Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

‘Tiktak’ ya Chama na dabi tamu ya ‘kituko cha mwaka’

KILIPIGWA jana pale Mbweni. Katika uwanja ambao haukuwa kwenye mazingira mazuri. Mwamuzi alitoka Morocco na wasaidizi wake lakini wakaishia kuchezesha kwenye Dimba bovu.

Tuanzie wapi? Tuanzie mbali kidogo. Yanga walizua kituko cha mwaka kwa kwenda kubadilishia nguo zao katika nyumba ya mtu. Umewahi kuisikia duniani hii? Zamani mechi za uswahilini zilikuwa hizi. Mechi za mtaani. Mnakutana kwa tajiri yenu kwenda kubadilisha nguo.

Yanga waliamua kwenda kubadilishia nguo huko. Wakati wa mapumziko wakaenda huko. Mpira ulipoisha wakaondokea huko. Wanajua haifai. Wanajua wataadhibiwa. Lakini nani anajali?

Sasa hivi wala hatutaki kufichana kuna hofu ya timu moja kupulizia dawa katika chumba cha wapinzani ili wachezaji wao wakose nguvu.

Imekuwa hofu maarufu nchini. Kuanzia mechi za kimataifa hadi hizi za ndani. Hakuna anayechukua hatua. Sijui kwa nini tumefika hapa. Aibu iliyoje. Inaonekana mambo haya yapo.

Turudi uwanjani. Kuna mwanzo mzuri ambao Simba wamewahi kuupata katika miaka ya karibuni dhidi ya mtani? Sidhani. Fikiria walicheza mechi tano mfululizo bila ya kuzigusa nyavu za Djigui Diarra. Ni mpaka Jumatano Suleiman Mwalimu alipofunga bao la penalti pale Unguja ndipo hatimaye walizigusa nyavu za Yanga baada ya miaka mingi.

Juzi Simba walicheka na nyavu za Diarra mara mbili ndani ya dakika 10 za mwanzo. Bahati iliyoje.

Bao la kwanza la Libasse Gueye. Bao rahisi lilitokana na ukabaji wa wachezaji wa Yanga. Kuna namna ambavyo nimeanza kufikiria Yanga wanamkosa Dickson Job katika safu ya ulinzi. Anajua kujipanga na anajua njia ambazo mpira utapita.

Kwa muda mrefu sasa Yanga wanacheza bila ya Job na watacheza bila ya Job. Kwa mara ya kwanza tutaiona kombinesheni ya Bakari Mwamunyeto na Ibrahim Bacca.

Tumezoea kuona Job akicheza na mmoja kati ya hawa. Anaweza kucheza na Bacca kwa sababu ndio kombinesheni iliyoaminika zaidi au anaweza kucheza na Mwamunyeto kwa sababu kama ile ya kufungiwa kwa Bacca.

Bao la pili la Simba lilikuwa la video haswa. Ni bao ambalo Simba hawakulitendea haki kwa sababu hauwezi kufunga bao kama lile halafu mechi ikaisha sare au ikaishia katika upande wa timu iliyofungwa. Lingekuwa bao la ushindi lingesisimua zaidi.

Unamsifu kwanza aliyepiga mpira wa pasi, Ellie Mpanzu ambaye alijua kufanya ‘timing’ na mwendo wa Clatous Chota Chama aliyekuwa anaingia katika boksi. Mpira ulipodunda ndipo Chama alipofanya kitu ambacho hauwezi kukirudia. Huwa kinatokea tu kama miujiza. Kitu ambacho haufanyii mazoezi. Kitu ambacho kinatokea pale pale kadri unapofikiria kwa haraka dhidi ya mpira uliodunda.

Ni kama Diego Maradona alipoifunga England kwa bao la mkono pale Uwanja wa Azteca Mexico katika fainali za kombe la dunia Juni 22, 1986.

Kuna jambo linatokea ghafla kiasi kwamba mchezaji baadaye unajiuliza kama unaweza kurudia tena.

Litabakia kuwa miongoni mwa mabao bora kuwahi kufungwa katika mechi za dabi ya Kariakoo nchini. Bahati mbaya halikuwa bao la ushindi kwani muda mchache baadaye Prince Dube aliirudisha Yanga katika safari ya matumaini. Alifunga bao lake la tisa msimu huu baada ya krosi ndefu kutoka upande wa kulia.

Yanga wakarudi tena katika ile nyumba kupeana mikakati. Sijui mmiliki wa ile nyumba ni nani lakini anaonekana kuwa mtu mzito na anayejiamini kweli kweli. Zaidi ya yote nadhani atakuwa Yanga wa kulialia.

Waliporudi kipindi cha pili waliongeza kasi na wakapata bao ambalo lilitokana na hofu yangu kuu. Simba hawana kipa wa kumuamini pale langoni.

Krosi ya Pacome Zouzoua ilitua katika kichwa cha Dube na mpira haukuwa na nguvu sana. Hata hivyo kipa wa Simba, Djibril Kassali aliurudisha mpira dhaifu ndani.

Hauwezi kufanya kosa kama lile katika mechi kama ile. Wachezaji wawili wa Yanga wangeweza kuutumbukiza mpira wavuni. Mwamnyeto na Bacca.

Bahati tu iliangukia kwa Mwamnyeto. Itamchukua miaka mingi kufunga bao jingine rahisi kama lile.

Baada ya hapo kadri dakika zilivyotokomea ndivyo ambavyo kulionekana uwezo wa timu yoyote kuondoka na pointi tatu. Hasa Yanga.

Alain Okello alimuacha Rushine De Reuck na kupiga krosi ya karibu kwa Pacome aliyeukosa mpira huku mlango ukiwa wazi. Kipa alikuwa ameshatoka.

Dube akafanikiwa kuvunja mtego wa kuotea na angeweza kufunga bao la ushindi dakika chache baadae. Upande wa pili Libasse Gueye naye angeweza kufunga lakini akakataliwa na Diarra. Mara ngapi  turudie kusema huenda Diarra ndiye mchezaji muhimu zaidi katika kikosi cha Yanga?

Mpira ulipomalizika Yanga walishangilia Simba akainamisha vichwa chini. Katika mechi kubwa kama hii unawezaje kuongoza mabao mawili na yote yakarudi?

Sawa, imewahi kutokea mara kadhaa huko nyuma lakini bado haijengi uhalali katika mechi ya juzi.

Inawezekana iliwahi kutokea katika mazingira ya kawaida tu lakini ukiutazama msimamo wa ligi kwa sasa Simba walihitaji pointi tatu za juzi kama dawa. Walihitaji pointi tatu kwa ajili ya kupunguza pengo la pointi tano za wananchi.

Baada ya matokeo ya juzi ni wazi kwamba pengo la kiuwezo uwanjani kati ya Simba na Yanga limepungua kwa kiasi kikubwa. Yanga aliwahi kumfunga Simba mara tano mfululizo lakini sasa wana mechi tatu mfululizo hawajaondoka na ushindi.

Wazungu wana msemo wao kwamba ‘nothing last forever’. Hakuna kitu kitakachobakia hivyo hivyo siku zote. Wakati tukiwashtua Yanga timu yao inashuka kiuwezo uwanjani tulikuwa tunapewa majibu mengi yanayohusu namba.

Tatizo la siku hizi watu wa mpira wanakimbilia katika namba zaidi badala ya ukweli ambao unaweza kuuona kwa macho.

Kuna mambo mawili hapa. Simba wamepandisha kiwango chao na Yanga wameshuka kiwango chao kwa kiasi fulani.

Wameshuka kwa kiasi kidogo na sio kiasi kikubwa. Kuna maeneo mengi hayapo sawa.

Unaachana na Khalid Aucho ambaye anaumiliki uwanja unakwenda kumchukua Mohamed Damaro ambaye sio tu hawezi kumiliki ‘tempo’ ya mchezaji lakini pia anakupa mashaka ya kupata kadi nyekundu kwa sababu muda wote anacheza rafu.

Anashindwa kuuzuia mwili wake kutofika katika mwili wa mpinzani.

Simba? Wana afadhali zao za kutosha kwa sasa. Wageni walioletwa wametiwa nguvu.

Na imezidi kugundulika kuwa bora uwe na Chama ambaye umri umekwenda kuliko kuwa na Joshua Mutale aliye fiti.