Prime
Vita ya ubingwa Simba yatoa msimamo, yapendekeza mawili TPLB
UKIZUNGUMZA na mashabiki wa Yanga akili yao ipo kwenye kuutafuta ubingwa wa tano mfululizo wa Ligi Kuu Bara na upande mwingine ukiwatafuta wale wa Simba, hakuna wanachotaka kusikia zaidi ya kumaliza ukame na kubeba ubingwa huo msimu huu, timu hizo zikitofautiana kwa pointi mbili tu. Wakati hali ikiwa hivyo, Simba wametoa msimamo wao.
Katika msimamo wao huo, Simba imetaka mechi zilizobaki ziamuliwe kwa haki, pia ikifanya kikao na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) juu ya masuala ya upangaji wa ratiba nao usiwe wa kukandamiza timu moja na kuibeba nyingine.
Simba yenye pointi 58 ikishika nafasi ya pili, imeendelea kuweka presha kwa vinara wa ligi hiyo, Yanga wenye pointi 60 katika kuwania ubingwa, zote zikicheza mechi 25 na zimekuwa zikishushana katika msimamo huo kila moja ikionyesha haitaki kufanya makosa katika kuangusha pointi, zikibakiza mechi tano pekee kabla ya kumaliza msimu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Crescentius Magori ametoa msimamo kuwa malengo ya klabu hiyo ni kuendelea kuwinda makombe mawili yaliyosalia ambayo ni Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la CRDB.
Magori alisema katika kuyasaka makombe hayo, Simba inataka mechi zilizosalia za kumalizia msimu zichezwe kwa haki kwa timu iliyostahili kushinda ipate ushindi wake, huku akiwataka mashabiki wa Wekundu hao kujaa uwanjani.
“Malengo yetu ni tunaendelea kuviwania vikombe vyote vilivyosalia, ukweli ni kwamba ni mechi ngumu zenye ushindani sana, Simba tunaomba usawa kwenye kila mchezo, timu iliyo bora ishinde, hicho ndicho cha muhimu kwetu,” alisema Magori.
“Mashabiki wa Simba waje kwa wingi uwanjani wajae, sina tatizo na viwanja vya mikoani, mwitikio umekuwa mkubwa sana, mashabiki wa hapa nyumbani Dar es Salaam wajue tunacheza Uwanja wa KMC ndio uwanja wetu wa nyumbani, waje mchezo ujao tutacheza Juni 14.”
Aidha Magori aliweka wazi licha ya Simba kuufukuzia ubingwa wa ligi, lakini bado haupo kwenye mikono yao na kama kila timu itashinda mechi zake, Yanga itakuwa bingwa kutokana na kutofautiana kwa pointi mbili huku akisema wanaiombea ianguke.
“Ubingwa hauko mikononi mwetu kwa sababu hata tukishinda mechi zote na mwenzetu (Yanga) ikishinda mechi zote ina maana ubingwa watachukua wao, lakini tunaamini ligi ni marathoni, wewe utashinda na sisi tutashinda.
“Hakuna anayejua, sisi tunaweza kupoteza au kupata sare na wao hayo pia yanaweza kutokea, kwa hiyo hadi sasa ni vigumu kutabiri, hata sisi kuna mechi hatukutarajia kuangusha pointi lakini ilikuwa hivyo, sisi tunaomba ikiwezekana mwenzetu afanye makosa, wateleze na sisi tushinde ili tuwe mabingwa.
“Suala la kukosa ubingwa kwa muda mrefu linatuumiza kila mmoja, ukiangalia mashabiki wetu, sisi viongozi na hata wachezaji wetu wana kiu ya kuona tunamaliza ukame huu wa makombe zaidi hasa huu ubingwa wa ligi,” alisema Magori.
KIKAO NA BODI YA LIGI
Akizungumzia ratiba ya ligi, Magori alisema Simba imefanya mkutano na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) ikipendekeza mambo mawili na la kwanza ni juu ya upangwaji wa ratiba hiyo, ikionyesha hairidhishwi na mambo yanavyofanyika.
Magori alisema eneo lingine ambalo waliliangalia ni juu ya mabadiliko ya viwanja kwa baadhi ya timu na ikiona kama kuna baadhi ya klabu zinabadilishiwa viwanja kutokana na kutafuta wepesi katika mechi zao.
“Tulikaa kikao na Bodi ya Ligi kwa sababu tulihisi kuna vitu vinatakiwa vifanyike hasa msimu ujao kwa sababu kuna vitu tulikuwa tunaviona, sijui kama nyie mmeliona hili ratiba yetu sasa ilikuwa Yanga anacheza halafu Simba anafuata, hii imeshamiri sana, sasa haya ni makosa ya kutengenezwa na mtu.
“Yaani kuna kitu kimetengenezwa. Wakati nikiwa makamu wa kwanza wa rais wa TFF tayari kulikuwa na program ya kisasa ya kupanga ratiba. Ile programu ukiweka inakupa ratiba lakini wakati ule tulikuwa tunaogopa kwa sababu klabu nyingi zilikuwa hazina uwezo hata wa kusafiri, tumependekeza kwa maandashi ratiba ipangwe kwa kutumia programu hii ya kisasa ili kuondoa mambo yanayoendelea sasa isipangwe na mtu au watu.
“Pendekezo letu la pili lilikuwa kila timu mechi zake zichezwe kwenye viwanja sawa, kuna timu leo inafika inatakiwa kucheza kwenye uwanja mgumu, inatafutwa sababu ule uwanja unafungiwa na haiendi huko, mchezo husika unakwenda kuchezwa kwenye uwanja huru, hapo haitapata ule ushindani ambao ingeupata kama ingecheza kwenye uwanja ule ulioondolewa.
“Baada ya muda sisi tukienda kucheza ule uwanja, utasikia umefunguliwa, wewe unakwenda kucheza kwenye uwanja ambao mwenzako ameukimbia, unaweza kukuta kuna timu inacheza kwenye viwanja huru katika mechi tatu na wewe hupati hiyo, sasa hapo hakuna usawa, tumewataka bodi kuliangalia kwa umakini,” alisema Magori.
Simba iliyobeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara 22, imekuwa na ukame wa kubeba taji hilo kwa misimu minne mfululizo na mara ya mwisho ililichukua msimu wa 2020-2021. Baada ya hapo, Yanga imechukua mara nne mfululizo 2021-2022, 2022-2023, 2023-2024 na 2024-2025.
Ikiwa katika ukame huo wa mataji, Simba pia ilichukua mara nne mfululizo ikiwa ni 2017-2018, 2018-2019, 2019-2020 na 2020-2021.