Prime
Ilivyo ngumu kuwapata kina Lamine Yamal Serengeti Boys
MIHEMKO mingi imeanza baada ya Serengeti Boys kufanya mambo yao kule Morocco. Huwa inatokea hivi mara nyingi na huwa tunasikia maneno mengi baada ya timu za taifa kufanya vizuri. Wanasiasa nao huwa wanaunga tela kwa ajili ya kujipatia sifa za hapa na pale.
Utasikia “Hivi kwa nini hawa vijana wasiwekwe pamoja waunde timu ya taifa mwakani au baada ya miaka michache”. Umewahi kuzisikia hizi kauli?
Huwa ni maarufu sana katika mpira wetu. Tunashindwa kuifahamu vema sayansi ya mpira.
Tatizo letu sio vipaji vya vijana. Tatizo letu ni mapokeo ya vijana baada ya hapo. Hawa vijana wanacheza katika timu za kawaida za mtaani ambazo huwa tunaita ‘academy’. Nyingi kati ya hizi haziendeshwi kisasa na hazina hadhi. Ni vile tu makocha wao huwa wanakomaa nao katika jua kali kwa ajili ya kupata kitu.
Tatizo ni baada ya michuano kama hii au baada ya kuonyesha vipaji kama hivi wanadakwa na timu zipi kwa ajili ya kuendelezwa? Hawa madogo wakirudi wanapaswa kudakwa na klabu mbalimbali kwa ajili ya mwendelezo wa ubora wao.
TFF hawana klabu. TFF hawana timu. Wao timu zao ni taifa na huwa zinakusanyika mara chache kwa mwaka. Kwa wenzetu wachezaji kama hawa wanarudi katika klabu zao ambako wanelelewa vizuri kuliko hata katika timu za taifa.
Lamine Yamal katika umri wa miaka 15 alikuwa katika mikono ya Barcelona. Kwanza kabisa aliitwa akitokea Barcelona ya vijana, na michuano inapoisha anarudi katika klabu yake.
Wale vijana wa Morocco na mataifa ya wenzetu yaliyoendelea kisoka Afrika wachezaji wao huwa wanaitwa wakitokea timu za vijana za Marseille, PSG, Anderlecht, Monaco, Parma na kwingineko. Sisi wanatokea katika vituo vya TFF vya pale Tanga na Kigamboni, na wengineo wanatokea katika vituo vya watu binafsi.
Wakati kijana wa Morocco anapandishwa kutoka timu ya vijana Kwenda timu ya wakubwa pale Stuttgart, sisi kijana wetu anahangaika kutafutiwa nafasi Mtibwa. Hajalelewa katika misingi bora ya kukomaa na kucheza soka la kikubwa akiwa mdogo.
Wale wale vijana wa Algeria ambao tuliwafunga katika michuano hii wana nafasi kubwa ya Kwenda kuwa wachezaji bora mbele kuliko vijana wetu. Nani anawaandaa vijana wetu kucheza ligi kuu nje na ndani ya nchi? Wana wakati mgumu.
Kitu pekee ambacho kinaweza kuwafanya imara watusaidie ni Kwenda nje. Kama kuna mawakala wamewaona na watawapeleka nje litakuwa jambo jema. Kwa kutegemea mpira usidhani kama watakuwa bora.
Jaribu kujiuliza, hawa wakubwa zetu wana vijana wao katika timu hii? Katika sayansi halisi ya mpira, hawa vijana walipaswa wawe wametoka wengi katika klabu za Simba, Yanga na Azam. Walau Azam imekuwa ikijitahidi kulea vijana katika misingi.
Wanaoamini kwamba vijana hawa wataunda Taifa Stars bora kwa kurudi nyumbani wakawekwa kambini pamoja wanajidanganya. Wanatakiwa watawanyike wacheze ligi ngumu mbalimbali hapa duniani. Baadaye wakikutana tena watajikuta imara zaidi.
Ukiwaweka kambini kwa pamoja watakuwa wanacheza katika ligi gani? Watakuwa wanacheza na nani? Hakuna mpira wa hivi duniani.
Mchukulie mchezaji kama Alphonce Mabula. Alikuwa katika kituo cha Alliance pale Mwanza na baadaye aliibukia Ulaya. Si ajabu ndiyo maana anatusaidia vema katika kikosi cha timu ya taifa. Alienda kulelewa vizuri Ulaya mashariki na sasa hivi tunaona matunda yake.
Novatus Ibrahim alilelewa vema na Azam ya vijana. Baadaye akacheza ligi kuu akiwa na Biashara Shinyanga kwa msimu mmoja kisha akaibukia Ulaya. Ndio maana anatusaidia katika timu ya taifa.
Na hata huko nje wanapaswa kupambana sana kama wakipata timu. Maisha hayawi rahisi sana. Akina Morice Abraham walicheza katika timu kama hizi za vijana na wakafanya vizuri. Walienda nje wakajaribu kupambana lakini leo wamerudi tena nyumbani.
Kevin John aliwahi kuitwa Mbappe katika timu kama hizi na walau yeye anajikongoja kupambana katika ligi Daraja la kwanza pale Denmark. Wenzake wako wapi? Waliobaki wapo katika timu hizi hizi za ligi kuu na wengine wapo katika timu za Daraja la kwanza. Ubora wao uko wapi?
Hawa vijana wana uwezekano mkubwa wakapoteza ubora wao kama hawatapokelewa katika mikono salama. Wadogo zetu akina Lamine Yamal wanakuwa katika mikono salama katika pande zote mbili. Katika klabu zao na katika timu za vijana. Ndio maana haishangazi kuona wakiibuka kuwa wachezaji bora katika siku za usoni tena wakiwa katika umri mdogo.
Wakitoka katika timu za vijana hawakusanywi. Wanarudi katika klabu zao na kuendelea kuwekwa katika programu za kisasa kwa ajili ya kuwakuza. Sisi baada ya maajabu ya kule Morocco tunaanza kuhangaika na programu za kufikirika ambazo hazipo katika sayansi ya mpira.
Kama tukiweza kuwatoa vijana saba tu wakaenda katika timu mbalimbali za vijana nje ya Tanzania nadhani tutakuwa tumewekeza vilivyo. Wakirudi hapa nchini ni wazi kwamba njia zote mbili hazitafanya kazi.
Kwanza kabisa hauwezi kuwaweka kambini kama timu kwa sababu TFF haimiliki timu ya mpira wa miguu inayoshiriki ligi yoyote nchini. Lakini pia ukiwapeleka katika timu za Ligi kuu bado malezi yao hayawezi kuwa katika ubora unaotakiwa.
Kila la kheri kwao. Ni matumaini yangu kina Kassim Juma wataonekana ‘huko duniani’. Miaka michache ijayo watakuwa tegemeo katika timu yetu ya taifa. Walioendelea katika bara hili huwa wanatumia njia hii ya mkato.