Twiga Stars yaichapa Afrika Kusini 2-1 WAFCON ikiandika ushindi wa kwanza
Muktasari:
- Ushindi huo ni wa kwanza kwa Tanzania katika historia ya ushiriki wake WAFCON tangu ilipoanza kushiriki michuano hiyo mwaka 2010.
HATIMAYE historia imeandikwa. Timu ya Taifa ya Wanawake Tanzania 'Twiga Stars' imeanza kwa kishindo kampeni yake ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2026 baada ya kuichapa Afrika Kusini kwa mabao 2-1 katika mchezo wa Kundi B uliochezwa kwenye Uwanja wa Moulay Rachid, Casablanca, Morocco.
Ushindi huo ni wa kwanza kwa Tanzania katika historia ya ushiriki wake WAFCON tangu ilipoanza kushiriki michuano hiyo mwaka 2010.
Vilevile ni mara ya kwanza kwa Twiga Stars kuifunga Afrika Kusini katika mashindano hayo ikiwa ni hatua kubwakwa maendeleo ya soka la wanawake nchini.
Kiungo Diana Msewa ameifungia Tanzania bao la kwanza dakika ya 38 baada ya Twiga Stars kucheza kwa kujiamini na kuwabana mabingwa hao wa zamani wa Afrika.
Afrika Kusini ilijitahidi kufanya mashambulizi makubwa na dakika ya 45 ikafanikiwa kusawazisha kupitia kwa beki Bambanani Mbane.
Kipindi cha pili kocha Bakari Shime amefanya mabadiliko dakika ya 50 kwa kumtoa Asha Mwalala na kumuingiza mshambuliaji Hasnath Ubamba yaliyozaa matunda na dakika ya 87 ameiandikia Tanzania bao la pili na la ushindi.
Kinachovutia zaidi ni kwamba wafungaji wote wawili wa Twiga Stars wanacheza soka la kulipwa Ulaya, Msewa akikipiga Trabzonspor ya Uturuki, huku Ubamba akiitumikia Madrid CFF inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake Hispania.
Kwa ushindi huo, kocha Shime na wasaidizi wake Esta Chabruma na Edna Lema wameandika rekodi kwa kuwa benchi la kwanza la ufundi la Twiga Stars kuifunga Afrika Kusini WAFCON.
Kabla ya mchezo huo, Tanzania na Afrika Kusini zilikuwa zimekutana mara mbili kwenye WAFCON.
Mwaka 2010, Afrika Kusini ilishinda mabao 2-1, huku 2024 mechi ilimalizika kwa sare ya bao 1-1.
Ushindi huo umeifanya Tanzania kuvunja rekodi hiyo na kupata ushindi wake wa kwanza dhidi ya wapinzani hao.
Rekodi nyingine iliyowekwa ni kwamba Twiga Stars imepata ushindi wake wa kwanza katika historia ya WAFCON.
Iliposhiriki kwa mara ya kwanza 2010 ilipoteza mechi zote tatu za hatua ya makundi, huku 2024 ikikusanya pointi moja baada ya sare moja na kupoteza mechi mbili.
Mwanzo huo mzuri umeongeza matumaini ya Tanzania kufanya vizuri zaidi katika WAFCON 2026. Kuibuka na ushindi dhidi ya Afrika Kusini, ambayo ni moja ya mataifa yenye historia kubwa katika soka la wanawake barani Afrika.