Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TFF imefanya uamuzi wa Lodi Lofa

ZENGWE Pict


Kulikuwa na gazeti moja kila mwezi lililopata umaarufu kutokana na katuni zake kuwa na vichekesho vinavyovutia, kikiwemo cha mtu mmoja aliyekuwa anaitwa Lodi Lofa.


Lodi Lofa alikuwa akifikiria kila kitu kwa mtazamo wa fedha na fikra zake zilikuwa, fedha ni kila kitu katika maisha, akiamini zinaweza kutatua matatizo yote.


Katika katuni moja, Lodi Lofa alienda kuangalia mechi ya mpira wa miguu. Akashangaa kuona wachezaji 22 wakipambana kuupata mpira mmoja. Kwa akili zake za kilofa alidhani wale wachezaji walikuwa wanahangaika kwa sababu hakuna mipira ya kutosha, hivyo akaondoka zake na kwenda kununua mipira mingine 21 ili kila mchezaji awe nao wake badala ya kuhangaika kugombea mpira mmoja.

Alijua tatizo la fedha ndilo lililosababisha wachezaji 22 wagombee mpira mmoja. Akaenda kuwakabidhi wasimamizi wa mechi, akisema haiwezekani wachezaji 22 wagombee mpira mmoja. Hizo zilikuwa ni akili za kilofa za mtu tajiri.

ZENG 01

Hakujishughulisha kujua utamu wa mchezo wa mpira wa miguu uko wapi wala sababu za mchezo huo kutumia mpira mmoja. Akaenda kutafuta suluhisho bila ya kujua tatizo ni nini.

Ndivyo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilivyotumia akili hiyo kutengeneza kanuni mpya ya kudhibiti timu zinazogomea kuingiam kwenye vyumba vya kuvalia nguo badala ya kujishughulisha kutafuta tatizo ni nini na suluhisho lake liweje.

Hata kabla ya kujua tatizo ni nini, TFF imekuja na suluhisho kama la Lodi Lofa; timu itakayogomea kuingia vyumba vya kubadilishia nguo itakatwa pointi tano! Hili suluhisho sijui wamelitoa katika miongozo gani wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu?

ZENG 03

TFF haijajishughulisha hata kufanya utafiti kujua ni kwa nini timu hugomea kuingia vyumba vya kubadilishia nguo. Na inakuwaje hadi timu kubwa Afrika kama Al Ahly ya Misri na TP Mazembe hugomea kuingia vyumba vya kubadilishia nguo zinapokuja kucheza na timu za Tanzania katika mechi za mashindano ya Afrika.

Hata kabla haijajua kiini cha tatizo, imeibuka na suluhisho kama vile Lodi Lofa, ikiamini kwa kuwa ina mamlaka inaweza kutunga kanuni ya kuipokonya pointi timu kirahisi (kama ile ya kwenda kununua mipira 21 ili kila mchezaji awe nao wake).

Si kitu rahisi kiasi hicho katika mpira wa miguu kuipokonya timu pointi eti kwa sababu haijaingia vyumba vya kubadilishia nguo. Pointi hazipokwi hovyo katika utamaduni wa mpira wa miguu.

Ni makosa machache sana husababisha timu kupokwa pointi na huwa kuna mlololongo wa mchakato kabla ya kufikia uamuzi wa kuipokonya timu pointi. Kwa mfano, Manchester City inakabiliwa na kesi nzito yenye mashtaka 115 inayotokana na ukiukwaji wa kanuni za fedha.

ZENG 04

Ikipatikana na hatia inaweza kupokonywa pointi au kushushwa daraja bila ya kujali makosa hayo yalifanyika msimu gani. Kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu sasa, keshi hiyo imekuwa ikiendelea bila ya kufikia ukomo kwa kuwa adhabu yake inaweza kuiathiri timu kwa kiasi kikubwa na hivyo ni lazima kuwa makini kuangalia kila kitu sawasawa kabla ya kufikia hitimisho.

Hiyo inaonyesha ni kwa kiasi gani suala la kupokonya pointi ni nyeti sana katika mpira, hasa kutokana na ukweli pointi hizo hutafutwa kwa udi na uvumba, kifedha, kisikolojia, kimchezo na mambo mengine mengi.

Klabu ikatumia mabilioni ya fedha kununua wachezaji, ikatumia mabilioni ya fedha kuwalipa wachezaji, ikatumia mabilioni ya fedha kuwalipa makocha, kugharimia kambi, kugharimia safari za timu, kuzunguka nchi mbalimbali kusaka wachezaji, kulipa mawakala na mambo mengine mengi, halafu watu waliokaa mezani waje waipokonye pointi eti kwa sababu ya tatizo ambalo hawakuhangaika kulifanyia utafiti?

Kosa jingine linaloweza kusababisha timu ipokonywe pointi ni lile la kumchezesha mchezaji batili, ama kutokana na kuwa na kadi zinazomzuia kucheza mechi, ama dosari katika usajili au jambo lolote linaloondoa uhalali wa kucheza. Hapo anakuwa ametumika mchezaji batili na hivyo kuipokonya timu pointi kwa kosa hilo hakuhitaji mchakato mrefu.

ZENG 02

Kosa jingine ni la kupanga matokeo, hasa linapofanywa na timu tofauti na linalofanywa na waamuzi. Kama wachezaji walichukua rushwa ili timu yao ipoteze mchezo, hapo ni moja kwa moja kupoteza ushindi. Na pia inaweza kuwa ni viongozi walihusika katika mpango huo kama ilivyokuwa kwa Juventus ya Italia na Olympique Marseile ya Ufaransa.

Lakini hali huwa tofauti inapobainika refa ndio alihusika kama ilivyokuwa kwa mwamuzi Robert Hoyzer wa Ujerumani, ambaye alikiri kuhusika kupanga matokeo ya mechi za Ligi Kuu na Kombe la Ujerumani. Hakuna timu ilipokonywa ushindi wala kushushwa daraja.

Kwa hiyo kunatakiwa uchambuzi wa kina na mijadala mingi kuhusu kanuni hiyo ya kupokonya pointi kabla ya kuihalalisha. Haiwezekani kanuni ikazuka tu usiku mmoja na asubuhi yake kutangazwa itaanza msimu ujao.

Ilitakiwa ijadiliwe katika ngazi mbalimbali, ikihusisha na klabu zinazofanya vitendo hivyo vya kugomea kuingia vyumbani na zile zinazotuhumiwa kuhusika ama kupulizia dawa au kufanya vitendo vya kimazingara. Pia kujua kama tatizo hilo limesambaa kiasi gani Afrika na duniani na limeshughulikiwa vipi.

TFF ilishawahi kujaribu kukodisha kampuni binafsi ilinde vyumba vya kubadilishia kwa siku nzima hadi kuamkia siku ya mechi na kupata taarifa kama kuna watu walijaribu kutaka kuingia ama kwa ajili ya kupuliza dawa au kufanya vitendo vya kishirikina? Maana kama ni kupuliza dawa hilo laweza kuwa kosa la jinai na kama ni ushirikina laweza kushughulikiwa kwa kujenga utamaduni ili kuhakikisha mshindi anapatikana uwanjani na si mezani.

Kufikia uamuzi wa kupokonya pointi tano timu kwa kosa ambalo halikuathiri mwenendo wa mchezo au halijafanyika uwanjani, si jambo rahisi kiasi hicho katika mpira wa miguu.

Jitihada zinatakiwa zifanyike ili timu zipate ushindi uwanjani na si kwa namna nyingine yoyote.

Ni muhimu kwa TFF kuzuia kwanza kanuni hiyo isiyoendana na utamaduni wa mpira wa miguu na kufanya utafiti wa kina wa tatizo hilo badala ya kuibuka na majibu mepesi ya tatizo kubwa.

Si kila tatizo linaweza kuondolewa kwa adhabu kali na ambayo inakiuka misingi ya mchezo wa mpira wa miguu. Wenye mamlaka hawana budi kuelewa mamlaka yanatakiwa kutumika kwa akili na busara na si kwa uamuzi wa kukurupuka.