Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Karibu Idrissa uboreshe Bodi ya Ligi

ZENGWE Pict

Muktasari:

  • Mechi hiyo iliahirishwa saa chache kabla ya muda wa kuanza wakati Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji Ligi, maarufu kama Kamati ya Saa 72 ilipodai imelazimika kufanya hivyo kwa maslahi ya mpira na kwa mamlaka iliyopewa na kanuni.

RAIS wa Azam FC, Nassor Idrissa ‘Father’ amechaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) akichukua nafasi ya Steven Mnguto aliyejiuzulu baada ya sakata lililodumu miezi mitatu la uahirishaji kiholela mechi ya watani wa jadi; Simba na Yanga.

Mechi hiyo iliahirishwa saa chache kabla ya muda wa kuanza wakati Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji Ligi, maarufu kama Kamati ya Saa 72 ilipodai imelazimika kufanya hivyo kwa maslahi ya mpira na kwa mamlaka iliyopewa na kanuni.


Simba ndio iliyoanzisha sakata hilo baada ya kutangaza kugomea mechi hiyo ya Machi 8 kwa maelezo kuwa, ilizuiwa kuingia uwanjani kufanya mazoezi mepesi usiku wa kuamkia siku ya mechi. Ilidai isingecheza pambano hilo na mingine hadi waliohusika kuwazuia wachukuliwe hatua.

Na Yanga ikasema itapeleka timu uwanjani kama ratiba inavyoonyesha, ikijenga hoja kuwa kanuni haziruhusu mechi kuahirishwa namna hiyo. Na ikapeleka timu uwanjani ambako hakukuwa na waamuzi. Ikafanya mazoezi ya kuipa joto miili na baada ya dakika 15 ikaondoka, ikitaka ipewe pointi zake.

ZENG 02

TPLB haikujishughulisha na badala yake ikatangaza tarehe mpya, yaani Juni 15 bila ya kushughulikia madai ya Simba ya kutaka wahusika washughulikiwe, wala ya Yanga ya kudai ipewe pointi tatu.

Hali ilipokuwa mbaya ndipo mtendaji mkuu akawaita viongozi wa Yanga kwa mazungumzo, ambayo yaliibua makubwa zaidi; kwamba kumbe agizo la kuizuia Simba isiingie uwanjani lilitolewa na kigogo mmoja wa wizara.

Mazungumzo hayo yakafikia kuanikiana siri kati ya Shirikisho la Soka (TFF) na klabu ya Yanga, huku wadhamini, benki za NBC na CRDB zikiwekwa njia panda. Benki hizo zilishuhudia jinsi waendeshaji mpira wanavyotumia vibaya fedha na kutoheshimu ratiba na kanuni zao.

Hatimaye Rais Samia Suluhu Hassan aliingilia kati na kuitisha kikao ambacho maazimio yake hayakuwahi kuwekwa bayana zaidi ya kusikia Mnguto na Ofisa Mtendaji Mkuu, Almasi Kasongo wameondoka na kuondolewa.

Sakata hilo pia limefuatiwa na kutoongezwa mkataba kwa katibu mkuu wa TFF, Wilfred Kidau, ambaye Yanga ilishinikiza aondolewe wakati sakata lilipokuwa moto.

ZENG 01

Sakata hilo ambalo ni la pili ndani ya miaka michache baada ya lile la kusogeza mechi mbele kiholela na kusababisha isichezwe hadi juhudi za ziada zilipofanyika. Pia mechi baina ya Simba na Kagera Sugar iliyokuwa ifanyike Kagera iliahirishwa saa chache kabla ya muda kuanza baada ya Simba kudai kuwa wachezaji wake walikuwa wagonjwa. Kagera ilienda uwanjani, lakini haikupewa pointi.

Kwa ujumla sakata hilo lilianika uozo mwingi na udhaifu wa Bodi ya Ligi na watendaji wa TFF. Lilionyesha udhaifu katika uwajibikaji, kutokuwapo kwa utawala bora na uholela katika uendeshaji na usimamizi wa mpira wa miguu.

Uahirishaji mechi ulikuwa ni jambo la kawaida na haukuwa unazungatia maslahi ya wadau wa soka, hasa mashabiki, wadhamini na watangazaji ambao wamelipia fedha nyingi kununua haki za kurusha matangazo ya moja kwa moja ya mechi hizo.

Ilibainika pia kuwa Mwenyekiti wa TPLB ndiye pia Mwenyekiti wa Kamati ya Saa 72 na ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi, ambayo katika hali ya kawaida ilitakiwa ndio imsimamie mwenyekiti na sekretarieti yake ya TPLB.

Ilibainika pia kuwa pamoja na Mwenyekiti wa TPLB kuchaguliwa na klabu, hawajibiki kwa mkutano mkuu wa klabu, bali Kamati ya Utendaji ya TFF. Kazi ya klabu ni kumchagua tu.

Mbali na hayo yaliyoibuliwa na sakata hilo, Kamati ya Saa 72 imekuwa ikifungia viwanja kiholela kana kwamba huwa hakuna ukaguzi mwanzoni mwa msimu ambao huhakikisha ubora wa viwanja vinavyotumiwa msimu unaofuata.

ZENG 03

Ni ajabu uwanja kufungiwa baada ya mechi za raundi moja tu. Hapa kuna tatizo kubwa na inawezekana kuleta hisia za ufisadi, lakini TPLB haijawahi kustushwa na ufungiaji viwanja hovyo wakati hutumia fedha zake kutuma watu mikoa mbalimbali kukagua viwanja.

Upo udhaifu mwingi sana ambao ama ulionekana ama haujaonekana wakati wa sakata hilo lakini ukifichuliwa unaweza kuwa mkubwa zaidi ya huo tuliouona.

Haya ndiyo mambo ambayo Idrissa anakutana nayo anapoingia tu ofisi ya Mwenyekiti wa TPLB. Hatumtarajii aingie ofisini na kuendeleza utamaduni huo wa kuendesha mambo kiholela.

Hatutarajii aonekane bora eti kwa kulinda mfumo wa uwajibikaji, uamuzi, muundo wa bodi na mengine mengi, bali kwa kuufumua muundo na mfumo wa sasa na kuunda TPLB mpya itakayokuwa inaweza kusimama kwa miguu yake na yenye muundo unaoheshimu utawala bora na uwajibikaji.

Tunatarajia aiongoze TPLB iwe shirika au kampuni ya kisasa itakayokuwa inagawa gawio kwa klabu za Ligi Kuu na yenye chombo huru cha kuendesha ligi bila kuruhusu walio nje kuingilia kufanya uamuzi.

Miaka 10 ilitosha kuifanya TPLB isimame kwa miguu yake na kuiacha TFF ijikite katika majukumu yake ya msingi ya kuendeleza soka badala ya kusimamia mashindano ya wachezaji waliokwishakamilika kimafunzo (complete players).

Nafasi yako Idrissa ina lawama ambazo ni lazima uzikubali na kuzifanyia kazi ili uimarike kiuongozi na kikubwa zaidi uiboreshe ligi yetu ianze kulingana na sifa za kuwa ya tano kwa ubora wakati uendeshaji wake ni holela.

Karibu sana Idrissa. Sisi tupo kukusifu pale unmapofanya vizuri au kukukosoa utakapoboronga.