Sakata la Fei Toto, Azam FC sasa tuwaachie wenyewe
Muktasari:
- Inasemekana malengo makubwa ya Azam msimu huu ndani na nje ya nchi yamesababisha klabu hiyo ya Chamazi, iamue kutoachana na rasilimali zake zote muhimu ili zifanikishe mafanikio ambayo imekuwa ikipishana nayo kwa muda mrefu.
KLABU ya Al Ahly Tripoli inasemekana inaendelea kupandisha dau la fedha ili kuishawishi Azam FC imuachie kiungo wake mshambuliaji, Feisal Salum 'Fei Toto' baada ya juhudi za awali kugonga mwamba.
Inasemekana malengo makubwa ya Azam msimu huu ndani na nje ya nchi yamesababisha klabu hiyo ya Chamazi, iamue kutoachana na rasilimali zake zote muhimu ili zifanikishe mafanikio ambayo imekuwa ikipishana nayo kwa muda mrefu.
Azam, klabu iliyoanzishwa takriban miongo miwili iliyopita na mfanyabiashara maarufu Saidi Salim Bakhresa (SSB), imeshatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara moja msimu wa 2013-2014, wakati ilipokuwa ikimiliki nyota wengi wazawa kama John Bocco, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Aishi Manula, Salum Aboubakar na Aggrey Morris. Pia wa nje kama Kipre Tchetche.
Mara baada ya kuachana na kundi hilo, wengi wakienda Simba ambako waliiwezesha kuachana na unyonge wa kuukosa ubingwa mfululizo, Azam ikapotea katika kinyang’anyiro cha ubingwa. Ikageuka kuwa timu hatari na machachari inayotingisha vigogo, lakini haitwai ubingwa zaidi ya ule wa Kombe la Mapinduzi.
Kwa takriban misimu mitatu hivi karibuni, Azam imeonekana kubadilika na kuutaka ubingwa kwa udi na uvumba, ikisajili wachezaji nyota kutoka kila kona ya Afrika na hata nje, lakini imekuwa ikishindwa kumaliza vizuri. Msimu wa 2023-2024 iliishia nafasi ya pili katika ligi nyuma ya mabingwa Yanga.
Msimu uliopita imerejea tena katika nafasi ya tatu baada ya kuboronga baadhi ya mechi muhimu zikiwemo zile zilizotokana na uamuzi mbovu ambao hutakatishwa kwa jina la ‘makosa ya kibinadamu’ kama yaliyotokea katika mechi ya hivi karibuni iliyoisha kwa sare.
Hata hivyo nia ya dhati ya Azam kuutaka ubingwa inaonekana katika baadhi ya mambo kama kuuboresha muundo wa uongozi na bila shaka utaratibu wa uamuzi, kuleta kocha anayesifika kwa makombe barani Afrika, Florent Ibenge ambaye ameshazifundisha klabu kama RS Berkane, aliyoiongoza kutwaa Kombe la Shirikisho Afrika na Al Hilal ya Sudan.
Jambo lingine linaloonyesha nia ya dhati ya Azam kutaka mafanikio ndani na nje ya nchi ni uamuzi wake wa kuboresha kikosi na zaidi kutomruhusu kiungo wake mshambuliaji Fei Toto kuondoka wakati huu ambao wanaanza vita muhimu zaidi ya kutafuta tiketi ya kucheza robo fainali ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Al Ahly Tripoli imekuwa ikirudi Chamazi kuongeza dau la kumpata Fei Toto, lakini matajiri hao wa Dar es salaam bado hawajashawishika kuachia hazina yao. Ni uamuzi wa busara na wenye malengo kwa klabu na mchezaji mwenyewe.
Iwapo ataondoka dirisha dogo, Fei atakuwa amepoteza nafasi nyingine ya kuonekana katika hatua za juu za mashindano ya klabu Afrika baada ya kupishana na hatua hiyo wakati akitoka Yanga kwenda Azam. Yanga ilifika fainali ya Kombe la Shirikisho iliyowezesha wachezaji wake kuvaa medali na kuimarisha soko la wachezaji kama Stephanie Aziz Ki na Clement Mzize. Atakuwa amepishana na hatua hiyo kwa kuwa ameshasajiliwa Azam kwa ajili ya mashindano ya klabu ya Afrika.
Azam itakuwa imempoteza mchezaji ambaye alishaanza kuizoea timu, ameshakuwa chachu ya ushindi na mmoja wa wachezaji tegemeo kwa vigogo hao wa jijini Dar es Salaam. Nimeona baadhi ya waandishi wakishinikiza Azam imuachie kiungo huyo mshambuliaji wakidai kuwa kama ingekuwa ni mchezaji wa Simba au Yanga anatakiwa kwa fedha nyingi, wachambuzi wangepiga kelele kila siku.
Lakini ni lazima kutambua kuwa klabu zinafanya biashara na pia zinataka mafanikio ili kujenga chapa na hivyo kuvutia wawekezaji na watangazaji wengi zaidi ili watumbukize fedha kuboresha mifuko yao.
Azam inauza wachezaji, inanunua na inalea wachezaji kwa ajili ya mafanikio ya kitimu. Kama kwao ni bora zaidi Fei Toto abaki, ni uamuzi unaotokana na malengo yao. Na kama ni uamuzi aondoke, ni utashi wao na si ukosefu wa fedha unaowalazimisha kufanya hivyo.
Hata Yanga waliamua kutomuuza Mzize kwa sababu kama hizo; kwanza kutokana na malengo yao ndani na nje ya nchi, na pili ni dau waliloweka au thamani waliyoiweka haikufikiwa na waliokuwa wanamtaka. Kwa hiyo, uamuzi wa klabu kumuuza au kutomuuza mchezaji huzingatia mambo mengi. Cha muhimu ni kampuni zao za menejimenti kuheshimu maadili ili kutochanganya wachezaji wao kisaikolojia.
Kampuni za menejimenti za wachezaji na mawakala hutakiwa kuheshimu usiri wa mawasiliano baina yao na klabu ili kutochanganya wachezaji. Baadhi huvujisha taarifa za madau yanayotolewa na klabu zinawazotaka wachezaji ili kuishinikiza klabu inayommiliki kumuachia mchezaji.
Yanga waliamua kuweka msimamo imara kwa Mzize licha ya yule aliyedai kuwa meneja wake kuzungumza sana na vyombo vya habari kuonyesha kuwa kuna dau kubwa limewekwa kwa mchezaji huyo. Suala hilo pia lilijitokeza kwa Azazi Andambwile wakati ilipoonekana kama meneja wake amevujisha habari kuwa hajalipwa fedha za kusaini mkataba, lakini Yanga wakalimaza juu kwa juu baada ya kuona upungufu katika menejimenti.
Hatujui hilo la Fei Toto linavujishwa na nani, lakini uamuzi wa kumuuza au kutomuuza ni lazima uzingatie malengo na mikakati ya Chamazi na si shinikizo la mijadala wala mitandao.