FUNGA MWAKA: Yaliyotrendi zaidi burudani Bongo 2025
Muktasari:
- Wapo mastaa waliobadili historia ya maisha yao kwa kufunga ndoa kwa mara ya kwanza, na wapo waliofanya shoo katika majukwaa makubwa, huku wengine wakiendeleza yale waliokwisha kuyafanya.
KUNA mengi yaliyojiri katika kiwanda cha burudani Bongo kwa mwaka huu ambao upo ukingoni kumalizika, lakini si yote yenye upekee na yaliyofanikiwa kuteka mazungumzo ya wengi kwa kiwango kikubwa.
Wapo mastaa waliobadili historia ya maisha yao kwa kufunga ndoa kwa mara ya kwanza, na wapo waliofanya shoo katika majukwaa makubwa, huku wengine wakiendeleza yale waliokwisha kuyafanya.
Sasa yale matukio machache yaliyoibua gumzo kutokana na nguvu ya ushawishi waliyonayo wahusika wake katika tasnia ya burudani nchini, ndio hasa tunaenda kuyaangazia katika makala haya kama ifuatavyo.
Hamisa, Aziz Ki - Ndoa & harusi
Ilianza kama utani, kisha tetesi na hatimaye Februari 16, Miss XXL After School Bash 2010, Hamisa Mobetto akafunga ndoa na aliyekuwa mchezaji wa Yanga SC, Aziz Ki ambaye sasa anaitumikia Wydad AC ya Morocco.
Wakikutanisha tasnia ya mitindo, muziki na michezo, shughuli yao nzima iliteka sana mijadala mitandaoni kuanzia tukio la utolewaji mahari, ndoa kufungwa na harusi yenyewe ambayo ilihudhuriwa na mastaa wengi.
Ndoa yao imekuwa na utulivu na mahaba ya kutosha wakisafiri pamoja sehemu mbalimbali duniani kuanzia Dar es Salaam, Casablanca hadi New York ilipofanyika michuano ya FIFA ya Kombe la Dunia la Klabu 2025.
Mbosso - Simba Day 2025
Katika tamasha la 17 la Simba Day lililofanyika Septemba 10, Mbosso ndiye alipewa jukumu la kutoa burudani akiwa kama msanii kinara ikiwa ni mara ya kwanza kufanya shoo mbele ya mashabiki takribani 60,000.
Akitumia zaidi ya saa moja juu ya jukwaa huku akiuzunguka uwanja na kutoa burudani, kingine kilichowavutia mashabiki na baadaye kugeuka kuwa gumzo ni muonekano wake pamoja na madansa wake.
Muonekano huo wa kama mazombi ulipata nguvu kubwa zaidi hasa kwa dansa wake mahiri, Queen Fraison maarufu kama Bonge la Dada ambaye mtindo wake wa uchezaji nao umekuwa gumzo mwaka huu.
Jux, Priscilla - Ndoa & harusi
Hatimaye Mei 28, katika ukumbi wa The Superdome, ndipo Jux na Priscilla walifanya harusi yao kubwa ikiwa ni kilele cha mfululizo wa sherehe tangu walipofunga ndoa Feb. 7 ikiwa ni miezi minane ya uhusiano wao.
Baada ya kufunga ndoa hiyo Februari 7, walienda Nigeria anakotokea Priscilla kwa ajili ya taratibu nyingine ambazo ziliambatana na sherehe zenye ufahari mwingi kitu kilichochea sana mijadala mtandaoni.
Mpangilio wa tukio zima hadi kufikia tamati ilikuwa ni gumzo huku baadhi wakihoji kuhusu gharama hadi kuibuka madai kuwa Jux amekopa fedha kiasi cha Sh1 bilioni ili kufanikisha hilo, madai aliyoyakanusha vikali.
Rayvanny - Ufunguzi wa CHAN 2024
Katika ufunguzi wa michuno ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi ya Ndani (CHAN) 2024 iliyofanyika mwaka huu, Rayvanny alikuwa msanii pekee wa Bongofleva aliyepata nafasi ya kutumbiza katika hafla hiyo.
Katika tukio hilo lililofanya Agosti 2, Rayvanny alitumbiza kwa nyimbo zake kadhaa ikiwamo Tetema (2018) na Kitu Kizito (2023) ulioshinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) kama Wimbo Bora wa Singeli 2023.
“Ndoto yangu ya kwanza imeshatimia kufanya shoo ya kimataifa kwenye Uwanja wa Mkapa! Sasa ndoto yangu ya wakati huu ni kuujaza uwanja huu. Tunza haya maneno,” alisema Rayvanny baada ya shoo hiyo.
Harmonize, Kajala - Warudiana tena!
Katika birthday party ya kwanza ya mtoto wa Paula na Marioo (Amarah) iliyofanyika Mei 3, Harmonize na Kajala Masanja walionekana pamoja na kuibua gumzo kubwa huku ikionekana kama watu waliorudiana.
Siku iliyofuatia, Harmonize alirejesha picha za Kajala katika ukurasa wake wa Instagram ambazo alikuwa amezificha lakini baada ya muda akaziondoa tena (archive) kisha kimya kirefu kikatawala.
Hata hivyo, wiki hii wamerejea tena kwenye vichwa vya habari baada ya Kajala kuibuka katika shoo ya Harmonize ambaye amesema yupo tayari kumvisha tena pete ya uchumba mrembo huyo, mama wa Paula.
Diamond, Zuchu - Ndoa
Katika hali ambayo haikutegemewa na wengi, usiku wa Juni 1, Diamond katika ukurasa wake wa Instagram alitoa taarifa akidai kuwa alishawahi kufunga ndoa na Zuchu, mwanamuziki mwenzake wa WCB Wasafi.
“Najua kila mmoja ana picha tofauti kabisa kuhusu Diamond Platnumz na kuoa, ila tu leo niwaambie kuwa huyu Diamond alishawahi kuoa, na kuna siku nitawaambia ikawaje,” alieleza Diamond.
Ni ujumbe ulioibua gumzo kubwa sana, sio Bongo tu hata kimataifa huku Zuchu akijitambulisha kama Mrs Diamond Platnumz katika wasifu wake wa Instagram (bio) akithitibisha uwapo wa ndoa hiyo.
Zuchu - Wiki ya Mwanachi 2025
Katika Kilele cha Wiki ya Mwananchi 2025, tamasha la Yanga SC lililofanyika kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam hapo Septemba 12, Zuchu kutokea WCB Wasafi ndiye alikuwa mtumbuizaji mkuu.
Ubunifu wa jukwaa, mtindo wa uchezaji na hata mavazi yake ndio viligeuka mjadala mkubwa huku akipata shangwe kubwa katika nyimbo zake kama Antenna (2024), Amanda (2025), Hujanizidi (2024) n.k.
Zuchu alipata fursa ya kutumbuiza Mwananchi Day zikiwa ni wiki mbili tangu afanye kitu kama hicho katika fainali ya CHAN 2024 iliyopigwa Moi Kasarani, Kenya ikiwakutanisha Madagascar na Morocco.