Ana Martins, mke na mtetezi namba moja wa Guimaraes
Muktasari:
- Bruno mwenye umri wa miaka 28 kwa sasa, alianza kuonekana hadharani na Ana miaka takribani sita iliyopita ila kwa wakati huo hakuwa na nguvu kubwa ya ushawishi kwa mashabiki kwa sababu hakuwa akiichezea klabu yenye mashabiki wengi.
KWA sasa Bruno Guimaraes anategemewa kuja kuwa mmoja wa wachezaji muhimu katika kikosi cha Arsenal, lakini wakati uwezo wake uwanjani ukiendelea kumfanya kuwa staa, upande wa pili wa maisha yake umekuwa ukiwavutia mashabiki hasa anavyoishi na mke wake, Ana Martins.
Bruno mwenye umri wa miaka 28 kwa sasa, alianza kuonekana hadharani na Ana miaka takribani sita iliyopita ila kwa wakati huo hakuwa na nguvu kubwa ya ushawishi kwa mashabiki kwa sababu hakuwa akiichezea klabu yenye mashabiki wengi.
Wawili hao wote wanatokea nchini Brazil lakini kwa wakati huu makazi yao yapo London, huku wakiwa tayari wamejaliwa kupata watoto wawili katika ndoa yao iliyofungwa katika ardhi ya taifa lao huko Amerika Kusini.
Bruno amejiunga na Arsenal msimu huu kwa dau la Euro75 milioni akitokea Newcastle United ambapo alionyesha kiwango bora. Alikuwa sehemu ya kikosi cha Arsenal kilichotwa Ngao ya Jamii 2026 baada ya kuichapa Manchester City magoli 3-0 wikiendi iliyopita.
Huu ulikuwa mchezo wa kwanza rasmi akiwa na Arsenal, pia wa kwanza tangu kumalizika kwa Kombe la Dunia 2026 ambapo Brazil ilitolewa hatua ya 16 bora na Norway kwa kufungwa magoli 2-1.
Katika mchezo huo, Bruno alikosa mkwaju wa penalti, kitu ambacho kilipelekea kutupiwa lawama nyingi na mashabiki lakini mkewe Ana alijitokeza mtandaoni akiandika ujumbe mrefu Instagram akimtia moyo kwa kawama, matusi na kejeli alizopokea kutoka kwa baadhi ya mashabiki.
"Soka lina uwezo wa kukupeleka mbinguni na kuzimu kwa kasi ileile na kwa kiwango kilekile. Katika mechi hizi ya mwisho, tuliweza kuishi mbinguni. Nilimuona mume wangu akitimiza ndoto zake na kulia kwa furaha. Niliiona familia yetu ikiwa katika furaha kubwa, wakwe zangu wakiwa wamejaa fahari, na watoto wangu wakifurahi kila walipomuona kwenye televisheni," aliandika Anna.
"Tulikuwa mbinguni na lengo lilionekana kuwa karibu kabisa kutimia. Lakini mchezo huu unaoitwa soka, ni rahisi sana kushuka kutoka juu kwenda upande mwingine.
"Kutoka ndani ya moyo wangu, namshukuru kila mtu ambaye ametenga hata dakika moja ya muda wake kututumia ujumbe wa upendo, faraja na kututia moyo. Inauma sana, inauma hadi kwenye nafsi, lakini hii ni sehemu ya mchezo.
"Kwa miaka mingi tumejifunza namna ya kukabiliana hisia na hasira kali za mashabiki. Tunaelewa kwamba hakuna mtu ambaye ni mzuri kiasi wanavyosema, kama ambavyo hakuna mtu ambaye ni mbaya kiasi wanavyosema.
"Ni jambo linaloeleweka kwamba watu hujaribu kumtafuta mtu wa kumlaumu, kwa sababu hilo huwasaidia kukabiliana na maumivu na kukatishwa tamaa kunakotokana na kushindwa. Tumeshazoea kupitia nyakati ngumu na tupo tayari kukabiliana na dhoruba nyingine tena tukiwa pamoja.
"Kwa mume wangu, ninachoweza kusema ni jinsi ninavyovutiwa na ujasiri wako na kujitolea kwako uwanjani. Wewe ndiye fahari ya maisha yangu, asante kwa kuniruhusu kuishi nawe katika nyakati hizi zisizosahaulika.
"Asante kwa kuwa nguzo ya familia yetu. Asante kwa moyo wako mzuri kama wa mtoto mdogo. Najua inauma sana lakini kila mvua inaponyesha huwa ni lazima ikatike. Kwako mapenzi ya Mungu bado ni mema, kamili na yenye kupendeza."
Bruno na Ana walianza kuonekana pamoja mwaka 2020 ingawa haijulikani ni lini hasa uhusiano wao ulianza. Walipata mtoto wao wa kwanza aitwaye Matteo mnano Oktoba 2022, baadaye alipata mtoto mwingine wa kiume, Pietro ambaye alizaliwa Machi 2024.
Juni 2023, Bruno na Ana walifanya uamuzi muhimu katika maisha yao, nao ni kufunga ndoa, tukio ambalo lilifanyika katika sanamu maarufu la Kristo Mkombozi (Christ the Redeemer), moja ya alama kubwa na maarufu katika jiji la Rio de Janeiro nchini Brazil.
Ana alikulia Curitiba, Brazil, katika familia inayopenda sana soka, wazazi wake wote ni mashabiki wa mchezo huo, hivyo soka lilikuwa sehemu ya maisha ya familia yao tangu akiwa mdogo.
Muda mfupi baada ya Bruno kujiunga na klabu ya Lyon akitokea Athletico Paranaense ya nchini kwao mwaka 2020, ndipo mrembo huyo naye alihamia Ufaransa ili kuendelea kumpa sapoti huku ikiwa ni mara yao ya kwanza kuishi barani Ulaya.
Tangu wakati huo, wawili hao amezoea maisha ya Ulaya na amekuwa akisafiri katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya utalii na mapumzikoni hasa ya mwishoni mwa msimu wa ligi.
Waliwahi kutembelea eneo la Cassis, kusini mwa Ufaransa, ambako walikodisha boti kwa ajili ya mapumziko yao, vilevile walitembelea Courchevel, eneo la kifahari ambalo ni maarufu kwa michezo ya kuteleza kwenye barafu ambalo lipo kusini mashariki mwa Ufaransa.
Mbali na kuwa mke wa Bruno na mama wa familia yenye watoto wawili, Ana anafanya kazi zake binafsi akiwa kama mtaalamu wa lishe na mazoezi kwa sababu amesomea taaluma hiyo hadi ngazi ya shahada. Mara kadhaa kupitia mitandao ametoa elimu kuhusu umuhimu wa lishe bora na mazoezi ya viungo.