Choki anawaambia dansi haijafa, ampongeza Bella
Muktasari:
- Kwa mujibu wa Choki, mafanikio ya Bella yanawapa presha nzuri wasanii wengine wa dansi kuhakikisha nao wanafanya kazi bora zaidi ili kuendelea kushindana kwenye soko la burudani.
MWANAMUZIKI wa Dansi, Ally Choki amesema muziki huo hauwezi kufa na utaendelea kutoa vipaji vitakavyokubalika na mashabiki, huku akimtaja Christian Bella amewapa presha kutokana na shoo yake kali.
Choki alikuwa miongoni mwa mastaa waliohudhuria tamasha la Asante Tanzania lililoandaliwa na Bella kwenye Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam na aliliambia Mwanaspoti watu wengi wamekuwa wakidhani muziki wa dansi umepoteza nguvu, lakini ukweli ni bado upo na unaendelea kukua kupitia wasanii wapya wanaojitokeza kila siku.
“Muziki wa dansi hauwezi kufa milele. Bado unatoa watu wapya wenye vipaji, mashabiki waendelee kuwasikiliza na kuwafuatilia ndipo watajua kuwa muziki huu bado upo sana,” amesema Choki.
Msanii huyo amesema changamoto kubwa ipo kwa mashabiki wenyewe ambao wakati mwingine hukata tamaa mapema bila kuwapa nafasi wasanii wapya kuonyesha uwezo wao katika soko la muziki wa dansi.
“Watu wengi hudhani muziki wa dansi umekufa, lakini si kweli. Wakifuatilia kazi mpya zinazotoka wataona bado kuna nguvu kubwa sana kwenye muziki huu,” aliongeza.
Katika mazungumzo hayo, Choki alimpongeza Bella kwa kuandaa tamasha hilo maalum la kuwashukuru Watanzania waliomuunga mkono tangu alipoanza safari yake ya muziki hadi sasa anapotimiza miaka 20.
Kwa mujibu wa Choki, mafanikio ya Bella yanawapa presha nzuri wasanii wengine wa dansi kuhakikisha nao wanafanya kazi bora zaidi ili kuendelea kushindana kwenye soko la burudani.
“Christian Bella ametupa changamoto kubwa sana sisi wengine wa muziki wa dansi. Akifanya vizuri yeye na sisi tunaanza kuumiza kichwa tufanye nini ili tuwe vizuri zaidi,” amesema.
Mbali na hilo, Choki alizungumzia suala la Bella kupewa uraia wa Tanzania, akisema ni jambo la kawaida na la kujivunia kwa Waafrika, kwa kuwa sanaa haina mipaka na kinachowaunganisha Waafrika ni utamaduni na mapenzi ya muziki.
“Hata mimi nikienda Congo nikapendwa wanaweza kunipa uraia wa Congo nikawa Mkongo, kwa sababu Afrika ni kitu kimoja, tofauti yetu ni nchi tu,” amesema Choki.