Ahsante Morocco, tungoje ya Gamondi
Muktasari:
- Wakati ndoa ya Morocco na TFF ikiishia njiani, inakwenda kusitisha utawala wa makocha wazawa, kwani kocha huyo alikuwa na wasaidizi wa kutoka ndani ya Tanzania wakiwamo Juma Mgunda na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ waliokuwa akifanya nao kazi.
ZAMA za kocha Hemed Suleiman ‘Morocco’ katika timu ya taifa zimefikia tamati baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutangaza Novemba 4, 2025 kuwa haitaendelea naye sambamba na benchi nzima la ufundi alilokuwa nalo tangu mwaka jana.
Wakati ndoa ya Morocco na TFF ikiishia njiani, inakwenda kusitisha utawala wa makocha wazawa, kwani kocha huyo alikuwa na wasaidizi wa kutoka ndani ya Tanzania wakiwamo Juma Mgunda na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ waliokuwa akifanya nao kazi.
Itakumbukwa makocha hao ilikuwa ni ajenda ya Rais wa TFF, Wallace Karia ambaye alikuwa na shauku ya kuona baada ya mfululizo wa makocha wa kigeni kuifundisha Stars, basi ajaribu kuwapa nafasi wazawa kuiongoza timu, lakini jambo hilo likaishia njiani.
Morocco ameondoka Stars akiwa ameacha alama isiyofutika ya kuwa kocha mzawa wa kwanza kuiongoza timu hiyo kufuzu fainali za CHAN na AFCON baada ya awali makocha wa kigeni kutamba kuanzia enzi za Mpoland, Slawomir Wolk.
Wolk alikuwa kocha wa kwanza kuipeleka Stars katika fainali za Afcon za mwaka 1980, kisha akafuata Mnigeria, Emmanuel Amunike Afcon za 2019 na Adel Amrouche 2023, wakati katika CHAN alianza Marcio Maximo 2009 na Mrundi Etienne Ndayiragije 2020.
Morocco alianza kwa kuipelekea Stars fainali za CHAN 2024 kisha Afcon 2025 ambazo ameondolewa, huku akikwama katika Fainali za Kombe la Dunia 2026 zitakazofanyika mwakani huko Marekani, Canada na Mexico, lakini akiandika rekodi tamu.
SAFARI ILIANZIA HAPA
Morocco alianza kuifundisha Stars akianza kama kaimu kocha mkuu Januari 19, 2024 timu ikiwa katika Fainali za Mataifa Afrika zilizopita zilizofanyika Ivory Coast akipata nafasi hiyo baada ya kusimamishwa kwa aliyekuwa kocha mkuu Adel Amrouche.
Adel alitangulia kusimamishwa na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na baadaye TFF kwa makosa ya kutoa kauli zenye utata dhidi ya Morocco ikiwa ni siku chache tangu Stars ilipotunguliwa mabao 3-0 katika mechi ya kwanza ya kundi.
Morocco, aliyekuwa msaidizi wa Adel ambaye ni raia wa Algeria, akapewa Stars kuiongoza katika mechi mbili zilizokuwa zimesalia katika michuano hiyo ambapo alianza na sare ya 1-1 na Zambia, kisha kuambulia suluhu mbele ya DR Congo.
Safari ya Stars ikaishia hapo ikimaliza hatua ya makundi ikiwa na pointi mbili, rekodi kubwa, kwani haikuwahi kupata alama kama hizo hapo kabla ukiwa ni mwanzo mzuri wa Morocco akiwa kama kaimu tu ndani ya kikosi hicho.
CHAN FRESHI
Baada ya Stars kuishia hapo zikafuata fainali za Mataifa kwa wachezaji wa ndani (CHAN) ambazo Tanzania ikiwa moja ya mataifa wenyeji ikaonyesha kupanda chini ya Morocco, ikiishia hatua ya robo fainali ambayo haikuwahi kufika hapo kabla na mbaya wa kocha Morocco akawa ni timu ya Morocco ikitung’oa kwa bao 1-0.
Kabla ya hapo Stars ilifanya vizuri hatua ya makundi ikimaliza bila kupoteza ikicheza mechi nne ikishinda tatu na kutoa sare moja wakiwa vinara wa kundi lao B kabla ya kwenda kuishia kwa Morocco ambao walikuwa washindi wa pili kwenye kundi A lililoongozwa na wenyeji Kenya.
Kwenye fainali hizo Stars ilikuwa ya moto ikicheza soka la malengo ikishambulia na kujilinda vizuri, lakini ubora kati yao na Morocco ukaamua kwenye hatua ya robo fainali ambapo taifa hilo ndio lililokwenda kubeba taji hilo mbele ya Madagascar ambao walikuwa wa pili kwenye kundi la Tanzania.
KAMBA YAKATIKIA HAPA
Kibarua cha Morocco kilianza kuharibika Septemba 9, 2025 kilipopoteza mchezo muhimu wa kufuzu Kombe la Dunia ikilala 1-0 nyumbani dhidi ya Niger huku wageni wao wakimaliza pungufu katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar.
Kama haitoshi Stars ikapoteza mchezo mwingine kwenye uwanja huohuo, mashindano hayohayo safari hii waliomtibulia walikuwa Zambia Oktoba 08, kwa bao lilelile 1-0, ikionekana kama imepoteza mbele ya timu dhaifu zaidi.
Matumaini ya Tanzania kufuzu kwenda kushiriki kwa mara ya kwanza fainali za Kombe la Dunia ziliishia hapo lakini haikuwa hivyo tu ilishusha matumaini kwamba benchi hilo la ufundi linatosha kuiongoza Stars kufanya makubwa zaidi, wadau mbalimbali kulishushia lawama wakiona kama halitoshi.
SARE MOJA, VIPIGO VINNE
Kuanzia Stars ilipopoteza mbele ya Morocco kwenye mchezo wa robo fainali ya CHAN, timu hiyo ilicheza mechi tano ikipoteza nne na kutoa sare moja hatua ambayo ilikuwa inawatibua mabosi wa TFF na hata wale wa serikali na presha kuwa kubwa kwa benchi la ufundi la kocha huyo.
MECHI 32 USHINDI 13
Morocco tangu akabidhiwe Stars kuanzia pale alipoichukua timu hiyo kutoka kwa Amrouche, takwimu zinaonyesha kwamba kocha huyo, ameiongoza timu hiyo kwa muda wa mwaka mmoja na miezi 10 kupitia jumla ya michezo 32.
Katika mechi hizo Stars ya Morocco, ilishinda 13, akitoa sare nane na kupoteza 11, lakini akiivusha timu katika fainali mbili kubwa kati ya tatu aliyoiongoza, zikiwamo CHAN 2024, Afcon 2015 na Kombe la Dunia 2026 ambazo alikwamia njiani.
Katika mechi hizo 32 Morocco aliiongoza Stars katika michezo 23 ya mashindano, ambayo alishinda tisa, akitoa sare sita na kupoteza nane huku mechi za kirafiki zikiwa tisa akishinda nne, akitoa sare mbili na kupoteza tatu.
Kwenye mabao takwimu zinaonyesha Stars ya Morocco ilifunga jumla ya mabao 25 lakini ikaruhusu mabao 22, ikiwa na tofauti chanya ya mabao matatu ndani ya michezo 32 ya mashindano yote mpaka anaondoka.
KUFUZU FRESHI
Morocco huenda akahukumiwa kwa Stars kutofuzu fainali za Kombe la Dunia pekee lakini kocha huyo aliivusha Stars kufuzu Fainali za Mataifa Afrika zikazofanyika Morocco na zile za mwaka 2027 ambazo zitafanyikia hapa nchini kwa ushirikiano pamoja na Kenya na Uganda.
TUMAINI KWA GAMONDI
Kikosi hicho sasa kitakuwa chini ya kocha wa mpito, Muargentina Miguel Gamondi ambaye pia ni kocha wa Singida Black Stars akisaidiana na mzawa Ahmad Ally ambapo wawili hao mechi yao ya kwanza itakuwa ni ya kirafiki dhidi ya Kuwait itakayopigwa Novemba 14, huko Cairo Misri.
Baada ya hapo kocha huyo aliyewahi kuinoa Yanga kwa mafanikio akiifikisha makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kupita miaka 25 tangu ilipocheza mara ya kwanza 1998 na kuipeleka robo fainali kabla ya kurudia tena msimu uliopita kutinga makundi.
Uzoefu alionao katika soka la Afrika na hata kwa wachezaji wa Kitanzania kupitia Yanga na Singida aliyoiwezesha kutwaa Kombe la Kagame 2025 na kuifikisha timu hiyo makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu, wengi wanaamini utaibeba Stars.
Hata hivyo, Gamondi atakuwa na kazi ya kufuta unyonge wa Stars katika fainali hizo za 35 za Morocco kwa kuhakikisha angalau timu hiyo inapata ushindi wa kwanza na hata ikiwezekana kuvuka kwenda raundi inayofuata kama ilivyotokea kwa Morocco CHAN 2024 zilizofanyika Tanzania ikishirikiana na Kenya na Uganda na kufika robo fainali.
MSIKIE MOROCCO
Akizungumzia kuondoka Stars, Morocco alisema amekubaliana na uamuzi wa TFF na sasa anabaki kuwa Mtanzania mzalendo, huku akiwashukuru wachezaji na wote alioshirikiana nao wakati wa kuiongoza timu hiyo.
“Kwanza nimshukuru Mungu kwa hatua hii. Nimeupokea uamuzi, nimepokea barua ya kunijulisha huo uamuzi ya TFF, mimi si mtu wa kupambana wala kupingana nao.”