Prime
Kasumba ya nje inavyothibitisha Simba, Yanga ni kubwa kuliko wazawa
NI rahisi sana kufanya jambo lisilo la kawaida na ukiulizwa sababu ya kufanya hivyo, jibu linakuwa rahisi sana; kwamba “mbona Misri wanafanya” au hata “kanuni zetu zinaruhusu.” Siku zote jibu hilo halitakuwa na sababu za msingi za kufikia uamuzi huo. Ndivyo tulivyo ‘Waswahili’ nikirejea neno alilokariri Jenerali Ulimwengu.
Kwamba ni wepesi sana kuiga jambo na kunyooshea kidole wengine waliofanya hivyo bila kujua sababu zilizowafanya wafikie huko. Lakini kwa sababu walifanya, basi dosari zote za uamuzi huo na madhara yake yanakuwa yameondolewa.
Lakini watu haohao ukiwauliza kwa nini hawafanyi jambo jingine muhimu la maendeleo, wanakuwa wepesi kukujibu “huwezi kutulinganisha sisi na wale kwa sababu wenzetu walishaendelea sana”.
Kwa hiyo, ukitaka kuwaelewa unaweza kuumiza kichwa kwa kuwa hawaeleweki ni wakati gani wataiga kitu kwa wengine na wakati gani watajiepusha kuiga.
Ndivyo ulivyo uamuzi mwingine wa kutumia marefa kutoka nje kuchezesha mechi ya watani wa jadi, Simba na Yanga itakayochezwa Mei 3 kwenye Uwanja wa Meja Isamhuyo, Mbweni, jijini Dar es salaam.
Mechi hiyo itakuwa ya pili kwa watani hao kwenye Ligi Kuu ya msimu huu baada ya ile ya kwanza kuisha kwa sare ya bila kufungana kwenye Uwanja wa New Amaan jijini Unguja.
Taarifa ya mamlaka za soka nchini haielezi sababu za kutumia waamuzi hao baada ya ile ya mwisho ya msimu uliopita kuchezeshwa na waamuzi kutoka Misri.
Binafsi, kwa muda mrefu sijawahi kushuhudia matatizo makubwa ya kiuamuzi katika mechi za timu hizo mbili kongwe katika nchini.
Mara ya mwisho kuona wachezaji wakifikia hatua ya kukunjana ilikuwa mwanzoni mwa miaka ya tisini.
Mechi zilizofuata zote hazijawahi kuwa na matukio ya uamuzi yaliyosababisha marefa kushambuliwa.
Kama kungekuwa na matatizo makubwa kiasi hicho, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) wangekuwa na hoja za kuamua kutumia waamuzi kutoka nje.
Lakini makossa yote yanayotokea katika mechi za wawili hao katika miongo zaidi ya minne ni kasoro ndogo ambazo ama zinakuzwa na uchambuzi ambao hupewa nguvu na picha za marudio ambazo, hata hivyo huwa hazitoshelezi kufikia uamuzi wa kusema refa alifanya uzembe au alipendelea.
Kasoro hizo nyingi huwa hazizingatii kanuni kuu ya mpira wa miguu kuwa tafsiri na maoni ya refa ndiyo ya mwisho.
Ndiyo maana wenzetu wanajaribu kila wanachoweza kutumia teknolojia ambayo itamuwezesha mwamuzi wa kati kuona tukio vizuri, kwa kuangalia picha zilizopigwa kutoka pande tofauti, picha za mnato na video zilizopunguzwa kasi ndipo aamue kwa maoni yake kuwa ni faulo au la.
Hata wachezaji hujua kuwa pengine hawakuona tukio vizuri ndio maana hawadiriki kuchukua hatua ya kumvamia mwamuzi pale anapofanya uamuzi ambao kwao wanaona si haki.
Kwa hiyo, hakuna hoja hadi sasa ya kuchukua uamuzi wa kualika wageni waje kuchezesha moja ya mechi za Ligi Kuu eti kwa sababu inazikutanisha klabu zenye hamasa kubwa.
Huku ni kudogosha waamuzi wetu na kuwaondolea kukubalika kwao mbele ya mashabiki. Zaidi ya yote ni uongozi kukwepa kuwajibika kwa uamuzi mbovu wa wazawa ambao kama wangewekewa juhudi za kutosha wao ndio wangekuwa wakialikwa nje kuchezesha mechi kubwa.
Hata Misri ambako baadhi ya mechi zinazoihusu Al Ahly huchezeshwa na waamuzi kutoka nje, kuna taratibu nzuri zimewekwa kufikia uamuzi huo. Kanuni zinataka klabu ndio iombe mamlaka ialike waamuzi kutoka nje kwa ajili ya kuchezesha mechi itakayotaka.
Kwa mfano msimu huu, Al Ahly aliomba mechi zake zote, baada ya kufungwa bao 1-0 na El Mahalla kwenye Uwanja wa Mahalla, zichezeshwe na waamuzi kutoka nje.
Kanuni inataka klabu inayoomba waamuzi kutoka nje ndio iwagharimie.
Na kwa sababu ukiweka wajibu huo kwa klabu kunaweza kutokea njama, Chama cha Soka cha Misri ndicho hulipia gharama hizo na hurudisha fedha zake kwa kuikata klabu iliyoomba waamuzi kwenye mapato yake. Kwa hiyo, si suala la TFF au TPLB kuamua tu kwamba mechi itachezeshwa na waamuzi kutoka nje, bali ni utashi wa klabu na taratibu zilizowekwa ndiyo hutamalaki.
Kwa mujibu wq kanuni zao,iwapo Chama cha Soka cha Misri kitakataa kuagiza waamuzi kutoka nje, kitatakiwa kitoe maelezo ya kina kuhusu uamuzi huo.
Hii yote ni kujaribu kuweka ugumu kwa mamlaka lakini pia kwa klabu kutumia kanuni kiholela na athari zake zitapakae katika Nyanja nzima ya uamuzi.
Kama ambavyo mamlaka zingejitetea kwa kutofanya jambo zuri kulinganisha na mataifa mengine, ndivyo ambavyo na mimi nasema soka letu bado halijafikia kiwango cha kutumia waamuzi kutoka nje.
Hawa waliopo wana uwezo unaolingana na kiwango chetu cha maendeleo na matumizi yetu ya teknolojia.
Kualika waamuzi kutoka nje, tena kwa ajili ya mechi moja tu msimu mzima, tena mechi ya raundi za kati na si zile za mwishoni zinazoamua bingwa, ni kuiga vitu bila ya kutafakari.
Kama mwamuzi Arajiga anaalikwa kwenda nje kuchezesha mechi kubwa za Ligi ya Mabingwa Afrika, iweje ashindwe kuchezesha mechi ya Simba na Yanga?
Huko ni kukosa viongozi thabiti wanaoweza kuwatetea waamuzi wao kila wakati wanaposhambuliwa.
Na kama ninavyosema kila mara, kitendo cha Kamati ya Masaa 72 kukutana kila mara na kuadhibu marefa kwa maamuzi ambayo walifanya kwa maoni yao kulingana na tafsiri ya vitendo walivyoviona uwanjani, kinazidi kuwaaminisha mashabiki wa mpira wa miguu kuwa hakuna waamuzi bora Tanzania na hivyo mechi za watani wa jadi zichezeshwe na wageni.
Fahari iko wapi kwa waamuzi wazawa kama mechi kubwa kama za watani wa jadi zitakuwa zikichezeshwa na waamuzi wageni? TFF inawajibika wapi kama inashindwa kuzalisha waamuzi hata wa kuchezesha mechi kubwa za ndani, achilia mbali hizo za CAF na FIFA ambazo imefikia wakati tuna haiwezekani?
Tumeruhusu wageni 12 kunufaika na rasilimali zilizoko kwenye soka la Tanzania. Na sasa tumeanza kualika wageni waje tena kunufaika na rasilimali za nchi kwa jina la marefa.
Basi kama tunakwenda vizuri katika mambo hayo, ifikie wakati tualike wageni waje nao kutuongoza maana kwao wameendelea sana.
Wanazalisha wachezaji bora wanaojazana Tanzania, wanazalisha waamuzi bora wanaoalikwa Tanzania. Iweje wasialikwe kuja kutuongozea soka letu?