Ezri Konsa ni rasmi Arsenal
Muktasari:
- Konsa, mwenye umri wa miaka 28, ametia saini mkataba wa miaka minne na Arsenal, huku kukiwa na kipengele cha kuongeza mwaka mmoja zaidi. Ada hiyo ina thamani ya pauni 51 milioni pamoja na pauni milioni nne zitakazolipwa kupitia bonasi mbalimbali.
LONDON, England: MABINGWA wa Ligi Kuu England, Arsenal, wamekamilisha usajili wa beki wa kimataifa wa England, Ezri Konsa, kutoka Aston Villa kwa ada ya jumla ya pauni 55 milioni.
Konsa, mwenye umri wa miaka 28, ametia saini mkataba wa miaka minne na Arsenal, huku kukiwa na kipengele cha kuongeza mwaka mmoja zaidi. Ada hiyo ina thamani ya pauni 51 milioni pamoja na pauni milioni nne zitakazolipwa kupitia bonasi mbalimbali.
Konsa alifanyiwa vipimo vya afya Alhamisi kabla ya kukamilisha uhamisho huo, ambao umekuja saa chache kabla ya Arsenal kuanza rasmi kampeni yake ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu dhidi ya Coventry City, timu iliyopanda daraja, katika Uwanja wa Emirates juzi na kushinda kwa mabao 3-0.
Usajili huo pia ni ushindi mkubwa kwa Aston Villa, baada ya Arsenal awali kumthaminisha beki huyo kwa takribani pauni 30 milioni. Konsa alikuwa amebakiza miaka miwili katika mkataba wake na Villa.
Beki huyo hakuwamo kwenye kikosi cha Unai Emery kilichopoteza mchezo wa UEFA Super Cup dhidi ya Paris Saint-Germain wiki iliyopita, baada ya kuwa mapumzikoni kufuatia kumalizika kwa majukumu yake ya Kombe la Dunia.
Katika msimu uliopita, Konsa alicheza jumla ya mechi 48 katika mashindano yote, akifunga mabao mawili na kutoa asisti moja. Villa ilitwaa taji la Europa League na kumaliza nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu England, matokeo yaliyoipa nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2026/27.
Konsa pia alivaa kitambaa cha unahodha katika baadhi ya mechi wakati nahodha msaidizi wa Villa, John McGinn, alipokosekana.
Kwa upande wa timu ya taifa, Konsa alicheza katika kila mchezo wa England kwenye kampeni yake ya Kombe la Dunia, ambapo Three Lions walimaliza nafasi ya tatu. Alianza mechi saba kati ya nane za England, huku kocha Thomas Tuchel akimatumia zaidi akiwa sambamba na Marc Guehi katikati ya safu ya ulinzi.
Mbali na nafasi yake ya beki wa kati, Konsa aliwahi pia kutumika kama beki wa kulia katika ushindi wa England dhidi ya Norway kwenye hatua ya robo fainali.
Usajili wake unatarajiwa kuongeza nguvu na ushindani katika safu ya ulinzi ya Arsenal, wakati kikosi hicho kikianza harakati za kutetea taji la Ligi Kuu na kupambana katika mashindano ya Ulaya msimu huu.