Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ubaya ubwela CAF

CAF Pict

Muktasari:

  • Taarifa kubwa katika hatua hiyo ni kuondolewa kwa mabingwa watetezi, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, iliyoshindwa na Wiliete SC ya Angola. Hata hivyo, vigogo wa soka la Afrika, wakiwamo Esperance, Zamalek na MC Alger, wamefanikiwa kusonga mbele baada ya kupambana katika mechi ngumu.

CAIRO, MISRI: KLABU 16 zitakazoshiriki hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2026/27 zimethibitishwa baada ya kumalizika kwa mechi za raundi ya pili ya awali Jumapili, huku droo ya kupanga makundi ikitarajiwa kufanyika Jumatano jijini Cairo, Misri.

Taarifa kubwa katika hatua hiyo ni kuondolewa kwa mabingwa watetezi, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, iliyoshindwa na Wiliete SC ya Angola. Hata hivyo, vigogo wa soka la Afrika, wakiwamo Esperance, Zamalek na MC Alger, wamefanikiwa kusonga mbele baada ya kupambana katika mechi ngumu.

Droo hiyo itafanyika Oktoba 28, 2026, saa 9:00 alasiri kwa saa za Misri,(sawa na saa 12:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki), katika makao makuu ya Shirikisho la Soka la Misri (EFA), Cairo.

Timu 16 zitagawanywa katika makundi manne yenye timu nne kila moja, huku hatua ya makundi ikitarajiwa kuanza Novemba. Timu mbili za juu katika kila kundi zitafuzu hatua ya robo fainali.

Sundowns, iliyokuwa ikitetea taji lake, ilitolewa na Wiliete SC, klabu ya Angola iliyoanzishwa mwaka 2018. Wiliete ilipata sare ya mabao 1-1 jijini Pretoria, Afrika Kusini, baada ya mechi ya kwanza iliyochezwa Lubango, Angola, kumalizika kwa suluhu. Matokeo hayo yaliipa Wiliete nafasi ya kusonga mbele kwa kutumia kanuni ya mabao ya ugenini.

CA 01

Pamoja na kuondoka kwa Sundowns, Afrika Kusini itawakilishwa na Orlando Pirates, iliyoiangusha African Stars ya Namibia kwa jumla ya mabao 5-0. Pirates ilishinda mechi ya marudiano kwa mabao 4-0.

Misri itakuwa na wawakilishi wawili, Zamalek na Pyramids FC. Zamalek, mabingwa mara tano wa Afrika, ilifuzu baada ya kuiondoa APR FC ya Rwanda, huku Pyramids ikiifunga El Merriekh Bentiu ya Sudan Kusini na kupata tiketi ya hatua ya makundi.

Esperance ya Tunisia, iliyotwaa taji la Afrika mara nne, ilinusurika kutolewa na Swehly ya Libya. Baada ya kupoteza mechi ya kwanza kwa bao 1-0, Esperance ilipambana na hatimaye kushinda kwa mikwaju ya penalti 3-1 na kufuzu.

MC Alger ya Algeria nayo ilifanya maajabu baada ya kufunga mabao matatu bila jibu katika kipindi cha pili, na hivyo kugeuza matokeo dhidi ya Rangers International ya Nigeria. MC Alger ilikuwa imepoteza mechi ya kwanza kwa mabao 2-0.

CA 02

Petro Atletico ya Angola pia ilirejea kwa nguvu baada ya kuifunga Scottland FC ya Zimbabwe mabao 3-0 jijini Luanda na kufuzu kwa jumla ya mabao 3-2.

Morocco itakuwa na wawakilishi wawili, RS Berkane na MAS de Fes. Berkane ilifuzu kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-0 dhidi ya Star Sport Academy ya Sierra Leone, wakati MAS de Fes ilipata ushindi wa mabao 2-1 dakika za mwisho dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast na kusonga mbele kwa jumla ya mabao 3-2.

Club Africain ya Tunisia nayo imerejea hatua ya makundi baada ya kuitoa TP Mazembe ya DR Congo, mabingwa mara tano wa Afrika. Club Africain ilishinda nyumbani kwa bao 1-0 na kufuzu kwa jumla ya mabao 2-1.

Tanzania itakuwa na wawakilishi wake wawili, Simba na Yanga, ambao wamefanikiwa kufuzu hatua hiyo. Sudan pia itawakilishwa na Al Hilal Omdurman, iliyomaliza kazi kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-0 dhidi ya Sidama Bunna ya Ethiopia.

Colombe Sportive ya Cameroon ilifuzu baada ya kuichapa Teungueth FC ya Senegal kwa jumla ya mabao 3-0, matokeo yaliyoipa klabu hiyo nafasi muhimu katika historia ya soka la klabu nchini Cameroon.

CA 03

FC Nouadhibou ya Mauritania iligeuza matokeo baada ya kupoteza mechi ya kwanza dhidi ya FC San Pedro ya Ivory Coast, na kushinda kwa jumla ya mabao 3-2. Huo ni mwendelezo wa mafanikio kwa Nouadhibou, ambayo imefuzu hatua ya makundi kwa mara ya pili katika historia yake.

Horoya AC ya Guinea ilikamilisha orodha ya timu 16 baada ya kuitoa Al Merriekh ya Sudan kwa mikwaju ya penalti, kufuatia sare ya jumla ya mabao 1-1.

Sasa klabu hizo zitasubiri droo ya Jumatano ili kufahamu wapinzani wao katika hatua ya makundi. Mbali na nafasi ya kuwania ubingwa wa Afrika, timu zitakuwa zikilenga pia zawadi nono, kwani bingwa wa msimu wa 2026/27 anatarajiwa kupokea dola za Marekani milioni sita, kiasi kinachotajwa kuwa rekodi katika mashindano hayo.

Timu zilizofuzu ni Al Hilal Omdurman (Sudan), Club Africain (Tunisia), Colombe Sportive (Cameroon), Esperance (Tunisia), FC Nouadhibou (Mauritania), Horoya AC (Guinea), MAS de Fes (Morocco), MC Alger (Algeria), Orlando Pirates (Afrika Kusini), Petro Atletico (Angola), Pyramids FC (Misri), RS Berkane (Morocco), Simba (Tanzania), Wiliete SC (Angola), Yanga (Tanzania) na Zamalek SC (Misri).