aron na Hasnath Ubamba ambaye amekuwa mhimili muhimu kwenye eneo la ushambuliaji la timu hiyo.
Tanzania Queens inaweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza Afrika Mashariki kufuzu kucheza Kombe la Dunia Wanawake U20, lakini inakuwa timu ya pili baada ya mwaka 2022 Timu ya Taifa ya Wasichana chini ya miaka 17 kufanya hivyo.
Tena timu zote hizo zimefanikiwa kufuzu Kombe la Dunia Wanawake kwa kuifunga Cameroon na kuonesha taifa hilo ni kama daraja la Tanzania upande wa wanawake.
Mara ya kwanza Tanzania kukutana na Cameroon mwaka 2022 Timu ya Taifa ya Wasichana chini ya miaka 17 ilifuzu Kombe la Dunia Wanawake U-17, fainali zilizofanyika India na kuishia robo fainali.
Katika harakati za kufuzu mashindano hayo, Tanzania iliiondosha Cameroon kwa jumla ya mabao 5-1 baada ya kushinda 4-1 ugenini na baadaye 1-0 nyumbani kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Hivyo Tanzanite Queens inakuwa miongoni mwa timu nne zitazowakilisha Afrika kwenye michuano hiyo mikubwa duniani, timu nyingine zilizofuzu ni Ghana iliyoitoa Uganda kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda mabao 2-1 nyumbani na kutoa sare ya 1-1 ugenini.
Nyingine ni Nigeria ilifuzu kwa kuichapa Malawi jumla ya mabao 3-2. Inayosubiriwa ni mechi ya Ivory Coast dhidi ya Benin itakayopigwa baadae ili kumpata mwakilishi wa mwisho ambapo timu hizo zilitoshana nguvu kwa sare ya 1-1 mechi ya kwanza.
Hii ni mara ya kwanza Tanzanite inafuzu kucheza Kombe la Dunia kwa umri huo na katika timu hizo Tanzania pekee ndio timu changa kwenye michuano hiyo.
Ghana inakwenda kucheza Kombe la Dunia U20 mara ya nane baada ya mwaka 2010, 2012, 2014, 2016, 2018, 2022, 2024, huku Nigeria ikifuzu mara 12 (2002, 2004, 2006, 2008, 2010, 2012, 2014, 2016, 2018, 2022, 2024 na sasa 2026).