Tottenham Hotspur yarudi Kwa Gakpo
Muktasari:
- Gakpo, mwenye umri wa miaka 27, tayari ameridhia masharti ya mkataba ambao utamuweka kaskazini mwa London hadi mwaka 2031, iwapo uhamisho huo utakamilika.
LONDON, ENGLAND: Tottenham Hotspur inajiandaa kuwasilisha ofa iliyoboreshwa kwa ajili ya mshambuliaji wa Liverpool, Cody Gakpo, katika harakati za kukamilisha usajili wa nyota huyo wa kimataifa wa Uholanzi.
Gakpo, mwenye umri wa miaka 27, tayari ameridhia masharti ya mkataba ambao utamuweka kaskazini mwa London hadi mwaka 2031, iwapo uhamisho huo utakamilika.
Mshambuliaji huyo wa pembeni amekuwa akipata nafasi kwa shida Liverpool na anaweza kupewa ruhusa ya kuondoka iwapo klabu hiyo itafanikiwa kukamilisha mipango yake ya kuwasajili Ibrahim Mbaye, Bradley Barcola na Jankuba Minteh.
Hali hiyo imeifanya Spurs kuendelea na harakati za kumnasa Gakpo, huku klabu hiyo ikipanga kufanya maboresho makubwa katika safu yake ya ushambuliaji.
Usajili wa Gakpo unatarajiwa kuwa sehemu ya mpango wa Spurs wa kuimarisha safu hiyo, sambamba na harakati za kuwasajili Omar Marmoush na Savinho.
Makubaliano yanaweza kufikiwa ndani ya siku chache zijazo iwapo Tottenham na Liverpool zitafikia muafaka kuhusu ada ya uhamisho wa Gakpo.
JOEL ORDONEZ
Aston Villa imewasiliana na Club Brugge kuzungumzia uwezekano wa kumsajili beki Joel Ordonez, 22, huku kocha Unai Emery akihitaji kuimarisha safu yake ya ulinzi katika wiki ya mwisho ya dirisha la usajili. Villa, ambayo hivi karibuni ilimpoteza Ezri Konsa, inaelezwa kuwa tayari kuwasilisha karibu pauni30 milioni kwa ajili ya Ordonez baada ya Southampton kukataa ofa ya pauni18 milioni kwa Taylor Harwood-Bellis.
ALLAN ELIAS
Manchester City imepiga hatua kubwa katika harakati za kumsajili winga wa Palmeiras, Allan Elias, 22, huku klabu hizo zikielezwa kufikia mwafaka kuhusu ada ya uhamisho. Palmeiras inataka angalau euro40 milioni pamoja na bonasi.City ikitarajiwa kuwasilisha ofa ya euro 40milioni na bonasi nyingine ya euro milioni tano. Makubaliano yanatarajiwa kukamilika ndani ya siku chache zijazo.
JULIAN ALVAREZ
Mtendaji Mkuu wa Atletico Madrid, Miguel Gil Marin, amesema klabu hiyo ilitaka mshambuliaji Julian Alvarez aendelee kubaki, lakini akadai mchezaji huyo amekuwa na “washauri wasiofaa” katika kipindi cha hivi karibuni. Akizungumza na EFE, Marin amesema: “Tunapaswa kuelewa kuwa Julian hajawa na washauri bora katika kuiongoza taaluma yake katika miezi ya hivi karibuni.” Kauli hiyo huenda ikazidisha mvutano katika kambi ya Alvarez na kusababisha wawakilishi wake kushinikiza zaidi kuondoka kwa mchezaji huyo Atletico.
JAMIE GITTENS
Roma imewasilisha ofa ya kumsajili kwa mkopo mshambuliaji wa Chelsea, Jamie Gittens, 22, lakini klabu hiyo ya London imekataa kumruhusu kuondoka Stamford Bridge kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili. Licha ya Roma kuonyesha nia ya kumsajili, Chelsea chini ya kocha Xabi Alonso imeeleza kuwa haina mpango wa kumtoa Gittens kwa mkopo katika dirisha hili.
JEAN-PHILIPPE MATETA
Aston Villa inamuwania mshambuliaji wa Crystal Palace, Jean-Philippe Mateta, huku kocha Unai Emery akitaka kutumia hali ya mkataba wa mchezaji huyo. Mkataba wa Mateta unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu ujao, hali inayoweza kuifanya Crystal Palace kuwa tayari kumuuza badala ya kuhatarisha kumpoteza baadaye bila kupata fedha nyingi.
DAVID RAUM
Manchester United imegeukia kwa beki wa kushoto wa RB Leipzig, David Raum, 28, baada ya kushindikana kwa harakati za kumsajili Lewis Hall. Kocha Michael Carrick anahitaji kuongeza nguvu katika nafasi hiyo kabla ya dirisha la usajili kufungwa, huku Raum akiwa chaguo linalowezekana kutokana na kipengele cha kuvunja mkataba wake kinachohitaji pauni34 milioni pekee.
JOE WILLOCK
Besiktas imeanza mazungumzo ya awali kuhusu uwezekano wa kumsajili kiungo wa Newcastle United, Joe Willock, huku klabu hiyo ikionekana kuwa tayari kumuuza mchezaji huyo. Newcastle inatarajiwa kukubali ofa yoyote kutoka Besiktas inayokaribia thamani ya sasa ya Willock sokoni.
MOISE KEAN
Como inajiandaa kuwasilisha ofa ya euro40 milioni kwa ajili ya mshambuliaji wa kimataifa wa Italia, Moise Kean, baada ya ofa yao ya awali ya euro30 milioni kukataliwa. Kean, aliyewahi kuichezea Everton, tayari amefunga bao katika Copa Italia msimu huu, huku usajili wake ukitarajiwa kuifanya Como kusitisha harakati za kumsajili mshambuliaji wa Chelsea, Liam Delap.
ELJIF ELMAS
Kiungo mshambuliaji Eljif Elmas, 26, anaondoka RB Leipzig na kujiunga na Atalanta kwa mkopo wenye kipengele cha lazima cha kumnunua, huku klabu hiyo ya Serie A ikigharamia mshahara wake. Elmas alijiunga Leipzig mwaka 2024 kwa euro milioni 24 na tangu wakati huo amekuwa akitolewa kwa mkopo mara mbili, Torino na Napoli. Atalanta imelipa euro milioni mbili kwa mkopo huo, huku ada ya kumnunua ikiwa euro12 milioni.
MAURO FURTADO
Girona FC imemsajili beki chipukizi Mauro Furtado, 18, kutoka Benfica kwa ada ya euro milioni moja na kumpa mkataba wa miaka mitano hadi 2031. Furtado, ambaye bado hajacheza mechi ya kikosi cha kwanza, amepewa nafasi kutokana na uwezo alioonyesha katika akademi ya Benfica na anaweza kucheza kama beki wa kati au wa kushoto.