Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hersi hana bahati na mastaa wa Simba, Azam

PUMZI Pict


KAMA kuna kitu ambacho Rais wa Yanga, Hersi Said, anatakiwa ashauriwe sasa ni kuacha kusajili wachezaji kutoka Simba na Azam kwa sababu hana bahati nao. Kinachomtokea Prince Dube kinatosha kabisa kuwa mhuri kwa dhana hii ninayotaka kuijadili hapa.


Hersi aliingia Yanga Desemba 2019 kama makamu mwenyekiti wa kamati ya usajili, akitokea kampuni ya GSM kama mkurugenzi wa uwekezaji. Hii ni baada ya GSM kuingia mazima kama mdhamini wa Yanga, kufuatia kudonyoa donyoa tangu wakati wa tukio la harambee ya kuichangia klabu hiyo lililoitwa KUBWA KULIKO.


Juni 2019. Mwaka 2022 akagombea nafasi ya Rais wa klabu na kushinda, nafasi anayoitumikia hadi sasa. Katika kipindi hicho Hersi amesaini wachezaji watatu kutoka Azam FC na wanne kutoka Simba...alichokipata kutoka kwao ni kidogo kulinganisha na matarajio.

Takwimu nitakazotumia hapa ni za Ligi Kuu Bara pekee. Achana na Mudathir Yahya, ambaye amekuwa staa mkubwa Yanga, lakini huyu hakujiunga moja kwa moja kutoka Azam, bali alisajiliwa na Hersi akitokea mtaani baada ya kumaliza mkataba Azam na kukaa kwa muda akiwa hana timu.


KUTOKA AZAM FC


PUM 01

1. Ditram Nchimbi

Dirisha dogo la 2019/20 Hersi alisafiri hadi Kampala, Uganda kwa ajili ya kumsaini nyota wa Azam FC aliyekuwa kwa mkopo Polisi Tanzania, Ditram Nchimbi. Nyota huyo maarufu kama Duma, alikuwa Kampala na timu ya taifa ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, kwenye mashindano ya CECAFA.

Wakati huo Nchimbi alikuwa wamoto sana. Alitoka kufunga mabao matatu (hat-trick) dhidi ya Yanga kwenye Ligi Kuu Bara.

Pia alitoka kung’ara na timu ya taifa ya CHAN aliyoisaidia kufuzu fainali za mashindano hayo kwa ushindi wa ugenini wa 2-1 dhidi ya Sudan. Usumbufu wake ulisababisha afanyiwe madhambi ya mkwaju wa adhabu ndogo yaliyozaa bao la kwanza, na akafunga bao la pili.

Hersi alitaka kujenga timu ya haraka haraka ili kuiwahi mechi ya watani wao wa jadi, Simba SC, ambao walikuwa na timu bora sana wakati huo. Mechi hiyo ilipangwa kufanyika Januari 4, 2020.

Na kweli, Nchimbi akaisaidia Yanga kupata sare ya 2-2, wakitoka nyuma 2-0. Mechi ya mkondo wa pili ya Machi 8, 2020, Yanga wakashinda kwa bao moja la mkwaju wa adhabu ndogo wa Bernard Morrison....Nchimbi akifanya kazi kubwa ya kufukuza kila mpira.

Baada ya hapo Nchimbi akawa hajulikani anafanya nini uwanjani...sio kufukuza mpira wala kufunga.

Alikaa mwaka mzima bila kufunga hata bao moja...kwenye moja ya mahojiano, yeye mwenyewe akakiri kwamba hakumbuki mara ya mwisho alifunga lini. Mkataba wa miaka miwili ukaisha Desemba 2021, akaondoka akiwa amefunga mabao matatu na asisti 4, katika mechi 49!

PUM 02

2. Salum Abubakary

Baada ya tetesi za zaidi ya miaka 10 kuhusishwa na Yanga, mwaka 2020 picha halisi ikajitokeza. Salum Abubakary akaiomba Azam FC, timu aliyoitumikia tangu 2007, imuache akatafute chamgamoto mpya.

Azam ikakataa...ikamwambia kama kuna timu kaipata, ilete ofa. Siku mbili baadaye Yanga ikapeleka ofa, Azam ikaikataa kwamba ni ndogo...ikamuita mchezaji na kumshawishi kubaki, akasaini mkataba mpya, akabaki.

Lakini Desemba 2021 akaandika tena barua akiomba kuondoka...safari hii Azam haikuwa na pingamizi, ikamruhusu kuondoka...akaenda Yanga. Tangu hapo hadi sasa Sure Boy hajawahi kuwa tegemeo Yanga huku akicheza mechi 66 na kufunga bao moja na asisti tano. Huyu ni kiungo wa ushambuliaji.

PUM 03

3. Prince Dube

Usajili uliochagizwa na hasira za kisasi kufuatia uhamisho tata wa Feisal Salum. Akiwa Azam FC alitajwa kama mchezaji hatari ambaye hajapata timu kubwa ya kumsaidia.

Matarajio yalikuwa akang’are akiwa Yanga, lakini maswali yamekuwa ni mengi licha ya mchango mkubwa katika kuipa Yanga ubingwa wa Ligi Kuu Bara katika msimu wake wa kwanza kuitumikia 2024-25.

Dube wa Yanga alihusika katika mabao 21 katika mechi 30 za Ligi Kuu Bara msimu uliopita, akifunga mabao 13 na kutoa asisti 8. Hizi sio takwimu za kuzichukulia poa hata kidogo hasa ukizingatia kuwa katika ligi nzima alizidiwa na mtu mmoja tu, mfungaji bora wa ligi, Jean Charles Ahoua wa Simba, ambaye alihusika katika mabao 25, akifunga 16 na kutoa asisti 9.

Hata hivyo, ukilinganisha na nafasi nyingi za kufunga ambazo anazipata na kuzipoteza, Dube hajawa yule aliyetarajiwa.

Aliondoka Azam akisema anataka kuchezea timu itakayompa mafanikio kimataifa, lakini kwenye mashindano hayo ndiko ambako amekuwa akipoteza nafasi nyingi zaidi za kuipaisha Yanga, licha ya kuchangia kuifikisha hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.


KUTOKA SIMBA SC


PUM 04

1. Jonas Mkude

Baada ya kuhudumu Simba kwa takribani miaka 15, Jonas Mkude alijiunga na Yanga kwaka 2023.

Kama kuna kitu ambacho Yanga watamkumbuka nacho Mkude ni mechi dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Lakini hakuna alichokifanya zaidi ya hapo. Misimu yake miwili Jangwani iliisha kwa kung’ara katika mechi moja, bila bao wala asisti ya bao.

PUM 05

2. Clatous Chama

Mwamba wa Lusaka mkazi wa Ndola, mzaliwa Nchanga Zambia. Baada ya kufanya mabalaa makubwa katika vipindi viwili tofauti akiwa na Simba 2019 - 2021 na 2022 - 2024, Chama alihamia Yanga kama mchezaji huru akitokea Simba moja kwa moja mwaka 2024.

Lakini maisha yake Jangwani yalifunikwa na nyota iliyoang’ara ya Aziz Ki kiasi kwamba yeye hakuonekana muhimu hata kidogo. Haikushangaza kuona Yanga imemnyima mkataba mpya.

Alicheza mechi 24 za Ligi Kuu, akifunga mabao 6 na kutoa asisti 3. Japo idadi ya mechi inaweza kuonekana kubwa, lakini dakika zake za uwanjani zilikuwa chache sana. Alicheza dakika 910, wastani wa dakika 38 tu kila mechi.

PUM 06

3. Bernard Morrison

Baada ya kuwafanyia uhuni Yanga mwaka 2020 alipohamia Simba na kuwaacha wanyonge, raia huyo wa Ghana alirudi Yanga 2023 baada ya Simba kumtema.

Akacheza msimu mmoja tu, 2023/24 akitumia dakika 650 tu ndani ya mechi 15...huu ni wastani wa dakika 43 kwa mechi.

Akafunga mabao 5 na asisti 4.

PUM 07

4. Mohamed Hussein Zimbwe Jr

Ni mapema sana kumhukumu mchezaji huyu ambaye hadi sasa amecheza mechi moja tu ya ligi.

Hapa nchini kila mtu anaujua uwezo wake, lakini hata hao wengine pia kila mtu aliujua uwezo wao kabla hwajaenda Yanga, lakini hadithi ikawa tofauti wakiwa huko.

Hatuombei naye aporomoke, lakini uelekeo wa wachezaji waliomtangulia uko hivyo. Hapa ndipo pananipa shaka mimi PUMZI YA MOTO.

Kusajili wachezaji kutoka mpinzani wa moja kwa moja kuna faida mbili, kwanza unaimarisha timu yako na pili unambomoa mpinzani.

Hata hivyo, usajili wa aina hii huja na gharama kubwa sana za kifedha. Ili kumshawishi mchezaji kuvuka mpaka, unalazimika kutoa pesa nyingi. Sasa anapokuja kufeli baadaye baada ya kusajiliwa, huleta simanzi sana kwa waliocheza bahati nasibu ya kumsajili.

Pia huongeza chuki na uhasama usio wa kazima baina ya timu. Ndio maana nasema kama kuna mtu yupo karibu na Injinia amwambie aachane hawa wachezaji.