Serena arejea US Open kwa kishindo
Muktasari:
- Williams, ambaye ni bingwa mara 23 wa Grand Slam, alirejea kwenye mashindano hayo makubwa ambako alicheza mechi yake ya mwisho ya tenisi miaka minne iliyopita, kabla ya kutangaza baada ya US Open 2022 kuwa angeanza kujiondoa kwenye mchezo huo.
NEW YORK, Marekani. NYOTA wa tenisi, Serena Williams mwenye umri wa miaka 44, amerejea kwa hisia kubwa kwenye viwanja vya Flushing Meadows baada ya kuungana na nyota wa Hispania, Carlos Alcaraz, katika mashindano ya mchanganyiko ya US Open.
Williams, ambaye ni bingwa mara 23 wa Grand Slam, alirejea kwenye mashindano hayo makubwa ambako alicheza mechi yake ya mwisho ya tenisi miaka minne iliyopita, kabla ya kutangaza baada ya US Open 2022 kuwa angeanza kujiondoa kwenye mchezo huo.
Hata hivyo, nyota huyo amekuwa akirejea hatua kwa hatua kwenye jukwaa la tenisi, akishiriki Wimbledon na Cincinnati Open mapema mwaka huu, kabla ya kurejea tena kwenye uwanja maarufu wa Arthur Ashe.
Jumamosi iliyopita, Shirikisho la Tenisi la Marekani (USTA) lilitangaza kuwa Williams na Alcaraz, 23, wamepewa nafasi maalumu (wild card) ya kushiriki mashindano ya mchanganyiko ya US Open.
Wawili hao wameingia kwenye mashindano yenye timu 16 za nyota mbalimbali, huku mshindi akitarajiwa kuondoka na zawadi ya Dola milioni moja.
Juzi Jumanne walishuka kwenye uwanja wa Arthur Ashe kwa mchezo wao wa kwanza dhidi ya Lloyd Glasspool na Erin Routliffe.
Hata hivyo, Williams hatashiriki mashindano ya wanawake mmoja mmoja katika US Open ya mwaka huu. USTA ilikuwa imeshikilia nafasi moja ya wild card kwa upande wa wanawake, huku ikiaminika huenda Williams akaitumia, lakini nafasi hiyo baadaye ilipewa Mmarekani Sofia Kenin, bingwa wa Australian Open 2020.
Williams alishiriki Wimbledon katika mashindano ya mmoja mmoja, lakini alitolewa raundi ya kwanza huku akipata majeraha ya goti. Baadaye alijiunga na dada yake, Venus Williams katika mashindano ya wachezaji wawili ya Cincinnati Open.
Huo ulikuwa mchezo wao wa kwanza pamoja tangu US Open 2022, lakini walipoteza kwa Peyton Stearns na Marta Kostyuk kwa seti 6-2, 1-6, 10-8.
Williams pia amewahi kutwaa ubingwa wa US Open katika mchanganyiko. Alifanya hivyo mwaka 1998 akiwa na Max Mirnyi, ambaye kwa sasa ni sehemu ya benchi la ufundi la Aryna Sabalenka.
Takribani miaka 30 baadaye, mashindano hayo yamepanuliwa na kuwa tukio la siku mbili linalowakutanisha baadhi ya mastaa wakubwa wa tenisi duniani, akiwemo Sabalenka na Novak Djokovic.