Yanga yapitisha bajeti ya Sh36 bilioni kwa msimu wa 2026/27
Muktasari:
- Bajeti hiyo iliwasilishwa katika Mkutano Mkuu wa klabu na Mhasibu Mkuu wa Yanga, Justina Kubila, ambaye alisema fedha hizo zitawezesha klabu kutekeleza malengo yake ya ushindani ndani na nje ya nchi.
Yanga imeweka wazi mipango yake mikubwa kwa msimu wa 2026/27 baada ya kupitisha bajeti ya Sh36 bilioni, ikiwa ni ongezeko la Sh3 bilioni kutoka bajeti ya Sh33 bilioni iliyotumika msimu uliopita.
Bajeti hiyo iliwasilishwa katika Mkutano Mkuu wa klabu na Mhasibu Mkuu wa Yanga, Justina Kubila, ambaye alisema fedha hizo zitawezesha klabu kutekeleza malengo yake ya ushindani ndani na nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Kubila, Yanga inatarajia kukusanya Sh20.6 bilioni kupitia vyanzo mbalimbali vya mapato, ikiwemo udhamini, mapato ya mechi, zawadi za mashindano na shughuli nyingine za kibiashara.
Katika upande wa matumizi, sehemu kubwa ya fedha hizo imetengwa kwa ajili ya mishahara na marupurupu ya wachezaji pamoja na wafanyakazi, ambapo klabu imepanga kutumia Sh13.1 bilioni.
Yanga pia imeonyesha dhamira ya kuendelea kuimarisha kikosi chake kwa kutenga Sh8.7 bilioni kwa shughuli za usajili na uhamisho wa wachezaji.
Kwa upande wa motisha, klabu imetenga Sh3.9 bilioni kwa ajili ya bonasi za wachezaji na benchi la ufundi ili kuongeza ari ya ushindani katika mashindano mbalimbali.
Maandalizi ya mechi, yakiwemo usafiri, malazi na chakula, yamepangiwa Sh5.7 bilioni, huku Sh1.1 bilioni zikitengwa kwa ajili ya gharama za masuala ya kisheria.
Aidha, Yanga imetenga Sh822 milioni kwa ajili ya kambi za timu katika maandalizi ya msimu mpya.
Bajeti hiyo inaonyesha azma ya mabingwa hao kuendelea kuwekeza kwa nguvu katika kikosi na miundombinu ya uendeshaji, wakilenga kufanya vizuri kwenye mashindano ya ndani na kimataifa msimu ujao.