Dili la Richarlison Vasco lavunjika
Muktasari:
- Ripoti kutoka Brazil zinaeleza kuwa Vasco ilikuwa ikitarajia kufikia makubaliano na Tottenham kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 29, lakini Richarlison kwa sasa hataki kurejea kucheza nchini kwao.
LONDON, ENGLAND: MSHAMBULIAJI wa Tottenham, Richarlison, amekataa nafasi ya kurejea Brazil kujiunga na Vasco da Gama, huku mipango ya uhamisho huo ikikwama kutokana na kutokuwepo kwa makubaliano ya maslahi binafsi ya mchezaji.
Ripoti kutoka Brazil zinaeleza kuwa Vasco ilikuwa ikitarajia kufikia makubaliano na Tottenham kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 29, lakini Richarlison kwa sasa hataki kurejea kucheza nchini kwao.
Inadaiwa Vasco ilikuwa tayari kumpa mchezaji huyo mkataba wa miaka mitatu na nusu, lakini mazungumzo hayakufikia mwafaka.
Richarlison alijikuta nje ya kikosi cha Tottenham baada ya kukataa kuhamia Everton kabla ya dirisha la usajili kufungwa. Kukwama kwa dili hilo pia kulichangia Tottenham kushindwa kumsajili Iliman Ndiaye.
Baada ya mpango wa Ndiaye kufeli, Tottenham iligeukia kwa Mykhailo Mudryk, lakini naye ameumia mazoezini na anatarajiwa kuwa nje kwa takribani miezi miwili.
Kocha wa Tottenham, Roberto De Zerbi, amesema hana majuto kuhusu namna klabu ilivyoshughulikia suala la Richarlison, ingawa amekiri angependa mambo yaende tofauti.
“Richarlison ni mtu mzuri. Nilizungumza naye sana na nilitumia muda mwingi kujaribu kumshawishi abaki,” alisema De Zerbi.
Kocha huyo aliongeza kuwa anaelewa kilichotokea katika kipindi cha siku 45 zilizopita na kwamba tabia ya Richarlison katika kipindi hicho ndiyo iliyosababisha hali ya sasa.
Richarlison, ambaye alikuwa mfungaji bora wa Tottenham msimu uliopita akiwa na mabao 11 ya Ligi Kuu England, pia amekuwa akichunguza uwezekano wa kuchukua hatua za kisheria ili kuvunja miezi tisa ya mwisho ya mkataba wake.
Wakati huohuo, Tottenham imeanza msimu kwa kusuasua katika safu ya ushambuliaji, ikiwa haijafunga bao katika mechi zake tatu za kwanza za msimu.
Katika sare ya bila mabao dhidi ya Nottingham Forest wiki iliyopita, Spurs haikufanikiwa hata kupiga shuti lililolenga lango.
De Zerbi, hata hivyo, anaamini kikosi chake kina uwezo wa kuzalisha mabao zaidi, huku akimtaka Omar Marmoush kubeba sehemu kubwa ya jukumu hilo.
“Marmoush anacheza vizuri. Nottingham alicheza mchezo mzuri. Alionekana kuwa hatari na alikuwa akishiriki kikamilifu,” alisema.
De Zerbi anaamini Marmoush ana uwezo wa kufunga mabao mengi zaidi kuliko alivyofanya katika misimu miwili iliyopita, akisisitiza kuwa licha ya kutokuwa katika kiwango cha Harry Kane, bado ana uwezo mkubwa wa kufunga.
Kocha huyo pia hakuficha uwezekano wa kumuunganisha Marmoush na Dominic Solanke katika safu ya mbele, akisema wachezaji hao wawili wanaweza kucheza pamoja.