Klay kutua zake Miami Heat, Harden Cleveland
Muktasari:
- Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyanzo mbalimbali, Klay atakuwa mchezaji huru baada ya kumaliza mchakato kuachana na kikosi hicho.
INDIANA, MAREKANI, Klay Thompson, ambaye ni All-Star mara tano wa Ligi ya Kikapu Marekani (NBA) na bingwa wa NBA mara nne, anaripotiwa kuwa anatarajiwa kusaini mkataba na Miami Heat baada ya kufikia makubaliano ya kuvunja mkataba wake na Dallas Mavericks.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyanzo mbalimbali, Klay atakuwa mchezaji huru baada ya kumaliza mchakato kuachana na kikosi hicho.
Katika msimu uliopita alifunga wastani wa pointi 11.7 na ribaundi 2.1 kwa Mavericks, na mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 36, ambaye anashika nafasi ya nne kwa muda wote katika NBA kwa idadi ya ‘three-pointers’ alizofunga, anatarajiwa kuipa Miami uwezo mkubwa wa kufungua uwanja kwa mashambulizi, hasa kwa nyota kama Giannis Antetokounmpo na Bam Adebayo.
Kuondoka kwake ni hatua ya hivi karibuni katika mabadiliko makubwa yanayoendelea kufanywa na Dallas katika kikosi chake na kunaacha wachezaji watano pekee kutoka kikosi kilichoanza siku ya ufunguzi wa msimu miaka miwili iliyopita.
Klay alishinda mataji manne ya NBA akiwa pamoja na Stephen Curry na Draymond Green wakiwa Golden State Warriors. Alitumia misimu yake 13 ya kwanza akiwa Golden State, ingawa alikosa misimu miwili kamili kutokana na majeraha ya goti. Katika misimu yake miwili akiwa Mavericks, alikuwa na wastani wa pointi 12.9 kwa mchezo na alitupa kwa usahihi wa asilimia 39 mitupo kutoka eneo la pointi tatu. Kwa ujumla wa maisha yake ya NBA ana wastani wa pointi 19.6 kwa mchezo na amekuwa na usahihi wa asilimia 41 wa mitupo kutoka eneo la pointi tatu.
Klay alimpita Damian Lillard na kuchukua nafasi ya nne kwenye orodha ya wachezaji waliofunga three-pointers nyingi zaidi katika historia ya NBA mwezi Januari. Kwa sasa ana three-pointers 2,899, akiwa nyuma ya Stephen Curry, James Harden na Ray Allen.
Klay alishindwa kucheza hatua ya mtoano mara mbili pekee katika misimu 11 aliyocheza akiwa Warriors. Cha kushangaza, idadi hiyo ya mara mbili ndiyo aliyokosa kucheza mchujo (playoffs) katika misimu yake miwili pekee akiwa Dallas.
Katika hatua nyingine, James Harden, anaripotiwa kutua Cleveland Cavaliers kwa mkataba wa miaka mitatu wenye thamani ya Dola 97 milioni akitokea Los Angeles Clippers alikodumu kwa miaka mitatu.
Kwa mujibu wa Shams Charania wa ESPN, mchezaji huyo mwenye All-Star mara 11 na aliyewahi kuwa MVP wa NBA 2018 amekubali kutia saini mkataba wa miaka mitatu wenye thamani ya Dola 97 milioni ambao una kipengele kinachompa fursa ya kuchagua kuendelea au kuondoka (player option) katika msimu wa tatu.
Harden aliamua kutotumia kipengele cha kuendelea na mkataba wake Clippers msimu ujao, huku taarifa zikieleza alikuwa akitafuta usalama zaidi wa mkataba wa muda mrefu.