Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba wasiposhtuka, propaganda zitawasumbua sana

ZENGWE Pict


KATIKA matokeo ambayo hayakutarajiwa na wengi ni kipigo cha bao 1-0 ambacho Simba ilikipata kutoka kwa Petro Atletico katika mechi ya kwanza ya makundi ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika iliyofanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.


Baada ya kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kuimarisha kikosi wakati wa usajili wa katikati ya mwaka, mashabiki wengi wa klabu hiyo walitarajia kuwa msimu huu hautakuwa na matatizo makubwa kama yaliyoizuia kutwaa Kombe la Shirikisho msimu uliopita.


Maingizo mapya kama Morice Abraham, Wilson Nangu, Yakoub Seleman, Balla Conte, Antony Mligo, Neo Maema na Rushine De Reuck yaliongeza imani kwa mashabiki kuwa Simba ina kikosi imara ambacho kina uwezo wa kufanya makubwa msimu huu kwenye mashindano ya ndani na nje.

Hata kuondoka kwa kocha Fadlu Davids (katikati ya hatua za mwanzo za mechi za awali za Ligi ya Mabingwa), aliyeiongoza klabu hiyo hadi fainali ya Kombe la Shirikisho, hakukuonekana kuwa tatizo kwa kuwa kulikuwa na kocha imara na hivyo kilichohitajika ni msimamizi wao na si kocha.

Hata Simba ilipojiona inahitaji huduma ya Dimitar Pantev ili azibe nafasi ya Fadlu, hakukuonekana kuwa kulitokana na jinsi timu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi ilivyosumbuliwa na Gabarone United katika raundi iliyopita ya Ligi ya Mabingwa.

ZENG 01

Kama kawaida ya propaganda za viongozi, “cha muhimu ilikuwa ni kuvuka kuingia hatua ya makundi” na si mchezo mzuri au mbaya ambao timu iliuonyesha ilipolazimishwa sare kwenye Uwanja wa Mkapa, ambao klabu hiyo huutumia kwa kaulimbiu ya “hatoki mtu kwa Mkapa”.

Na kuteuliwa kwa Pantev kuwa meneja badala ya utamaduni wa kawaida wa kocha mkuu pia kulipokewa na pongezi na sifa nyingi kuwa klabu imeanza kufuata mfumo wa klabu za Ulaya ambazo hutumia mameneja kusimamia kila kitu katika vikosi, ikiwa ni pamoja na maslahi, usajili na shughuli za ujumla za kikosi.

Kile kipigo cha bao 1-0 ilichopewa na mtani wake wa jadi, Yanga, katika mechi ya Ngao ya Jamii kilipokewa kwa mijadala mingi ya jinsi Pacome Zouzoua alivyosemekana ameingilia mchezo kabla ya kuufuata mpira uliotemwa na kipa na kufunga kirahisi.

ZENG 02

Wengi wakajiridhisha kuwa bila “goli la kuotea” la Pacome mechi ingeisha kwa sare na pengine Simba ilikuwa na nafasi ya kuua mchezo katika kipindi cha kwanza kama si washambuliaji wake wasingekosa umakini walipobaki na kipa Djigui Diarra.

Na propaganda hii inataka kuendelezwa katika matokeo ya mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Lakini, kwa jicho la kimpira, Simba ilihangaika kupata ushindi katika mechi dhidi ya Petro Atletico ya Angola.

Tayari propaganda zimeshaanza kuwa Simba ilikuwa na nafasi ya kumaliza mchezo kipindi cha kwanza wakati washambuliaji wake walipopata nafasi mbili za wazi, lakini wakakosa utulivu na hivyo kuzipoteza akiwemo Elie Mpanzu na aliyepewa pasi na Abraham lakini akafanikiwa kumkwepa kipa wa Petro na akaishia kuugongesha mpira kwenye nyavu za pembeni ya goli.

ZENG 03

Kibaya zaidi, lawama zilezile za mashabiki ambazo huenda zikageuka kuwa shinikizo kubwa kwa viongozi sasa zimeshamiri. Siku zote mashabiki huangalia upangaji kikosi kwa kudhani ndio pekee ambao unaweza kuipa timu mafanikio.

Kitu cha pili mashabiki huangalia wachezaji wa akiba wanaoitwa kuingia uwanjani kuongeza nguvu. Kama kikosi hakitakuwa kinacholingana na matarajio yao, basi ushindi hufuatiwa na sifa nyingi kuwa kocha ana mbinu kubwa, kiasi cha kuona hakukuwa na haja ya kuanza na mshambuliaji hata mmoja.

Lakini kikosi hichohicho kikishindwa kuibuka na ushindi ndipo pale zile sifa hugeuka lawama na kasoro, na pengine kuhoji uwezo wa kocha. Ndivyo iliyotokea kwa Pantev baada ya uamuzi wake wa kutoanza na mshambuliaji halisia kutompa matokeo mazuri.

ZENG 04

Katika safu ya ushambuliaji, Simba ina Mukwala, Sowah na Ahoua na wote walianzia benchi hadi katikati ya kipindi cha pili ndipo wawili walipoingizwa kwa nyakati tofauti, lakini wakatumia muda mwingine kuungana na wenzao kulinda lango au kutafuta mipira sehemu ya kiungo.

Timu haikuwa ikijenga vizuri mashambulizi na mara nyingi ilipoteza mipira katikati wakati ilipotaka kupita sehemu ya kiungo kwa kasi, huku Mpanzu akidhibitiwa pembeni ya uwanja asiweze kutuma mipira ya hatari golini.

Kwa ujumla uchakataji mpira wa Simba kuelekea goli la mpinzani haukuwa mzuri na kiungo hakikuweza kukamata mchezo vizuri kiasi cha kuwalazimisha Petro kurudi golini kwao kujilinda.

Badala yake, Petro ndio wakawa wanasonga mbele kwenda golini katika kipindi cha pili, ambacho kwa kawaida mgeni hubaki golini kwake angalau kutafuta sare.

ZENG 05

Ukimuona yule kiungo wa Simba aliyeshindwa kujitoa muhanga kutibua shambulizi wakati Petro wakitokea upande wa kushoto kwa pasi za mguso wa moja moja kwenda kufunga bao lile, unashangaa wale wanaosema kuwa Waangola walifunga bao la bahati kutokana tu na mpira kumgonga beki, hawaoni jinsi mfungaji alivyokuwa na muda mwingi wa kujiandaa na nafasi ya kutosha kuamua apeleke wapi mpira.

Ninajua viongozi wanaweza kuwa na mtazamo tofauti na mashabiki wao na wachambuzi kuhusu matokeo hayo, lakini ni ngumu kwao kueleza bayana kilichojiri kuonyesha wameliona tatizo na wanalishughulikia. Hii ni aina ya propaganda ya kuruhusu mashabiki waongee yao ili lawama zielekezwe kusikostahili.

Idara ya habari ambayo hasa inahusika na propaganda ndiyo ilitakiwa iwaeleze ukweli mashabiki badala ya kuhamishia matarajio kwenye mechi ijayo ya ugenini dhidi ya Stade Malien wiki hii. Mambo yasipokuwa mambo, lawama hizo kwa Pantev zitabebwa kipropaganda kama zilivyo na kuachana na Mbulgaria huyo.

Ni muhimu Simba ikaachana na hizi propaganda na kufanya mambo kisayansi zaidi. Kufungwa ni sehemu ya mchezo, lakini kujua sababu za kufungwa na kuzifanyia kazi ndio uongozi wenyewe.