Wizara ya Maliasili na Utalii mguu sawa kuelekea AFCON 2027
Muktasari:
- Uboreshahi wa miundombinu ndani ya hifadhi zilizopo hapa nchini utatoa fursa ya kufikia malengo ya Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kufikisha idadi ya watalii milioni 8 ifikapo mwaka 2030 na kuchagiza ongezeko la pato la taifa wakati na baada ya fainali za AFCON 2027 zitakazofanyika Tanzania kwa kushirikiana na Kenya na Uganda.
WIZARA ya Maliasili na Utalii, imewahakikishia wawekezaji na wadau wa michezo ushirikiano wa kutosha kuwezesha ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya kisasa ili kuongeza thamani ya vivutio vya utalii vilivyopo hapa nchini.
Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Utalii, Nkoba Mabula, ameyasema hayo alipokutana na kuzungumza na mmiliki wa Kampuni ya Tilo World Properties Holding Limited kutoka nchini China, inayojihusisha na uwekezaji wa utoaji wa huduma za malazi ndani na nje ya hifadhi.
Mabula ameongeza kuwa wakati Tanzania ikiwa katika maandalizi ya Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) 2027, Wizara inahitaji kufanya uwekezaji mkubwa kwenye maeneo ya utalii ili kuongeza thamani katika hifadhi zake.
Miongoni mwazo ni Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Hifadhi ya Taifa Arusha, Msitu wa Asili Pugu Kazimzumbwi, eneo la Wizara Kigamboni na Msitu wa Pande ili kuwa na vivutio vipya vya utalii hususan katika kipindi hiki ambacho Tanzania inajiandaa na AFCON 2027 ili kupata wageni wengi ikiwemo wachezaji maarufu wa timu za taifa.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Adamu Deng, amesema uwekezaji huo umelenga kuanza kufanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa kujenga kambi ya kudumu ya watalii (Permanent Camp) yenye vyumba 50 utakaogarimu kiasi cha Dola za Marekani milioni tatu (Sh7.8 bilioni za Tanzania) na utakaokamilika ndani ya miezi nane hadi kumi na mbili.
Uboreshahi wa miundombinu ndani ya hifadhi zilizopo hapa nchini utatoa fursa ya kufikia malengo ya Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kufikisha idadi ya watalii milioni 8 ifikapo mwaka 2030 na kuchagiza ongezeko la pato la taifa wakati na baada ya fainali za AFCON 2027 zitakazofanyika Tanzania kwa kushirikiana na Kenya na Uganda.