Scholes aichambua United, Carrick atelekezwa
Muktasari:
- United imeanza vibaya msimu huu, ikishinda mchezo mmoja pekee kati ya mitano ya mwanzo ya Ligi Kuu England. Ushindi huo ulikuwa wa mabao 5-2 dhidi ya Ipswich Town, huku ikipoteza dhidi ya Hull City na Manchester City na kutoka sare na Everton pamoja na Fulham.
MANCHESTER,England; MKONGWE wa Manchester United, Paul Scholes, amekosoa uongozi wa klabu hiyo akidai umemuangusha kocha Michael Carrick kutokana na kile alichokiita “ukosefu wa tamaa” katika usajili wa wachezaji wakati wa dirisha la majira ya kiangazi.
United imeanza vibaya msimu huu, ikishinda mchezo mmoja pekee kati ya mitano ya mwanzo ya Ligi Kuu England. Ushindi huo ulikuwa wa mabao 5-2 dhidi ya Ipswich Town, huku ikipoteza dhidi ya Hull City na Manchester City na kutoka sare na Everton pamoja na Fulham.
Mbali na matokeo hayo, United pia iliondolewa mapema kwenye Kombe la Carabao.
Scholes amesema kiwango cha usajili wa United wakati wa kiangazi hakijaonyesha nia ya klabu hiyo ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu.
Baada ya Casemiro kuondoka kwenda Inter Miami na Manuel Ugarte kupata majeraha, United iliwalenga Elliot Anderson na Mateus Fernandes kama baadhi ya chaguo muhimu katika kiungo.
Hata hivyo, Anderson alijiunga na Manchester City akitokea Nottingham Forest kwa ada ya pauni 116 milioni, wakati Fernandes aliichagua Tottenham baada ya klabu hiyo kulipa Pauni 85 milioni.
United pia ilifanya mazungumzo kuhusu Sandro Tonali na Bruno Guimaraes, lakini ikashindwa kufikia ada zilizohitajika. Tonali baadaye alijiunga na Tottenham kwa Pauni 92.5 milioni, huku Guimaraes akienda Arsenal kwa Pauni 75 milioni.
Badala yake, United ilimsajili Carlos Baleba kwa Pauni 70 milioni, ingawa kiungo huyo wa Cameroon bado hajacheza kutokana na majeraha ya kifundo cha mguu.
Andrey Santos naye alisajiliwa kwa pauni 48 milioni, lakini ameanza mchezo mmoja pekee, wakati Youri Tielemans alijiunga kwa pauni 35 milioni. Kipa Karl Darlow alisajiliwa bila ada.
Akizungumza kwenye podcast ya The Good, The Bat & The Football, Scholes alisema usajili huo haujatoa ishara kwamba United inalenga kuwania ubingwa.
“Inasikitisha kusema hivi, lakini Manchester United kwa sasa si klabu inayojaribu kushinda ligi kupitia usajili wake,” alisema Scholes.
Aliongeza kuwa wachezaji waliosajiliwa wanaweza kuimarisha timu kimwili, lakini bado hawajaonyesha uwezo wa kuifanya United kuwa bora zaidi.
Scholes pia alimtaja Anderson kama mchezaji ambaye, kwa mtazamo wake, angeweza kuleta tofauti kubwa zaidi endapo angejiunga na United.
Kwa upande mwingine, mshambuliaji wa kati amekuwa eneo jingine linalotia wasiwasi Scholes na aliyekuwa kiungo mwenzake wa United, Nicky Butt.
United ilionekana kuwa tayari kumruhusu mshambuliaji Joshua Zirkzee kuondoka wakati wa dirisha la usajili, lakini uha misho huo haukukamilika.
Kocha Carrick amekuwa akisita kumtumia Zirkzee kwa kiwango kikubwa wakati Benjamin Sesko hayupo, huku Mholanzi huyo akicheza kama mchezaji wa akiba mara mbili pekee katika Ligi Kuu. Matheus Cunha amekuwa akipewa nafasi ya kuanza kama mshambuliaji wa kati.
Butt amesema matumizi ya Cunha kama namba tisa hayamuwezeshi kucheza katika nafasi yake bora.
“Kumchezesha Cunha kama namba tisa kunamuumiza. Yeye si namba tisa. Hayuko karibu na kiwango chake anapocheza pale,” alisema Butt.
Butt aliongeza kuwa United inategemea zaidi Sesko kama mshambuliaji wa kati, huku akisema Zirkzee bado hajaonyesha kwamba anaweza kuwa suluhisho la nafasi hiyo.
Carrick aliiongoza United kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu msimu uliopita, jambo ambalo limewafanya Scholes na Butt kuhoji kama kocha huyo amepewa usaidizi wa kutosha na viongozi wa klabu.
Scholes alisema Carrick anaweza kuwa amevunjika moyo na namna mambo yalivyokwenda katika usajili wa kiangazi. “Michael lazima awe amesikitishwa sana na yaliyotokea wakati wa kiangazi. Nafikiri nyuma ya pazia anahisi ameangushwa. Kile alichofanya msimu uliopita kilikuwa kizuri sana,” alisema.
Scholes alisisitiza kuwa mwanzo wa msimu ulikuwa muhimu kwa Carrick kujenga msingi wa mafanikio ya msimu mzima.
United imekuwa na mabadiliko kadhaa ya makocha tangu INEOS ya Sir Jim Ratcliffe ichukue usimamizi wa shughuli za soka za klabu hiyo mwaka 2024.
Erik ten Hag alifutwa kazi miezi michache baada ya kupewa mkataba mpya, kabla ya Ruben Amorim kuchukua nafasi yake. Amorim naye aliondoka baadaye.
Butt amesema hali hiyo inaonyesha kuwa matatizo ya United hayawezi kuhusishwa na makocha pekee, bali pia namna klabu inavyoendeshwa katika ngazi ya juu, ikiwamo usajili wa wachezaji na uteuzi wa makocha.
Alikosoa pia kauli ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa United, Omar Berrada, klabu hiyo inalenga kushinda Ligi Kuu ifikapo mwaka 2028.
Scholes naye alitoa wito kwa uongozi kuangalia upya mfumo wa usajili badala ya kuendelea kuwalaumu makocha.
“Sidhani kama tunaweza kuendelea kuwalaumu makocha kila wakati. Huwezi kuendelea kubadilisha makocha kwa kasi hii,” alisema.
Alisema United inapaswa kuwa na uhakika zaidi kuhusu wachezaji inayowalenga badala ya kusajili wachezaji kwa sababu tu nafasi zao zinahitaji kujazwa.
Scholes alidai kuwa klabu hiyo imekuwa ikiridhika na chaguo za tatu, nne au tano katika orodha ya wachezaji wanaowalenga, jambo ambalo amesema halitoshi kwa klabu yenye matarajio ya kushinda mataji.