Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kibarua cha Tanzanite Queens Kombe la Dunia 2026

TANZANITE Pict

Muktasari:

  • Ni mafanikio makubwa kwa soka la wanawake Tanzania na hatua inayoonyesha namna mchezo huo ulivyoanza kukua kwa kasi nchini. Tanzania imeungana na mataifa mengine ya Afrika ambayo ni Nigeria, Ghana na Benin.

HATIMAYE ndoto ya muda mrefu imetimia baada ya Timu ya Soka ya Taifa Tanzania kwa Wanawake chini ya miaka 20, Tanzanite Queens kufuzu Kombe la Dunia, fainali zitakazofanyika Septemba 5 hadi 27, mwaka huu nchini Poland.

Ni mafanikio makubwa kwa soka la wanawake Tanzania na hatua inayoonyesha namna mchezo huo ulivyoanza kukua kwa kasi nchini. Tanzania imeungana na mataifa mengine ya Afrika ambayo ni Nigeria, Ghana na Benin.

Lakini pamoja na furaha ya kufuzu, ukweli unabaki kuwa Tanzania ina kazi nzito mbele yake huko Poland. Kombe la Dunia sio mashindano ya kawaida. Ni jukwaa linalokutanisha timu bora kutoka mabara yote duniani zikiwa na maandalizi makubwa, uzoefu wa kimataifa na mifumo bora ya soka la vijana hivyo Tanzania inahitaji kwenda mashindanoni ikiwa imejipanga ndani na nje ya uwanja.

TANZA 01

SAFARI YAO

Safari ya Tanzanite Queens kufuzu Kombe la Dunia mwaka huu ilianzia raundi ya pili baada ya kuitoa Angola kwa ushindi wa jumla wa mabao 7-0, ikishinda mabao 4-0 katika mechi ya kwanza na marudiano ikashinda mabao 3-0.

Ikafanikiwa kutinga raundi ya tatu ikaitoa majirani zao Kenya kwa mikwaju ya penalti 3-1 baada ya mechi mbili baina ya timu hizo kumalizika kwa sare ya bao 1-1 na raundi ya nne ikakutana na Cameroon.

Mambo yalianza kuwa magumu kwenye mechi ya kwanza ya raundi ya nne ambayo ilikuwa ya mwisho, Tanzanite ilipoteza kwa mabao 3-1 kule Cameroon na baadhi ya mashabiki waliikatia tamaa timu hiyo na kuona tayari safari yao imeishia hapo.

Licha ya kukatiwa tamaa timu hiyo ikaibuka kifua mbele na kiufunga Cameroon mabao 2-0 Uwanja wa New Amaan Complex na kuifanya Tanzanite kufuzu Kombe la Dunia.

TANZA 02

REKODI YA SHIME

Kwenye mafanikio hayo nyuma kuna mchango wa makocha waliofanya kazi kubwa ya kuweka rekodi.Miongoni mwao ni Bakari Shime.

Shime ambaye ndiye kocha mkuu wa kikosi hicho anaandika rekodi ya kuwa kocha pekee wa kutoka Tanzania kuzipeleka timu mbili za taifa katika fainali za Kombe la Dunia.

Mara ya kwanza kuipeleka timu Kombe la Dunia ilikuwa mwaka 2022 akiwa na kikosi cha  Serengeti Girls fainali zilizofanyika India.

Kocha huyo alizipeleka timu zote mbili kwa kuifunga Cameroon ile ya mwaka 2022 aliifunga kwa jumla ya mabao 5-1 akiitandika mabao 4-1 ugenini na kumalizia kazi Zanzibar kwa kuifunga bao 1-0.

Kipindi hicho ndio kilitoa wachezaji nyota akiwemo Clara Luvanga ambaye alikuwa mfungaji bora wa mashindano hayo akimaliza na mabao 10.

TANZA 03

TIMU ZINGINE

Jumla ya timu 24 zimefuzu kushiriki fainali ya Kombe la Dunia. Mbali na wenyeji Poland waliofuzu moja kwa moja, timu nyingine 23 zimefuzu kupitia mashindano sita tofauti ya mabara.

Bara la Afrika limetoa timu nne ambazo ni Tanzania, Nigeria, Ghana na Benin, Bara la Asia limeingiza idadi hiyo pia timu hizo ni China, Japan, Korea Kaskazini, Korea Kusini.

Bara la Amerika ya Kaskazini, Amerika ya Kati na Karibiani imeingiza pia timu nne ambazo ni Canada, Mexico, Costa Rica na Marekani.

Amerika ya Kusini (Brazil, Ecuador, Argentina na Colombia),

Kwa Bara la Oceania limeingiza timu mbili (New Caledonia na New Zealand).

Bara la Ulaya limeingiza timu sita ikiwemo wenyeji Poland, Ufaransa, Italia, England, Ureno na Hispania.

Hii ni mara ya kwanza Tanzanite inafuzu kucheza Kombe la Dunia kwa umri huo na katika timu hizo Tanzania pekee ndio timu changa kwenye michuano hiyo.

Kwa Afrika Tanzania na Benin ndio wageni kwenye michuano ya umri huo kwani Ghana inakwenda kucheza Kombe la Dunia mara ya nane baada ya mwaka 2010, 2012, 2014, 2016, 2018, 2022, 2024, huku Nigeria ikifuzu mara 12 (2002, 2004, 2006, 2008, 2010, 2012, 2014, 2016, 2018, 2022, 2024 na sasa 2026).

TANZA 04

KIBARUA KIPO HAPA

Tanzanite imeshafuzu lakini ina kibarua kigumu cha kuvunja rekodi iliyowahi kuwekwa na timu ya Taifa 'Serengeti Girls' na ile ya timu ya taifa ya Wanawake ya Futsal ya kuwa timu pekee za taifa za Tanzania zilizowahi kufuzu Fainali za Kombe la Dunia chini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA).

Sasa kufuzu sio stori tena kwa timu za Tanzania changamoto ipo baada ya kufuzu itafanyaje kuhakikisha inafanya vizuri kwenye michuano hiyo.

Kwenye mashindano ya Futsal ambapo Tanzania na Morocco zilifuzu kwenye ukanda wa Afrika, haikufanya vizuri ikiwa ndio mara ya kwanza kushiriki mashindano hayo duniani.

Tanzania ilimaliza nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi 'C' ikiwa na pointi tatu ilianza kwa kufungwa mabao 10-0 dhidi ya Ureno, ikashinda mabao 4-2 dhidi ya New Zealand na leo imeondolewa kwa kupokea kichapo cha mabao 9-0.

Ukiachana na Futsal pia kwenye kikosi cha Serengeti Girls kilifika hadi hatua ya robo fainali Kombe la Dunia hivyo Tanzanite ina kibarua cha kuhakikisha inafanya vizuri kwenye michuano hiyo mikubwa duniani.

TANZA 05

MAANDALIZI

Kibarua cha kwanza kwa Tanzania ni kuhakikisha timu inaandaliwa mapema. Mara nyingi timu nyingi za Afrika huangushwa na maandalizi ya mwisho, jambo linalozifanya ziende mashindanoni bila utimamu wa kutosha.

Tanzania inahitaji kuweka kambi ya muda mrefu yenye mazingira bora ya mazoezi, lishe na huduma za kitabibu. Wachezaji wanapaswa kupewa muda wa kutosha kujenga maelewano na kuzoea presha ya mashindano makubwa.

Lakini zaidi, timu inahitaji mechi nyingi za kirafiki za kimataifa. Kukutana na timu za Ulaya, Asia au Amerika kutawasaidia wachezaji kuelewa tofauti ya kasi ya mchezo, matumizi ya nguvu na nidhamu ya kiufundi inayotumika katika mashindano ya dunia.

Bila maandalizi hayo, Tanzania inaweza kujikuta kwenye wakati mgumu.

TANZA 06

BENCHI LA UFUNDI

Soka la kisasa, ushindi haupatikani kwa vipaji pekee. Uchambuzi wa wapinzani na mbinu sahihi ni sehemu muhimu ya mafanikio.

Benchi la ufundi lina kazi ya kuhakikisha linafanya uchambuzi wa kina wa timu zitakazoshiriki mashindano hayo. Kila timu ina udhaifu wake na Tanzania inaweza kutumia hilo kupata matokeo mazuri.

Mfano baadhi ya timu za Ulaya hupenda kucheza pasi nyingi na kushambulia kwa kasi pembeni, wakati timu za Amerika Kusini hutegemea zaidi ubunifu wa mchezaji mmoja mmoja.

Tanzania inapaswa kuwa na mfumo wa kucheza unaoweza kubadilika kulingana na mpinzani badala ya kucheza mtindo mmoja kila mechi.

Aidha, mipira iliyokufa inaweza kuwa silaha muhimu. Kona, faulo na mashambulizi ya kushtukiza vinaweza kusaidia Tanzania kupata mabao hata dhidi ya timu kubwa.

TANZA 07

KUJIAMINI

Kwenye mashindano makubwa, presha huwa kubwa. Wachezaji wengi wa Tanzania watakuwa wanacheza Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza, hali ambayo inaweza kuleta hofu.

Tanzania inahitaji kuwajenga wachezaji kuamini kuwa wanaweza kushindana dhidi ya timu yoyote. Mara nyingi timu ndogo huingia uwanjani zikiwa tayari zimefungwa kiakili kwa sababu ya majina makubwa ya wapinzani wao.

Lakini historia ya soka inaonyesha kuwa timu zenye nidhamu, moyo wa kupambana na kujiamini zinaweza kufanya maajabu hata dhidi ya mataifa makubwa.

TANZA 08

NIDHAMU YA ULINZI

Katika mashindano makubwa, makosa madogo huigharimu timu haraka. Tanzania inapaswa kuwa makini zaidi katika safu ya ulinzi.

Timu nyingi za vijana hupenda kushambulia kwa nguvu lakini huacha nafasi nyuma. Katika Kombe la Dunia, kosa hilo linaweza kutokea.

Benchi la ufundi linapaswa kujenga timu inayoweza kujilinda vizuri huku ikitumia nafasi chache zinazopatikana kushambulia kwa haraka.

Mara nyingi kwenye mashindano ya aina hiyo, timu zinazojilinda vizuri huwa na nafasi kubwa ya kufanya vizuri hata kama hazipewi nafasi na wengi.

TANZA 09

TANZANIA IWAKILISHE VYEMA

Nigeria na Ghana zina historia kubwa katika soka la wanawake Afrika, hivyo macho na masikio mengi yatakuwa zaidi kwao. Tanzania inaweza kutumia nafasi hiyo kucheza kwa utulivu.

Kikubwa ni kupambana kwa kila dakika, kutumia nafasi zinazopatikana na kucheza kwa nidhamu kubwa.

Kwa sababu katika soka la vijana, tofauti kati ya timu kubwa na ndogo huwa si kubwa sana kama watu wengi wanavyodhani.

TANZA 10

WASIKIE WENYEWE

Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Oscar Mirambo anasema wachezaji na benchi la ufundi lilifanya kazi kubwa kuhakikisha timu hiyo inafuzu.

"Kitu kikubwa kuanzia sasa ni kutengeneza fikra nzuri muda huu hadi tutakapoenda Poland kucheza mashindano, kuwajenga wachezaji na kufanya maandalizi mazuri."

Kocha mkuu, Bakari Shime anasema "Haikuwa rahisi sisi kufuzu kutokana na ubora wa wapinzani wetu lakini niwapongeze wachezaji wangu wameweza kuvumilia hadi dakika za mwisho hili limeisha na tutakwenda kujiandaa vizuri Kombe la Dunia."